Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. S. GULAMALI - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa namna ambavyo umeweza kusimamia hoja ya Kamati vizuri, nakupongeza sana.
Pili, nitumie fursa hii kuwapongeza Wabunge wanane ambao wamechangia hoja ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wabunge ambao wamechangia, Wabunge watano wamechangia sekta ya nishati na hususan hali ya upatikanaji wa umeme, utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji na utekelezaji wa mradi wa REA. Kamati inashukuru kwa kuunga mkono maoni na mapendekezo ambayo Kamati imeyatoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa machache yaliyokuwa yamebainika kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia; Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mheshimiwa Vedasto Manyinyi; na Mheshimiwa Josephine Genzabuke wamezungumzia upande hasa wa masuala mazima ya usambazaji wa umeme vijijini, REA, namna ambavyo utekelezaji wake unavyoenda na pia Mheshimiwa Waziri Januari amezungumza hapa kwa ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia utekelezaji wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kule Rufiji ambao amezungumza Mheshimiwa Nusrat Hanje, na namna ambavyo utekelezaji wa transmission line kutoka kwenye Bwawa la Mwalimu kuja Chalinze. Pia iende sambamba na ujenzi wa substation pale Chalinze.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bwawa lile unaenda sambamba pamoja na ujenzi wa transmission line. Kama ambavyo mchangiaji alivyozungumza kwamba tunaiomba pia Serikali ihakikishe kwamba usimamizi wa ujenzi wa transmission line kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere kuja Chalinze ukamilike uende kwa haraka na ukamilike kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukamilishaji wa substation iliyoko pale Chalinze na yenyewe pia kwa sababu inaonekana asilimia yake iko chini, tunaiomba pia Wizara ihakikishe kwamba suala hili inalikamilisha kwa haraka ili iende sambamba na ukamilishaji wa bwawa lenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunampongeza Mheshimiwa Rais kipindi ambacho mwezi wa 12 wakati wa ujazaji wa maji katika lile bwawa, Mheshimiwa Genzabuke amezungumza hapa. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na uendelezaji wa kutoa fedha kwenye mradi huu wa Mwalimu Julius Nyerere, kwamba haukwami na unaenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo lilizungumzwa hapa na Mheshimiwa Tabasam ni suala la mafuta hususan kuchelewa ushushaji na hivyo kuongeza bei ya mafuta. Ni suala ambalo Kamati imekuwa ikilisema sana na Mheshimiwa Tabasam amelizungumza hapa. Kwa hiyo, naomba tu Serikali iboreshe miundombinu na Bandari ya Dar es Salaam kuhakikisha kwamba suala hilo la upakuaji mafuta linaenda kwa wakati ili kupunguza gharama kwa watumiaji wa mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamechangia kuhusu kupeleka umeme kwenye migodi, na Mheshimiwa Waziri amelizungumza hapa, hivyo tumwombe Waziri alisimamie suala hili kuhakikisha kwamba migodi inapata umeme. Nimesikia Mheshimiwa Tabasam amezungumzia kule Sengerema na migodi mingine ambayo ipo ndani ya nchi yetu, hata kule Igunga, Nzega na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika upande wa madini, Wabunge wanne wamechangia; Mheshimiwa Iddi Kassim, Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mheshimiwa Nusrat Hanje, pamoja na Mheshimiwa Waziri Dotto Biteko. Hususan kwenye suala zima la Mwanza Refinery, GST, STAMICO, na leseni za uchimbaji wa Magnet. Kamati inawashukuru sana na kweli suala la Mwanza Refinery ni lazima Serikali ichukue hatua za makusudi kuhakikisha kwamba kiwanda kile kisiweze kusimama au kisiweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchangiaji wa maandishi Mheshimiwa Engineer Manyanya pia naye amezungumzia katika taarifa yake kwamba miundombinu ambayo inaweza kuirahisisha nchi yetu kufanya biashara na nchi jirani zetu kama Kongo, Serikali iboreshe miundombinu kuhakikisha kwamba sekta ya madini inakua na hasa ukizingatia nchi ya Congo ni potential katika eneo zima la rasilimali madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niliombe Bunge lako Tukufu lichukue mapendekezo ya Kamati kuwa mapendekezo ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa hoja.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.