Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Musoma Mjini, Jimbo langu lilibahatika kupata na lenyewe ule mpango wa umeme wa REA hasa katika yale maeneo au mitaa ya pembezoni pamoja na kwamba liko mjini. Baadhi ya mitaa iliyofaidika na mpango huo iliyoanza kufaidika ni pamoja na ule Mtaa wa Bwiribukoba, Nyabisare, Songambele, Kwangwa, Zanzibar, Bukanga ni mitaa ambayo ilibahatika na ilianza kubahatika na huo mpango. Baada ya 2015 - 2020, tulipoanza 2021 mpaka leo ule mpango kwa pale Musoma Mjini ukaondoka na baada ya kuondoka tunaishukuru kwamba TANESCO imeendelea kusambaza hata zile transformer katika hiyo mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu yale maeneo mitaa ya pembezoni ni maeneo ambayo yanafanana na maeneo ya vijijini. Kwa hiyo unakuta transformer imepelekwa lakini watu walioweza ku-tap pale umeme hawavuki watu watatu, wanne na sababu ni rahisi tu kwamba sasa kwa sababu ile miji inakaa mbali mbali lazima mwananchi aweke nguzo zaidi ya mbili. Sasa nguzo mbili unazungumzia zaidi ya shilingi 500,000. Sasa hebu tuliangalie hili kwamba yule aliyebahatisha 2015 - 2020 aliweka umeme kwa shilingi 27,000. Leo huyu mwingine jirani yake ambaye wakati ule aliomba lakini hakupta nafasi anaambiwa aweke umeme kwa zaidi ya shilingi 500,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kutokana na hali hiyo, kwa hiyo watu wangu wengi wote walioko maeneo ya pembezoni wameshindwa kuweka umeme na kama tunavyofahamu mahitaji ya umeme ni makubwa na hasa katika mazingira ya sasa, wananchi wangependa wapate huo umeme. Sasa leo cha ajabu sasa ukija pale Musoma Mjini na nimwombe Mheshimiwa Waziri Makamba aje pale Musoma mwenyewe ashuhudie kwamba leo jirani yangu ni Butiama, pale kuna Kijiji cha Nyabange, pale wanapata umeme wa shilingi 27,000, hapa kwangu Bwiribukoba wanapata umeme wa shilingi 500,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo matokeo yake leo watu badala ya kukimbilia mjini watu wengi wanahamia pale jirani kwa sababu pale ndipo sasa gharama za kuishi zimekuwa nafuu. Sasa kutokana na hali hiyo, watu wangu wameshindwa kufahamu kwamba hivi wao kumbe kuingia mjini tena imekuwa adhabu kwao? Sasa natambua kabisa na wote tunatambua kwamba bado ile miradi ya peri urban bado ipo na kama ipo, sasa sisi ambao tayari tulibahatika kuingia kwenye huo mpango wa REA, leo tuna dhambi gani, badala ya kuendelea kulipa kwa shilingi 27,000 ili watu wote waweze kupata hiyo huduma sasa matokeo yake wao wanalipa umeme kuanzia shilingi 300,000 mpaka zaidi ya shilingi 500,000?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningependa wakati Mheshimiwa Waziri anajibu, ni vyema awaambie kabisa watu wa Musoma watambue kwamba sasa ule mpango utarudi au ndiyo wameendelea kuusahau. Kama wameendelea kuusahau hata umuhimu wa zile transformer haupo kwa sababu Serikali inapoteza resource pale inapopeleka transformer halafu wanaweza ku-tap watu wanne au watu watatu peke yake. Kwa hiyo nadhani kuna haja ya kuliangalia hilo ili tuone namna ya kuwasaidia watu wetu wa Musoma kwa sababu nao wangependa kupata hiyo huduma ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, liko jambo ambalo vile vile huwa linanichanganya kidogo. Leo unakuta kwamba kuna mtu anahitaji umeme na kwa sababu anahitaji umeme akienda TANESCO, wanamwambia hawajawa tayari au hawana bajeti kwa mwaka huu kwa ajili ya kumsogezea umeme. Yule mwananchi anasema sawa, mimi nina hiari sasa kulipia in advance. Sasa akikubali kulipia in advance, TANESCO wanasema ukishalipia kwa hiyo gharama labda ya kupeleka pale umeme kununua transformer pamoja na zile nguzo labda unakuta ni Sh.20,000,000. Sasa najiuliza kama yule mwananchi amekubali kulipia huo umeme in advance, ni kwa nini TANESCO wasiendelee kumrudishia aidha kwa kumkata pole pole mpaka zile fedha zake zitakapoisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tofauti na hapo anaambiwa wewe kaa subiri siku tukiwa tayari na bajeti tutakuwekea umeme. Kwa hiyo nadhani kuna kila aina ya sababu kwa yule ambaye ameshajitolea amelipa in advance walau TANESCO wakubali kuja kumrudishia hizo gharama kuliko kusema kwamba hawako tayari tena kuja kumlipa hizo gharama wakati bado wanaendelea kumchaji ile bili yake ya kila mwezi. Kwa hiyo nadhani hapo napo kuna haja kidogo ya Serikali kuendelea kuliangalia hilo tatizo la kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye upande wa madini. Tunatambua kwamba STAMICO ni caretaker kwa ajili ya wale wachimbaji wadogo na kama kweli tunapenda kuwasaidia wale wachimbaji wadogo, hivi STAMICO Mheshimiwa Waziri, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inawasaidia STAMICO uwezo kwa kuwapa fedha za kutosha ili waweze kuwakopesha wale wachimbaji wadogo wadogo waweze kujenga uwezo? Kwa sababu leo hii ukiangalia hata katika takwimu wale wachimbaji wadogo ni kati ya watu ambao wanachangia sana pato la nchi hii, lakini wapo tu wala hakuna namna wanayosaidiwa ili waendelee kukua, waendelee kukuza mitaji na kutokana na hali hiyo wachimbaji wadogo uzuri wao ni kwamba leo ukimsaidia akijenga uwezo anarudi ku-re invest humu humu nchini tofauti na wale wachimbaji wakubwa ambapo unaambulia tu kile kifaida, fedha nyingine yote inayobaki anaipeleka kwao. Kwa hiyo kuna kila aina ya sababu ya kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo kwa sababu akishapata fedha hapo ataendelea kujenga hoteli, ataendelea kufanya miradi mikubwa ambayo itaendelea kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani kuna kila aina ya sabau ya kuona namna ya kuwasaidia. Kwanza kuisaidia STAMICO, lakini vile vile aweze kuwasaidia wale wachimbaji wadogo na kwa kufanya hivyo watasaidia sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.