Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ADAMSON E. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye huu Mpango uliowasilishwa na Waziri wetu wa Fedha. Kwanza nauunga mkono kwa asilimia moa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa hapa nilipofika. Maandiko yameandikwa kwamba Mwenyezi Mungu humpa amtakaye na kumnyima amtakaye. Kwa hiyo, nashukuru kwamba wenzetu ambao wanapiga kelele sana Mwenyezi Mungu aliamua tu kwamba hawa hawafai kwa sasa. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Kwa kuiba.
MHE. ADAMSON E. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niwashukuru wananchi wangu wa Tabora kwa kunichagua kuwa Mbunge wa Tabora Mjini. Pia hawa ndugu zetu wanapoongelea suala la Hapa Kazi Tu, nashindwa kuelewa sijui hawaoni au hata hawasikii kwa sababu unapoongelea kauli mbiu ambayo wewe unaona kwa vitendo inafanyika, mimi nashangaa kama hawaoni hata kama kuna mabadiliko hata ya ukusanyaji kodi tu nayo hawaoni. Kama tunakwenda kwa kauli, mnaelewa kuna viongozi ambao walisemwa kwenye Bunge hili hili, wakatukanwa sana, lakini leo wakaja na kauli mbiu ya siku 100 nyumba za nyasi hamna wakati kwao kuna nyasi nyingi tu lakini leo wanakumbatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mimi nianze kuchangia kwa suala la reli. Sisi ambao tuko Kanda ya Ziwa, suala la reli kwetu ni muhimu sana na siyo tu Kanda wa Ziwa lakini kwa uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. Reli ya kati kwa jinsi ilivyo sasa kuanzia Dar es Salaam kuja Tabora lakini kutoka Tabora kwenda Mwanza, kwenda Kigoma na Mpanda ni chakavu sana na ndiyo maana mara kwa mara reli hii imekuwa na matatizo ya kukatika vipande vipande. Kwa hiyo, lile suala la standard gauge, naiomba Serikali iipe kipaumbele reli hii kwa sababu inasaidia vitu vingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la viwanda, kwa mfano Tabora tulikuwa na Kiwanda cha Nyuzi nimeshawahi kuzungumza hapa ambacho sasa kimekufa kwa sababu ya mwekezaji ambaye hakuwa mkweli. Sasa Mheshimiwa Waziri mhusika nadhani nilizungumza niliongee kwa ufupi kidogo, kile kiwanda yule aliyebinafsishiwa sasa amegeuza godown lakini pia kakifunga. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Viwanda, Tabora tunahitaji sana viwanda kwa sababu raw materials zipo, tunahitaji pia Kiwanda cha Tumbaku kwani inalimwa zaidi Tabora kuliko mkoa mwingine wowote, hakuna sababu ya Kiwanda cha Tumbaku kuwa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wanatabora tunaomba katika kuweka vipaumbele mkikumbuke Kiwanda cha Tumbaku Tabora kwa sababu ndiko zao linakolimwa zaidi. Kwa sasa tuna vile viwezeshi vingi vya kufanya hata ile tumbaku yenyewe ifikiwe kiurahisi. Barabara hii inayokatisha Manyoni maeneo ya Chaya imebaki kama kilomita 82 kufika Tabora Mjini. Kama barabara ile itakuwa imekamilika basi Tabora mtakapokuwa mmetuwezesha Kiwanda cha Tumbaku mtakuwa mmetusaidia. Siyo suala tu la kama wameisaidia Tabora, lakini na uchumi kwa sababu hata wale ambao wanasafirisha tumbaku ile kuitoa Tabora kuipeleka Morogoro ni gharama kubwa lakini pia gharama zile zinafanya wakulima wa tumbaku wanaumia zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora wamekuwa waaminifu sana wote mnafahamu, imekuwa ni ngome ya Chama cha Mapinduzi hata kama wapinzani wanajaribu kubeza lakini ile imekuwa ngome ya Chama cha Mapinduzi. Mkoa wetu wa Tabora watu huwa hawasemi sana wanaenda kwa vitendo. Kwa kuwa hawasemi sana naomba tusiwachukulie upole wao kwa kuwacheleweshea vitu ambavyo vinaonekena kwa macho. Nadhani mnaelewa Tabora ukiwaudhi kidogo unakaa miaka mitano unatoka nje ya ulingo. Tabora katika miaka thelathini haijawahi kumrudisha Mbunge zaidi ya miaka mitano na hizi ni hasira zao. Pamoja na hayo bado hawachagui mpinzani, watamtoa wa CCM wataweka wa CCM kwa maana ya kwamba bado wanaimani na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
MHE. ADAMSON E. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Tabora pia tunarina asali kwa kiwango kikubwa. Naomba tunapoweka mipango hii tuweze kukumbuka hata kuwa na kiwanda kidogo cha kusindika asali Tabora. Si hilo tu, Tabora pamoja na Shinyanga na mikoa inayofuata wafugaji ni wengi sana, ngozi inayopatikana kule, viwanda kama leather goods lakini pia viwanda vya kusindika nyama vinahitajika kule. Maana ili uwe na viwanda pia ni vizuri kama kile kiwanda kiwe ni kiwanda ambacho kina faida kwa uchumi wa Tanzania na siyo siasa zaidi. Kitu cha kujiuliza raw materials zinapatikana maeneo yale, Tabora zinapatikana. Kwa hiyo, naomba mtukumbuke kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala lingine ambalo linahusiana na reli hiyohiyo ya kati kutoka Isaka kwenda mpaka Keza na kutoka eneo la Uvinza kwenda Msongati hii ni reli mpya. Reli hii tunaihitaji kwa ajili ya uchumi, tunaihitaji kwa ajili ya kupata maendeleo katika maeneo hayo ambayo kwa kweli ni ngome ya Chama cha Mapinduzi kama nilivyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie reli upande wa hapa Morogoro hasa maeneo haya ya Godegode. Kila mara imekuwa pale ndiyo pana matatizo makubwa, tatizo ni nini kama Malagarasi imeshajengwa? Kama Malagarasi daraja limeweza kufanya kazi nina imani Serikali hata pale Godegode inawezekana. Hata hiyo standard gauge tutakayoitengeneza kwa mujibu wa mpango huu basi isije ikawa tena kufika Godegode yakawa yaleyale. Naomba Waziri anayehusika na hilo aweze kulitilia maanani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nizungumzie…
TAARIFA
MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Haya taarifa Mheshimiwa Mtulia.
WABUNGE FULANI: Aaaaah.
MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimpe taarifa mazungumzaji kwa kutumia Kanuni ya 64(1) (a) amezungumza maneno ambayo siyo sahihi na katika Bunge hili Tukufu Mbunge yeyote hatakiwi ama hapaswi kuzungumza uongo. Mzungumzaji aliyekaa ametoa taarifa za uongo ya kwamba Tabora hakuna Mbunge wa Chama cha Upinzani isipokuwa ni CCM tu wakati humu ndani tuna Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka Tabora. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Huko siyo Tabora ni Kaliua.
MHE. ADAMSON E. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliweke sawa hili labda pengine unajua Kiswahili kina matatizo yake. Mimi ni Mbunge wa Tabora Mjini na hawa wanaongelea sijui Kaliua mimi sijaongelea Kaliua. Nimezungumzia miaka 30 ambayo inahusiana na mjini na huu ni ukweli.
MBUNGE FULANI: Ulisema Tabora.
MHE. ADAMSON E. MWAKASAKA: Narudia Tabora Mjini haijawahi kutokea katika miaka 30 Mbunge akarudi mara mbili. Naomba nieleweke sijaongelea Kaliua kwa hiyo sikusema uongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde zile dakika zangu ambazo imeingia hoja ambayo nayo haikuwa ya kweli. Tunapoongelea hii reli, reli ina matatizo mengine ambayo Serikali bado nadhani haijakaa sawa. Ni vizuri kukumbuka suala la wafanyakazi wa reli, reli hii imekuwa ikihujumiwa mara nyingi sana. Kile kipindi cha transition wakati reli imechukuliwa na wale wawekezaji wa India, wafanyakazi wale walipokuwa wanarudi kujiendesha wenyewe waliahidiwa kulipwa mafao yao ambayo yatakuwa tofauti na mkataba wa mwazo ambayo mpaka leo hayajalipwa kwa wafanyakazi wale. Wafanyakazi wengi wa reli kwa muda mrefu wamekuwa katika kipindi cha malalamiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iweze kufikiria kulipa wale wafanyakazi haki zao stahiki ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na waweze kuipenda kazi yao. Kwa sababu mengine yanatokea inakuwa ni hujuma tu kwa sababu mtu hajaridhika na kitu anachokipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli kuna matatizo wafanyakazi hawajalipwa haki zao ambazo ziliahidiwa na Serikali kwamba akishatoka yule mwekezaji wa Kihindi basi kuna maslahi ambayo watalipwa ambayo wanayapigania mpaka sasa. Nina imani wale wafanyakazi watakapokuwa wamelipwa zile staili ambazo waliahidiwa basi ufanisi katika Shirika letu la Reli la Tanzania utakuwa umeboreka na utakuwa wa kupendezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono kwa asilimia mia moja Mpango huu kama ulivyowasilishwa, ahsante sana. (Makofi)