Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwanza kuwashukuru Wenyeviti wote wawili ambao asubuhi ya leo wamewasilisha Taarifa za Kamati zote mbili na taarifa hizi ni muhimu sana. Sisi Wizara tunamshukuru sana Mwenyekiti, Mheshimiwa Makoa pamoja na Mheshimiwa Kihenzile kwa sababu, Kamati hii imekuwa ikitupa mawazo muhimu sana. Tumekuwa tukishauriana namna gani bora ya kuendeleza masuala mazima ya maliasili na utalii, kwa kweli, tunaishukuru sana kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeleta taarifa yake na kuna maeneo mengi Kamati imeelekeza tuboreshe. Kwa hiyo, moja kwa moja niseme kwamba, ushauri wote na maoni waliyotoa tunayapokea, tutayafanyia kazi na tutaendelea kuyawasilisha katika Kamati kama ilivyo ada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo limezungumzwa kwa mfano habari ya bajeti, kwamba, zipo taasisi zilikuwa na mbuga 16, lakini sasa hivi TANAPA inasimamia mbuga 22, TAWA, Ngorongoro, ni namna gani tunaweza tukaongeza mapato ikiwa ni pamoja na retention.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni masuala ya msingi sana, wakati mwingine kunakuwa na majanga ya moto, kwa hiyo, inakuwa ni changamoto kutegemea OC. Katika maeneo kama haya lazima kuwe kuna bajeti ya kutosha ya kuweza kuhimili mikiki. Wageni watalii wanapokuja lazima tuhakikishe madaraja yako salama na barabara ziko salama. Kwa hiyo, Kamati imekuja na ushauri wa msingi kabisa nasi Serikali tumesikia, tunasema haya waliyopendekeza Kamati ni mambo ya msingi na tutayazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imetukumbusha katika taarifa yake na waliochangia kwamba, zoezi la kuhamisha watu kwenye makazi bora kutoka Ngorongoro kwenda Msomera ni jambo ambalo linapaswa kuendelea. Nasi tunasema jambo hili linaendelea, mpaka sasa tumeshahamisha kaya kwa hiyari takribani 551, watu 3,010, mifugo isiyopungua 15,321 na zoezi hili linaendelea. Lengo la kuhamisha kwanza ni kuhakikisha kwamba, watu wetu wanapata makazi bora, wanapata eneo ambalo wataweza kufuga, kulima, vitu ambavyo walipokuwa wanaishi kule Ngorongoro sheria haziruhusu; haziruhusu kilimo, haziruhusu ujasiriamali, kuna vijana wanataka kufanya shughuli za bodaboda, akinamama wafungue shughuli zao, lakini Ngorongoro hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunachokifanya ni suala la haki za binadamu. Tunapozungumzia haki za binadamu ndugu zetu wanaoishi Msomera ni muhimu wakapata maeneo ambayo wanaweza kuishi kama wananchi wengine; wakaweza kumiliki bodaboda, kumiliki usafiri, kumiliki ardhi. Sasa wanapokuwa wanaishi ndani ya eneo la Ngorongoro huko kuna restrictions, lakini Serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ikasema hawa watu lazima wapate maeneo bora, maeneo mazuri ya kuishi. Huo ndio mkakati tuliokuwa nao kama Serikali na zoezi linaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru sana maoni ya Wajumbe wa Kamati pamoja na Wabunge katika michango yao mbalimbali, kwamba, tuangalie Sheria ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi. Hii ni kweli kabisa, wakati umefika sasa sheria hii tuifanyie marekebisho, Wizara yangu inatambua hilo na sheria hii lazima ifanyiwe marekebisho. Tumeshazungumza pia na Attorney General, tuone namna gani ikiwezekana ije tushirikishe wadau. Hii ni sheria ya muda mrefu, kwa hiyo, ni muhimu sana sheria hii ikafanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni kwamba, tupo kwenye kuona namna gani ya kuendelea kudhibiti changamoto iliyopo kati ya wanyama wakali pamoja na binadamu. Hili ni eneo ambalo tunaendelea nalo, tmeshajenga vituo vya askari 16 na tunaendelea na sasahivi tumesema tuanze kuweka mabwawa ndani ya maeneo ya hifadhi. Kutokana na hela za UVIKO tumepata mitambo, tuchimbe mabwawa kule ndani ili wanyama hawa wanaotoka kwa ajili ya kutafuta maji waweze kukaa kule ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeanza kuchimba, Ruaha National Park tuna mitambo tunachimba maji yapatikane. Tunaendelea na uchimbaji wa mabwawa katika maeneo mbalimbali, lakini sasa hivi pia kuna zoezi la kuvalisha kola, baadhi ya makundi ya tembo tunavalisha GPS collar; ukivalisha collar unaweza ukaona kwamba, hili kundi sasa linatoka kwenye hifadhi, tufanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Lindi, Mtwara, tumeanza kuvalisha collar. Kulikuwa kuna tembo, kulikuwa na changamoto na tumetuma hadi helicopter kuhakikisha kwamba, wanasogeza wale tembo, warudi katika maeneo yao ya hifadhi. Kwa hiyo, haya ni maeneo ambayo tunaendelea nayo kuhakikisha kwamba, Vituo vya Askari vinaendelea kuwepo ili wananchi wetu waendelee kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningeomba pia, kuendelea kukumbushana ni habari ya mifugo kutoingia katika hifadhi. Ndugu zangu tumekuwa na changamoto kubwa sana, tumeenda kule Usangu tumebadilisha GN 28, Kamati ya Mawaziri Nane imezunguka nchi nzima kuona nini tunafanya katika vijiji 975. Maeneo mengi tumesema tuwaachie wananchi, ili maeneo ya hifadhi yawe salama, ikiwa ni pamoja na eneo lile la Usangu tumebadilisha GN kuwaachia wananchi ili sasa maeneo ya hifadhi yabaki salama, wananchi wanahitaji maeneo ya kilimo. Tumeachia hadi ranch ya Usangu, imetoka kwenye Hifadhi ya Ruaha National Park, ili watu wapate maeneo ya kufugia, wapate maeneo ya kilimo ili hifadhi zetu ziwe salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Watanzania wenzangu kwamba, tujitahidi sana kutoingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi. Askari wetu wanakuwa na changamoto sana kusogeza hiyo mifugo na wanajitahidi sana kuhakikisha kwamba, wanalinda raia, Jeshi la Uhifadhi liko pale, wanalinda maliasili hizi na tuna maeneo mengi, tusipoyalinda sote tutapata changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya ya hifadhi, maeneo haya ya national park, misitu, ndani yake kuna vyanzo vya maji. Sasa hivi lazima tujaze Mwalimu Nyerere pale Hydro Electric Power, namna yoyote ya kuruhusu mifugo, kilimo, shughuli za binadamu, tunaweza kuwa jangwa. Kwa hiyo, nitoe rai tushirikiane Waheshimiwa Wabunge tutoe elimu, tuwakumbushe Waheshimiwa Madiwani tushirikiane kusema kwamba, maeneo ya hifadhi ni kwa maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Tanzania tuna chakula cha kutosha hadi watu wa nchi jirani wanakuja kununua, hii yote ni kutokana na mvua ya kutosha na mvua hii inategemeana na misitu tunavyoilinda. Kule juu ukienda ramani ya Afrika tayari wameshakuwa jangwa, nchi za pale juu nisingependa kuzitaja. Sasa ni namna gani tunashirikiana kulinda hizi hifadhi, maliasili hizi, maana tunasema tumerithishwa, tuwarithishe, namna yoyote ya kuachia sote tutapata kazi. Kwa hiyo, nitoe rai ndugu zangu tuangalie namna gani tunadhibiti mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemshukuru sana Waziri wa Mifugo amesema ikiwezekana sasa mifugo badala ya kuitembeza, kuchunga, tufuge. Unakuwa na eneo lako zuri, unaweka josho, unaweka sehemu ya kunyweshea maji, lakini mifugo inapozunguka nchi nzima hii ni changamoto. Tuone namna gani tunajipanga kwa mifugo yetu tuweze kuweka eneo moja, kuna watu wana viwanda vya maziwa, watu hawa wanafuga eneo moja badala ya kuzunguka nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia nafasi hii kuwashukuru sana Jeshi la Uhifadhi na maoni ya Waheshimiwa Wabunge kwamba, maslahi na mafao ya askari wetu wa Jeshi la Uhifadhi yaangaliwe. Waheshimiwa wamechangia akiwemo na Mheshimiwa Soud. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kumekuwa na changamoto, askari wetu wamekuwa wakivamiwa. Kuna askari amevamiwa na mshale wenye sumu hivi karibuni, tukio hilo limetokea Serengeti. Jana kuna askari wawili Uvinza na wenyewe wamevamiwa, askari hawa wanajitoa kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi yetu kwa faida yetu sote, maeneo haya wanaingia majangili, wengine wanatoka nchi za Jirani, ni hatari sana. Sasa askari wanapojitoa kulinda maeneo yetu ya rasilimali wanavamiwa, wanapigwa mishale, hili ni jambo ambalo naomba nitumie nafasi hii kwa kweli, kulikemea na kulaani kwa nguvu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbuka askari hawa wamebeba silaha, wanakuwa ni wavumilivu, wanapigwa mishale na wale askari walinyamaza kimya kumsaidia mwenzao mpaka kumfikisha hospitali na tumempoteza kijana wa miaka 42, Deus Mwajegele. Kwa hiyo, niombe sana, tuwape ushirikiano, tuwalinde askari wetu, tusichukue sheria mkononi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)