Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii nami niweze kuchangia kuhusu taarifa za Kamati ambazo ziko mbele yetu. Awali ya yote napenda kuishukuru Serikali kupitia Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Kilimo. Kama taarifa yetu ya PIC ilivyojieleza, tulipata nafasi ya kuwaita kwa ajili ya kufuatilia maazimio ambayo tuliyaweka hapa ya Serikali kulipa deni kwenye Sekta Ndogo ya Bodi ya Pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, waliweka wazi kwamba wanakamilisha uhakiki na wakasema mpaka kufikia mwezi wa tatu uhakiki utakuwa umekamilika na wataingiza kwenye mwaka wa bajeti unaokuja kwa ajili ya kulipa. Nawapongeza, lakini niseme tu Serikali ijipange ihakikishe kweli kwenye bajeti ijayo inaingiza deni hili la sekta ndogo ya pamba. Kwa nini? Kwa sababu sekta ndogo ya pamba imedorora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu ilipotokea ile patashika ya mwaka 2019, baada ya Soko la Pamba Duniani kucheza, na hatimaye watu wakaingiza mitaji yao kwa promise ya Serikali kwamba itaweza kutoa ruzuku, ukweli ni kwamba Serikali iliposhindwa kutoa ruzuku upatikanaji wa pembejeo umekuwa ni shida. Kwa sababu kuna deni la zaidi ya Shilingi bilioni 80 la pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata wanunuzi wenyewe wamesinyaa kuendelea na shughuli hiyo, kwa sababu yako madeni makubwa ambayo ni zaidi ya Shilingi bilioni 100 Serikali inapaswa kulipa ili kuhakikisha kwamba sekta ndogo ya pamba inaendelea kustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye taasisi yetu, Shirika la TANAPA. Jambo la kwanza, Hifadhi ya TANAPA labda kwa uelewa tu, awali ilikuwa na hifadhi 16 ambazo zina kilomita za mraba zaidi ya 57,000. Zikaongezeka mwaka 2019 kama sikosei, zikaongezeka hifadhi sita ambazo zina kilomita za mraba 47,000. Ikafanya jumla ya hifadhi zote zikawa 22 ambazo zina kilomita za mraba zaidi ya 100,004.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni ongezeko zaidi ya asilimia 45. Cha kushangaza sasa, badala ya Serikali kuwa inaongeza fedha za maendeleo na matumizi ya kawaida, imekuwa inazipunguza kila mwaka. Cha ajabu hicho! Ukiangalia kwa mfano, kuanzia mwaka 2019 zilipoongezeka hifadhi sita mwaka 2019 Serikali ilitenga shilingi bilioni 70 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwenye Shirika la TANAPA. Mwaka uliofuata wakapunguza shilingi milioni 500, yaani ikawa ni shilingi bilioni 69.5. Mwaka uliofuata wakapunguza zaidi wakatenga shilingi 64,500,000,000/=. Mwaka huu tulionao wamepunguza zaidi, wametenga shilingi bilioni 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unafikiria, ni kitu gani hiki? Yaani umeongeza ukubwa wa kazi kwa TANAPA kutoka hifadhi 16 mpaka 22 ongezeko la zaidi ya asilimia 45, badala uwaongezee fedha, wewe unapunguza. Mimi sijui tunafanya kitu kitu hapa! Ni kituko ambacho hakivumiliki. Wamekuja kwenye Kamati wanalialia pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Serikali ichukue hatua. TANAPA tuna kila sababu ya kuiongezea fedha. Kwanza, ni taasisi za kimkakati. Hawa wanasimamia zaidi ya asilimia 11 ya eneo la nchi yetu. Bwawa la Mwalimu Nyerere liko chini yao pia. Kuna Askari zaidi ya 120 ambao wanalinda pale Bwawa la Mwalimu Nyerere. Wanaimarisha ulinzi na usalama. Hawa hawana nyumba za kulala, hawana usafiri wa uhakika. Bwawa ambalo lina matrilioni ya Shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, TANAPA tunajua imeajiri Watanzania wengi sana; tunajua TANAPA ni chanzo cha mapato kwa Serikali; tunajua TANAPA kupitia hifadhi zake na shughuli zake ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni; pia TANAPA inalinda urithi wetu na utambulisho wetu kupitia mbuga zetu mbalimbali na vivutio vya kiutalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba tuna kila sababu ya kuongezea fedha shirika hili. Kama tunaihitaji TANAPA kwa maana ya hifadhi zake ziendelee kuwepo, urithi wetu uendelee kuwepo, utambulisjho wetu uendelee kuwepo, tuendelee kupata mapato, ajira za Tanzania, tuendelee kusimamia kikamilifu hii asilimia 11 ya nchi yetu, lazima tuwaongezee fedha TANAPA ili waendelee kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TANAPA mahitaji yao; tuliwahoji siku ile walivyokuja kwenye Kamati. Wao wanaomba fedha za maendeleo shilingi bilioni 120 kwa ajili ya vifaa vya maendeleo. Wanaamini wakipata fedha hizi watafanya miradi mikubwa ambayo itaboresha sana mazingira ya hifadhini na hatimaye kuongeza watalii kwa kiasi kikubwa sana. Hata hivyo, wanahitaji zaidi ya shilingi bilioni 220 kwa sababu tumewaongezea eneo la kufanya kazi zaidi ya asilimia 45. Wanahitaji shilingi bilioni 222 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashindwa kuelewa, yaani Serikali kupitia Mheshimiwa Rais, amefanya kazi nzuri sana ya ku-promote utalii wa nchi hii kupitia Royal Tour na watalii wameongezeka kweli kweli, wanatiririka kweli kweli! Tume- overcome hata ile challenge ya Covid, imeisha na watalii wanazidi kuja kutokana na initiative ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya kupitia Royal Tour. Sasa Watendaji wa Serikali wanashindwa vipi kuhakikisha kwamba wanaweka mazingira mazuri ili hao watalii wakija wakutane na mazingira ya kisasa zaidi ambayo ni rafiki, wazidi kuja Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Wabunge wote, naomba sana tuweze kuungana kuibana Serikali kwa kuishauri iongeze fedha kwa ajili ya TANAPA ili TANAPA wawe na uwezo wa kusimamia na kuendesha hifadhi zake vizuri kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru sana TANROADS kwa kazi nzuri sana ambayo wanayoifanya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri, muda wako umekwisha.

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.