Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii kuweza kutoa machache kulingana na Taarifa ya Kamati na niishukuru pia Kamati kwa hoja zao na mapendekezo waliyoyatoa na niishukuru kwa ushirikiano wao ambao wamekuwa wakituonesha, wakitupa kama Wizara, ushauri na maoni yao mara nyingi tunauzingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda mbali naomba tu pengine kwa wazo la ujumla katika taarifa ya Kamati mwanzoni wakati anaongelea habari ya Wizara kulikuwa na maazimio sita ambayo yanasema hakuna hata moja pengine ambalo limefanywa kwa ukamilifu. Pengine Kamati na Mwenyekiti utanisadia; moja ya azimio lililokuwepo lilikuwa ni lile la Bodi pamoja na Mabaraza yanayoshughulika na usijali, basi yashughulikie nidhamu za watumishi na wataalam pale wanapokuwa wanaharibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tumelijibu kwa ukamilifu kabisa kwamba hatua zimeshachukuliwa kwenye Bodi ya Udhamini, masuala kumi yameshughulikiwa kati ya hayo makampuni matano yamelipishwa faini, kampuni moja imesitishiwa leseni na wataalam watatu wamepewa onyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda upande wa usajili wa wataalam wa mipango miji, masuala kumi na tano yameshughulikiwa, ambapo wataalam nane wamepewa onyo, wataalam watatu wametozwa faini, kampuni tano zimesimamishwa kufanya kazi na kampuni mbili zinatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Baraza la Taifa la Wapima kuna maonyo pale yametoka manne, lakini Kampuni tano zimefutiwa leseni. Sasa pengine labda ule ukamilifu wa kutekelezwa ni upi, pengine watanisaidia labda sikuweza kueleawa vizuri, lakini tumeyafanya kwa ukamilifu kama ambavyo maazimio yalikuwa yanasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la Mradi wa Uboreshaji wa Milki ambao Wajumbe wamelizungumza na Kamati pia imelisema katika azimio lake, na ndiyo maana pale nikatoa taarifa ya kwamba unapoanzisha mradi wowote unakuwa na malengo, na lengo kuu la mradi huu kama nilivyosema naomba niisome kama ilivyo nisije nikaikosea.

Lengo kuu la mradi ni kuweka miundombinu ya kujenga mifumo, kujenga uwezo wa wataalam na kununua vitendea kazi ili kuwezesha kazi za upangaji, upimaji, umilikishaji kuwa endelevu ikiwemo upimaji wa mipaka ya vijiji na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi. Huwezi kwenda kupima vijiji tu peke yake kabla ujaweka ile mipango, kama huna miundombinu huwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imezungumzia suala la kwamba mifumo ipo katika mikoa miwili na haifanyi vizuri sana na hasa ya Dodoma. Sasa mradi huu unakwenda kuweka mifumo kwa nchi nzima mikoa yote, maana yake ni kwa wataalam wetu sasa kote watakwenda kufanya kazi hii na ule mradi wa kufanya data conversion tumeshakamilisha ramani zote za ardhi na ramani zote za mipango miji kwa asilimia 100. Kinachofuata sasa ni mifumo ili kazi hii iende kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mbali na hiyo mradi huu unakwenda kwenye Mikoa 16, Halmashauri 41; kati ya hizo Halmashauri 41, Halmashauri 34 zinakwenda kutoa hatimiliki milioni moja na kwenda kutoa leseni za makazi milioni moja; halafu Halmashauri saba zinaenda kupimiwa vijiji 250; sasa hii pesa inazungumzwa kama vile inaenda kufanya kazi moja wakati ina kazi nyingi tofauti na ambavyo wanavyofikiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti, kwenye mradi wenyewe kama ulivyo ukienda kwenye kile kipengele cha tatu ambacho ndiyo kinajumuisha kama miundombinu, ukienda unangalia mradi mmoja baada ya mwingine kipengele kimoja baada ya kingine kila moja ina kazi ambayo ni compliment ya kile kinachoenda kufanyika finally. Huwezi kwenda kutoa hati tu kabla hujafanya maandalizi mengine. Hati ni final product baada ya haya mengine yote yamekuwa yamefanyika. Upimaji unakuwa umefanyika na kila kitu kinakwenda, ukiangalia hapa wanapozungumza ofisi 25 kwa mikoa yote zinaenda kujengwa na ile mifumo sasa ya muunganiko wa taarifa za wamiliki wa ardhi zinakwenda kuingia katika ile mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia pia kuna suala la kununua vitendea kazi kila tulikopita Halmashauri zinalalamika hazina vitendea kazi, havina magari unakwendaje kupima kule huwezi kumfikisha yule mtaalam kwenye eneo. Kwa hiyo, kuna vitendea kazi ikiwemo pamoja na magari kwa ajili ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo bado kuna ku- support Mabaraza, tumesema Mabaraza hayafanyi kazi vizuri, mradi huu unakwenda kuboresha Mabaraza kuweza kuyapa vitendea kazi, waweze kuboresha kazi zao na Mabaraza ambayo yanazungumzwa kwamba hayajafika katika Wilaya zote, Mabaraza yamefika Wilaya zote 139 kwa maana ya kuundwa, lakini katika utendaji wake ni Mabaraza 88 ambayo ndiyo yana Wenyeviti wa Mabaraza, lakini hakuna ambalo alihudumiwi kwa sababu unakuta Mwenyekiti mmoja anahudumia labda Wilaya mbili. Ukichukua kwa mfano hapa Dodoma tunao Wenyeviti wawili, mmoja anahudumia pia Kongwa na Bahi mwingine anahudumia Mpwapwa ahaa sorry Mpwapwa na Kongwa, huyu mwingine anahudumia hapa Bahi, Kondoa ndiyo linajitegemea.

Mheshimiwa Mwneyekiti, kwa maana hiyo nikwamba kote wanafikiwa, lakini cha msingi tu nikwamba tuna upungufu wa hao Wenyeviti ambao tayari kuna Wenyeviti 34 ambao wanahamia kutoka kwenye Idara tuliomba hapa, tuliomba katika Wizara kwamba wale ambao ni wanataaluma waweze kuja kwa ajili ya ku- support, tayari 34 wamepatikana, kwa hiyo wakija katika ile 55 ambao ina upungufu tutakuwa pia tumepunguza gap na vilevile Bunge hili lilishauri kwamba hawa wanapokuwa na mkataba kazi haziendi vizuri. Sasa hivi walishakubaliwa kuwa waajiriwa, maana yake ni kwamba fursa za kuajiri zikitoka tutakuwa tumeziba gap tena hawa wanaohamia na hawa wengine tutakuwa tayari tumewapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo yale yote ambayo yanaelekezwa na Kamati tunayatekeleza japokuwa yanakwenda hatua kwa hatua kwa sababu huwezi kwenda ukayamaliza yote kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la kodi kwenye masuala mazima ya makampuni kutolipa na mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa nchi hii Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa msamaha kwa watu kulipa kodi bila riba na katika hayo baadhi ya makampuni yameweza kuitikia kati ya makampuni hayo tunayo VETA, tunayo TTCL, tunayo PSSSF, tunayo VETA hizi ni taasisi za Serikali, zimeitikia na kuweza kufaidika katika huo msamaha, lakini bado kama Serikali kuna utaratibu ambao umewekwa kuhakikisha kwamba taasisi zote za umma zinalipa kodi, kwa sababu kodi hiyo hiyo ndiyo inakwenda ku-supplement kwenye matumizi ya Serikali kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachofanya hapa ni kuhakikisha kila hatua inayoelekezwa tunaifanyia kazi, kila hatua, hakuna hata moja ambalo tumeliacha. Kwa hiyo, ninachotaka kusema katika hili, kila ambacho kimetolewa maelekezo tunayafanyia kazi kulingana na maelekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huu mradi pia umekuwa na kelele nitakukabidhi karatasi hii ambayo inaonesha kila item itakavyokwenda kufanyiwa kazi na pesa yake iliyopangwa. Kwa hiyo, ukiipata hii ndio utajua. Maana unapo-combine bila kujua kila kipengele kinafanya kazi gani, huwezi kupata picha halisi. Nitaomba nikukabidhi hii ili pia iweze kukuongoza kuhusu kile ambacho Waheshimiwa Wabunge wanakilalamikia na kile ambacho kimepangwa kwenye mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ambayo yamezungumzwa mengine pia kuhusiana na Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995 ambayo rasimu yake ilikwishakamilika toka Julai, 2021. Sera hii bado haijatoka kulingana na mabadiliko ambayo tunakuwa nayo kwa sababu, tulikuwa tunahitaji pia kuwa na sera ya nyumba, lakini pia tunahitaji kuwa na sera ya makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizo sera kuna mahali ambapo zinaingiliana kutokana na mabadiliko yanavyokuja. Unapokaribisha na wawekezaji na nini, unakuta sera haziwabebi kulingana na jinsi ambavyo matakwa ya nchi yanataka. Kwa hiyo, katika hili tunaendelea na rasimu ambayo inaandaliwa, baadaye tuweze kuja ku-harmonize na wenzetu. Kwa mfano wenzetu wa Mambo ya Nje wanatengeneza Sera ya Diaspora ambayo sasa nao watahitaji masuala ya kuwekeza na kuweza kumiliki wakati mwingine. Sasa hii bila kuwa na sera huwezi kupata, kwa hiyo, lazima tukamilishe hii halafu twende kwenye sheria. Kwa hiyo, haya yote tunayaweka katika ule utaratibu ambao umekubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chege alizungumzia suala la miradi kutokukamilika. Katika ile miradi ya NHC, tuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, wameridhia sasa NHC kukopa pesa na wameshakubaliwa kukopa bilioni 173 ambazo zitakwenda kukamilisha hii miradi ambayo ilikuwa imesimama kwa muda mrefu. Tunachofanya ni mambo mawili; kuna hiyo pesa ya kukopa, lakini kuna hii pesa ambayo imetajwa ya bilioni 47 ambazo ni accrued interest katika mradi ule kusimama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya tutafanya mazungumzo na yule mkandarsi ili kuona tunatokaje katika hili kwa sababu, kama pesa imepatikana maana yake ujenzi utaendelea. Kwa hiyo, masuala ya accrued interest ambayo anatudai basi tunaweza kuona ni jinsi gani tunaweza tukaongea nao na tukaweza kumaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya masuala ambayo yote yamezungumzwa nilitaka nitolee ufafanuzi huo kwa sababu ni mambo ambayo yanahitaji pia kwenda kwa pamoja katika uelewa. Nirekebishe pia, taarifa ya Mheshimiwa Hawa aliposema kwamba, huu mradi haujui ndio ameusikia hapa. Mradi huu ulianza kuandaliwa 2016, tukaanza discussion 2018, mwaka 2021 mradi ukakubalika, mwaka 2022 ukasainiwa na bajeti ya mwaka jana kwenye hotuba ya Waziri na pamoja kwenye randama mradi huu upo na Mbunge alikuwa ni Mjumbe wa Kamati na wala hajabadilishwa yupo. Sasa anaposema anakuja kuusikia hapa, basi niombe tu wakati mwingine tunapotoa taarifa, basi Wajumbe wawe wanazipitia vizuri kuliko kuja kutoa taarifa ambazo sio sahihi katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)