Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii, nami mchango wangu utajielekeza katika taarifa ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kutambua rasilimali watu tuliyonayo katika Diaspora, tumeona hivi karibuni ameendelea kutoa nafasi mbalimbali za uteuzi kwa Watanzania wenzetu ambao walikuwa wanafanya kazi nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo nipongeze Kamati kwa kutambua umuhimu wa Diaspora pia kwa kutambua kwamba bado hatuna mfumo sahihi wa kutambua wenzetu wa Diaspora lakini kuweza kuwafungamanisha katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea mwaka 2021 mwezi Juni nilichangia katika mchango wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje hapa Bungeni ilikuwa ni Tarehe 01 Juni, 202, ambapo niliishauri Serikali, kwakuwa suala la uraia pacha lina changamoto mbalimbali na linagusa Katiba, tujielekeza katika suala la Hadhi Maalum ambalo litawezesha diaspora kupata kila kitu na kunufaika na kujishughulisha na shughuli zote za kiuchumi, kasoro maeneo mawili. kujishughulisha na masuala ya kisiasa pamoja na ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama. Nashukuru wakati ule tulipata jibu hapa hapa Bungeni kwamba Serikali inafanyia mapitio Sera ya Mambo ya Nje, ndani ya Sera ile itaweka suala la diaspora na sera ile itakuwa tayari Disemba 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ni takribani miaka miwili toka Bunge la Bajeti 2021, mpaka leo hii bado Serikali haijaja hapa Bungeni kutueleza bayana ni lini itakamilisha mpango wa hadhi maalumu kwa ajili ya diaspora. Ninasema hivi kwa sababu mchango wa diaspora katika ukuaji wa uchumi kwa Taifa letu ni mkubwa sana. Kwa mwaka 2022 Kenya peke yake imepata dola bilioni nne kupitia Diaspora na imefikia mpaka Diaspora ndiyo wana mchango mkubwa zaidi kwa foreign currency katika nchi ya Kenya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunahitaji rasilimali watu, tunahitaji rasilimali fedha, tunajaribu kukuza uchumi, tunao diaspora ambao wana taaluma kubwa, tunao diaspora ambao wana mitaji lakini kwa kuwa bado tunashindwa kutambua hadhi maalum na kukamilisha mchakato wake tunashindwa kunufaika na diaspora lakini na diaspora wanashindwa kunufaika na nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa muda mrefu katika safari zake za nje ya nchi na kila nchi anayokwenda anakutana na diaspora, ni mara kadhaa Mheshimiwa Rais amekuwa akiahidi diaspora kwamba suala la hadhi maalumu linafanyiwa kazi, sasa nashangaa sana kwa nini Wizara hii inakwamisha maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea Bungeni na kutueleza bayana suala la hadhi maalumu kwa ajili ya diaspora litakamilika lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha naomba sana nipate kauli ya Serikali ni lini itakamilisha mchakato wa wenzetu diaspora kupata hadhi maalum ili waweze kujishughulisha na shughuli za kiuchumi nasi kama Taifa tuweze kupata: -

(i) Takwimu sahihi za diaspora,
(ii) Takwimu sahihi za mchango wanadiaspora kwenye ukuaji wa uchumi wetu,
(iii) Kuwatumia katika rasilimali watu pale ambapo tunahitaki taaluma zao,
(iv) Kuwatumia katika rasilimali fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Wizara hii iunge mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kufungua uchumi wetu kidiplomasia na isiwe sehemu ya mkwamo wa kufanikisha suala la hadhi maalumu kwa diaspora. Ahsante. (Makofi)