Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuhitimisha hoja hii.

Mheshimiwa Spika, pili, nitoe shukurani za dhati kwa Wabunge wote ambao wamechangia katika taarifa yetu hii ya Kamati, tumepata michango ya zaidi ya Wabunge 13 na Mawaziri Watatu ambao kiukweli katika michango yote wameelezea na wameunga mkono mapendekezo yaliyotolewa na Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika michango iliyotolewa na Wabunge hawa, ambao walimekuwa makini katika michango yao, hoja nyingi zinaenda kumgusa mwananchi wa kawaida ambaye yeye ndiye mwananchi namba moja katika nchi hii. Hoja nyingi zimezungumzwa hapa lakini zipo hoja mahsusi tatu ambazo zimezungumzwa na Wabunge walio wengi.

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ilitokana na TARURA kuhusiana na fedha za dharura na ujenzi wa barabara. Tunapozungumza fedha za dharura maana yake tunajiandaa endapo tatizo litatokea tuweze kutatua tatizo hilo. Tumefuatilia fedha hizi zinazoombwa za dharura zinaenda kutengeneza barabara ambazo zimekuwa zikitengewa fedha kila mwaka na TARURA.

Mheshimiwa Spika, sasa tunatakiwa tujiulize hapa, TARURA kila mwaka tunatenga fedha lakini barabara hizo zikijengwa baada ya muda fulani zinaharibika. Yawezekana katika ujenzi wa barabara hizo vipo vitu vya kitaalam vinakuwa havikidhi vigezo. Moja ya jambo ambalo limeonekana sana, huwezi kujenga barabara usipoweka mifereji. Kwa sababu barabara nyingi zinajengwa bila ya mifereji matokeo yake inapofika wakati wa mvua barabara zile zinaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa napitisha dodoso kwa baadhi ya Wabunge kuwaambia wanitajie barabara moja ambayo ndani ya miaka mitano imetengewa fedha kiasi gani za spot improvement, periodic maintenance na matengenezo mengine. Nilivyojumlisha katika zile barabara nimeona kama fedha zile zote zingejumlishwa kwa pamoja basi barabara ile kwa mwaka mmoja ingejengwa kwa kiwango kikubwa na hatimae tungeondokana na hii kadhia ya kuomba fedha za dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara limechukua mjadala mpana sana katika Bunge letu leo kwa maana kila Mbunge aliyezungumza na wengine waliochangia kwa maandishi wamekuwa na kero kubwa ya barabara. Kutokana na hayo, nimepokea nyongeza ya maazimio katika suala hili la TARURA, kwa sababu ulitoa maelekezo toka jana, naomba kwa idhini yako sasa nilisome. Azimio hilo linasema kama ifuatavyo: -

Kwa kuwa, Serikali imetoa mwongozo kwa Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 za fedha za mapato ya ndani katika ujenzi wa miundombinu ya barabara;

Na kwa kuwa, Halmashauri nyingi hazitekelezi mwongozo huo,

Hivyo basi, Bunge linaitaka Serikali kuandaa sheria ya utengaji wa asilimia 10 ya mapato ya ndani katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Spika, tunakumbuka huko nyuma Serikali ilitoa mwongozo wa utengaji wa asilimia 10 lakini kwa sababu ulikuwa siyo wa kisheria basi watu walikuwa wanafanya kadiri watakavyo na baada ya kuufanya wa kisheria, Halmashauri nyingi zimekuwa zikitekeleza. Kwa hiyo naomba na hili nalo liwe katika sehemu ya azimio.

Mheshimiwa Spika, nasema hili sababu ukichukua baadhi ya Halmashauri hasa za Dar es Salaam, kwa mfano Halmashauri ya Ilala kwa mwaka inatenga Shilingi Bilioni 6.2 kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwa ajili ya zile asilimia 10. Sasa fedha hizi zikitumika vizuri kila mwaka tunazungumzia kilometa takribani 10 za lami nyepesi. Kwa maana hiyo, ndani ya miaka mitano tutakuwa tumetengeneza takriban kilometa 50 za lami nyepesi.

Mheshimiwa Spika, suala jingine ambalo limechukua nafasi kubwa katika mjadala wetu ni mgogoro wa ardhi katika Jiji la Dodoma. Ni wakati sasa Serikali ilichukulie jambo hili very serious. Wananchi wengi katika Jiji la Dodoma na Halmashauri nyingine nchini wamekuwa wakilalamikia masuala haya ardhi. Ukienda pale Kawe, kule Nyakasangwe, sijui wapi, kuna migogoro mikubwa ya ardhi. Kwa hiyo, Serikali sasa tutayarishe mpango maalum wa kwenda kutatua hii migogoro ya ardhi. Migogoro hii mara nyingi inawahusu wananchi wanyonge. Kwa hiyo tunapowaonea wananchi wanyonge tafsiri yake wananchi walio wengi wanaenda kupata uonevu mkubwa katika maeneo yetu. Kwa hiyo ninaomba na kusisitiza sana, migogoro ya ardhi ichukuliwe hatua stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala jingine ambalo limechukua nafasi kubwa ni miradi ya TACTIC, kuna mradi mwingine wa RISE na mradi wa uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam yaani DMDP. Ninaiomba sana Serikali miradi hii Wabunge wengi wanaitegemea, tuangalie uwezekano mkubwa wa kila maeneo yenye mahitaji basi miradi hii ifanyike na hatimae sasa tuweze kuondoa tatizo kubwa la miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, suala zima la TAKUKURU rafiki. Tunazungumzia habari za fedha nyingi za maendeleo katika maeneo yetu lakini Wabunge tusipopata uelewa mzuri wa TAKUKURU rafiki, fedha hizi zinaenda kupotea. TAKUKURU rafiki inamuhusisha moja kwa moja mwananchi wa kawaida wa pale kijijini kwenda kujua fedha zilizoletwa na namna gani atakayezisimamia zile fedha ili ziweze kutekeleza ule mradi kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni rai yangu, Serikali sasa ione namna bora ya Wabunge hawa kuwapa uelewa mkubwa wa dhana nzima ya TAKUKURU rafiki ili na wao waende kutoa maelezo hayo kwa wananchi hawa. Ukisoma ile sheria ya 288 ya uanzishwaji wa Serikali za Mitaa utaona kazi ya Mtendaji wa Kata ni kumsaidia Mkurugenzi katika utekelezaji wa majukumu yake. TAKUKURU rafiki wakielekezwa hawa Watendaji wa Kata na Mitaa wataenda kuisaidia halmashauri, wataenda kuisaidia mapato ya Serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo sasa naomba kutoa hoja kwamba mapendekezo yote ya Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa yakubaliwe na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. SEBASTIAN H. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, naafiki.