Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa shukrani, maana katika diplomasia tunachojua zaidi ni kushukuru na kushukuru tena kwa kila jambo. Nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye taarifa ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, na kama back bencher kwa mara ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijazungumzia mada zenyewe, naomba kupitia kwako, namshukuru kipekee Mheshimiwa Spika, kwa kunipokea nilipotoka katika Uwaziri na kunipangia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Namshukuru sana Mheshimiwa Spika na nakiri kwamba Kamati hii imepanua sana uelewa wangu wa mambo mengi kuhusu sekta tunazozisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Mwenyekiti wa Kamati yetu, Mheshimiwa David Kihenzile na Makamu wake, Mheshimiwa Eric Shigongo na Wajumbe wenzangu wa Kamati pamoja na Makatibu wetu, Ndugu Anjelina Sanga na Ndugu Chipanda kwa mbeleko kubwa walionipatia na kuniwezesha kujifunza kuwa Mjumbe wa Kamati hii katika kipindi kifupi. Nimejifunza mengi, tumeenda kwenye ziara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa kwenye Posta sikujua kwamba Mheshimiwa Spika uliwachagua Wajumbe wa Kamati hii pamoja na ujuzi wao wa biashara lakini wanajua ku-entertain. Kwa hiyo, nakushukuru kwamba nimejifunza mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, naomba niunge mkono hoja ya Kamati yetu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira pamoja na mapendekezo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wetu. Pia naunga mkono hoja ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kuongeza mchango wangu kwenye maeneo matatu yanayohusu Sekta zetu za Viwanda, Biashara na Mazingira kwa ajili ya tafakuri ya Bunge lako Tukufu na pia kuishauri Serikali yetu sikivu. Kama mwanadiplomasia mmoja alivyosema, yamesemwa mengi, lakini naomba niseme yale ambayo hayakusemwa katika kuweka msisitizo kwa taarifa ya Kamati yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika maeneo matatu. Moja, ni mabadiliko ya viwanda duniani. Kwa lugha ya siku hizi inaitwa fourth industrial revolution. Pia nitajikita kwenye eneo la biashara bunifu, yaani kwa Kiingereza startups. Mwisho nitajikita katika uchumi wa viwanda vya kijani (green industries) lakini kupitia Sera yetu ya Mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati tumepata wasaa wa kutembelea viwanda, tumepokea ripoti za Serikali na mipango iliyonayo. Nafurahi kuwa wote tuliopo hapa leo tunaelewa umuhimu wa viwanda katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Viwanda vinasaidia kutengeneza ajira, kutupatia kazi, lakini napenda sana kuishauri Serikali kutupia jicho na kujiandaa na mabadiliko makubwa ya viwanda ambavyo nimesema yanapewa kipaumbele duniani (fourth industrial revolution). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine tutakuwa na semina, tutaomba watupe semina kuhusu hii, lakini kwa kifupi niseme, tofauti na karne ya 19 na 20, viwanda vya leo vinapigana vikumbo kutengeneza bidhaa zinazohusika sana na electronic na pia zinazoongeza thamani ya bidhaa. Kwa mfano, katika hiyo fourth industrial revolution yameanza kutengenezwa magari yanayotumia umeme, robot na vifaa vya kieletroniki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo, niseme kwamba nchi yetu imejaliwa rasilimali zote katika kwenda njia hiyo ya fourth industrial revolution. Mtakumbuka katika Mkutano wa Davos wa World Economic Forum, Mheshimiwa Rais aliongelea rasilimali tulizonazo. Nchi yetu imebahatika kuwa na nickel, graphite na earth minerals ambazo sasa hivi zinatumika katika kutengeneza viwanda vya sasa vyenye supply chain, na kufanya hivyo, tutajihakikishia nafasi yetu katika mapinduzi ya nne ya viwanda yajayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu startups, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara alitupa faraja kwamba mmeanza kuangalia jinsi ya kupitia sera na kutoa umuhimu kwa zile startups ambazo zaidi zinatumia teknolojia, ubunifu na zenye uwezo wa kuumuka kulinganisha na biashara za kawaida. Nisingependa tukawa tunachanganya kuhusu startups na SMEs. SMEs zinaweza kuwa startups, lakini startups siyo SM’s.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mnavyoona facebook, uber, zote hizo zilianza kama startups, lakini mnaona sasa ziliweza kuendelea kufanya biashara ya hali ya juu. Kwa Watanzania tuna kampuni ambazo zilikuwa kwenye incubators kama Max Malipo, Kopa Gas na Nala, lakini bahati mbaya biashara hizi bado hatujazipa kipaumbele na wala hazina sera. Nchi nyingi zimeweza kuvutia wawekezaji, (financial Investment) katika hizo. Kwa mfano, kama Nigeria sasa hivi wametangaza karibu Dola bilioni 100.37 ambazo zime-attract baada ya kupitisha sheria ya startups. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, pia Mheshimiwa Rais amekuwa mwepesi, anajenga chuo. Ameelekeza tujenge Chuo cha Digital Technology Institute ambacho kitasaidia vijana katika kuendeleza ubunifu na teknolojia na tayari Serikali ya Jamhuri ya Korea imekubali kusaidia kujenga chuo hiki. Kwa hiyo, rai yangu kwa Serikali ni kuifanyia kazi ili tuwe na sera mapema iwezekanavyo, tufungulie fursa kwa vijana wabunifu waweze kubuni na kuvutia mitaji mikubwa kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, lakini siyo wa umuhimu, ni eneo la mazingira. Tuendapo, ajenda ya mazingira na viwanda inaenda sambamba. Nampongeza sana Mheshimiwa Spika kwa kuweza kuliona hili na kuunganisha hizi Kamati ya Viwanda na Biashara na Mazingira. Ila tumekuwa tunaangalia katika upande wa kuchafua mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ya viwanda katika hii inayoitwa nishati jadifu (green energy), nchi nyingi au makampuni mengi kusudi waweze kuwekeza kwenye viwanda vyetu lazima tuzingatie hii green energy. Ndiyo maana inaitwa green energy industries, tuliangalie na tulipe umuhimu. Maana yake hakuna mtu atakayetaka kuwekeza viwanda ambavyo havikidhi masharti ya green energy. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nihimize Ofisi ya Makamu wa Rais wachangamkie fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimekuwa zinatangazwa kwenye mikutano mikubwa, lakini pia kupitia Green Climate Fund na Global Environment Fund. Fedha hizi ni kwa ajili ya nchi zilizoendelea, lakini wawekezaji wetu wa ndani wanaweza kupata fedha hizi ikiwa wanaweza kuwa na viwanda mbali mbali ikiwemo recycling plants. Kwa hiyo, ni wakati wa sasa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira ifungulie fursa za aina hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona biashara ya carbon. Kabla hujanitoa, nilikuwa nasema tumepewe Mwongozo wa Kitaifa wa Biashara ya Carbon. Sijui wangapi wanajua, lakini tumeambiwa pia Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Carbon imekuwa mfano kwenye Mkutano wa COP27. Mimi nataka wote tuweze kujua kwamba hii ni biashara, lakini kampuni za nje ndiyo zimekuwa zinafaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalize kwa kushukuru tena, lakini pia niseme naunga mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)