Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuweza kunipa nafasi ya kuchangia juu ya taarifa hizi ambazo zimewasilishwa hapa hususani katika huduma za jamii, pamoja na maendeleo ya jamii.

Mheshimiwa Spika, mimi niseme tu nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Wizara ya Afya, lakini pamoja na Wizara ya Elimu kwa namna ambavyo wameweza kujenga miundombinu mingi sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu karibu katika kila jimbo kuna majengo ya zahanati, vituo vya afya pamoja na madarasa mengi ambayo mpaka sasa hizi mengine yanakuwa yanakosa watoto. Kwa hiyo kwa hili nampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Rais ameendelea kupambana na haya masuala ya vitendo vya ukatili kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii. Tunaona ni kwa namna gani ambavyo Mheshimiwa Waziri wetu Gwajima amekuwa akiendelea kupambana kupitia hii SMAUJATA na nini kuhakikisha zile kesi za watoto na akina mama wanaofanyiwa kule kama wale watu wa maeneo husika wanashindwa kuzingatia utaratibu wa kuzifikisha kesi mahakamni, yeye mwenyewe amekuwa akiingilia kati. Kwa hiyo, mimi niseme tu nawapongeza kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mjadala wangu leo mimi ninapenda nijielekeze kwenye hali ya ufaulu nchini. Tunafahamu kabisa mwaka huu hali ya ufaulu nchini imekuwa ya kusikitisha sana na kimsingi ni hali ambayo kama Taifa tunatakiwa tujitafakari na tuone ni nini kinatakiwa kufanyika kuona Watoto wetu wa Kitanzania wanapata elimu iliyo bora, elimu ambayo itakuwa na tija na kubadilisha maisha ya Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kauli ambayo ipo inasema collapse of education is a collapse of the nation (anguko la elimu ni anguko la Taifa). Natamani tulichukue hili katika hali ya uhalisia kabisa kwamba elimu hii isipopewa kipaumbele katika nchi yetu tutaendelea kuwa na taifa ambalo lina watu wasiokuwa na weledi wa kutosha kukabiliana na changamoto za maisha ambazo zinakuwa zinatukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuaona masomo ya sayansi watoto wetu wame-fail sana na masomo ya sayansi ndiyo masomo mengi yanayoweza kumwezesha mtoto kuweza kujiajiri katika sekta mbalimbali. Mtu aliyesoma maabara ni rahisi kwenda kufungua kituo chake cha maabara na kufanya ile tasnia yake pale kwa kuwasaidia Watanzania na tasnia zinginezo.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni nini? Ninatamani kuona Serikali yetu hii ya Chama cha Mapinduzi inachukua hatua kubwa sana kuhakikisha kuwa lililotokea mwaka huu, mwakani halitokei.

Mheshimiwa Spika, ninaumia sana kwa sababu nina uzoefu wa namna ambavyo watoto mbalimbali au wazazi mbalimbali wamekuwa wakifanya jitihada ya kuhakikisha watoto wao waweze kufanya vizuri kwenye masomo. Kuna watoto ambao wanasoma katika private schools (shule za binafsi), watoto hawa mimi niseme tu kwa nafsi yangu naamini ndio waliotubeba kwenye matokeo haya ya mwaka huu. Wengi ndio walikuwa na nafasi ya kuweza kufundishwa na walimu kwa kutosha, lakini pia kwa kuwa na walimu wenye uangalizi na msisitizo wa ukaribu wa kuhakikisha wafanye vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninawapongeza sekta binafsi hii ya elimu kwa namna ambavyo wametubeba angalau kwa hizi asilimia ambazo tunakuwa tunaona kwamba tuna watoto waliofaulu kama Taifa wanatusaidia.

Mheshimiwa Spika, mimi nina-grade kwa namna nyingine kwamba wapo watoto ambao walikuwa wanasoma kwenye shule za Serikali ambao wazazi wao walijitoa kwa kuwatafutia walimu binafsi na tuition, ndio ambao wameweza kutubeba na kutufikisha Taifa kama hapo. Kwa hiyo pia niwapongeze wazazi ambao wamekuwa na wito wa kusimamia elimu ya watoto wao bila kuwaachia walimu peke yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakuja kulitazama kundi la tatu la wale Watanzania ambao hawana wazazi wenye kipato kikubwa cha kwenda private, lakini hawana wazazi wa kuwatafutia walimu wa kuwafundisha tuition. Hawa ndio watoto wa Watanzania wengi, ndio wame-fail sana na kiukweli kwa kuliona hili ndipo ninaona gap la aliyenacho na asiyenacho linazidi kuongezeka katika Taifa letu. Kama Taifa nadhani kumekuwa na harakati nyingi za kupambana kupunguza gap la walionacho na wasiokuwa nacho. Lakini kwa kuendelea na mfumo huu wa elimu ambao watu ambao wanakuwa na fedha wanaweza kuwapeleka watoto kwenye shule nzuri na wakapata elimu nzuri na wengine wakabaki wakapata elimu yetu hii bure halafu wakakosa usimamizi mzuri, naiona hatari ya kuwa na Taifa ambalo watu wengi ni dhaifu na hawana ufikiri mzuri.

Mheshimiwa Spika, niseme tu ninaiomba Wizara hii watafute namna bora ya kuhakikisha watoto wetu wale wa Kitanzania, wale halisi wa mkulima, mfugaji, wavuvi wale watu wa chini kabisa wajasiriamali wadogo wadogo wanasaidiwa kupata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaongea nikiwa na uchungu mkubwa sana, moyo wangu unaumia kwa sababu mimi ni kati ya wale watoto ambao tumesoma hizo shule lakini kwakweli bila ya yale mapambano binafsi ya mtoto kuhakikisha unajituma na nini, mazingira yalikuwa supportive, yanakusaidia kuweza kujituma ukawa na access ya hivyo vitabu, unakuta katika ripoti ya CAG unaona kabisa kuna vitabu havijapelekwa kwenye maeneo ya shule yetu, lakini unaona morale ya wazazi kuwahamasisha watoto kwenda shule imeshuka.

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi tunaziona kwenye mabango yanayoendelea kutolewa na Mikoa mbalimbali kwamba wanafunzi idadi fulani hawajaripoti shuleni, wanafunzi kiasi fulani hawajaripoti shuleni, kwa hivyo, morali ya wazazi kusomesha watoto imeshuka, hii ni kutokana na kwamba watoto wengi ambao wamesoma wanaonekana ni mizigo wanaporudi nyumbani kwa sababu kwanza wanakuwa tayari wameshakuwa ni wavivu, hawataki kujituma na kazi zile za kawaida za kijamii zinazowazunguka hawataki kushiriki. Waliosoma wengi hata walioishia Form Four tu hawataki kushika majembe, hawataki kushiriki kwenye vikundi, wanajiona kama they are extra-ordinary, wanakuwa wako tofauti na wenzao wale ambao waliwaacha kabla hawajaenda kwenye hizo elimu zao, kwa hiyo wazazi pia morali imeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona pia hata Walimu wetu, mimi naona morali ya Watumishi hususani Walimu pia imeshuka. Mwalimu badala ya kupambana kumsaidia mwanafunzi anapambana kupata extra money ya kujikimu yeye na familia yake, kwa sababu mwalimu mwenyewe angependa kuona mtoto wake anasoma katika shule hizo za private nzuri, kipato chenyewe ndiyo kama hiki ambacho tunakiona, wote tunafahamu kwamba kima cha chini cha mishahara bado siyo toshelevu kulingana na mfumko wa bei wa bidhaa mbalimbali na maisha kwa ujumla yanakuwa yamepanda gharama.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amekuwa akiendelea kuunda Tume mbalimbali, tumeona ameunda Tume ya Mambo ya Haki Jinai, lengo ni kuboresha haki ya Watanzania waweze kupata haki lakini hata elimu ni haki! Kwa hiyo, ninatamani kuona Mheshimiwa Rais atuangalizie au atuundie Tume nyingine ya kuchunguza huu Mfumo wa Elimu utaendelea kumkandamiza au kumuumiza mtoto wa kipato cha chini mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, katika suala la ufaulu nisiseme mengi niishie hapo, ufanyike utafiti wa kina wa kuhakikisha watoto wa chini wanasaidiwaje ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

Mheshimiwa Spika, pia niendelee kuomba ukarabati wa shule…

SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha kengere ya pili imeshagonga.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru naamini majengo yote ya shule za zamani yatafanyiwa ukarabati. Ahsante sana. (Makofi)