Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kuunga mkono hoja za Wenyeviti wa Kamati zote tatu ambao wamewasilisha hapa Bungeni siku ya leo. Hata hivyo, naomba nichangie kwenye baadhi ya maeneo nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali PAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba jukumu tulilonalo kama Bunge ni usimamizi wa Shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na kushauri pale ambapo panawezekana. Kwa hiyo, naomba niwe na maeneo ya kushauri kutokana na observations ambazo nitazifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujikita zaidi kwenye taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali kutokana na ufinyu wa muda ili angalau niwe na mchango fulani wa kutoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwenye nchi yetu na bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumza hapa, kwamba tuna kiu kubwa ya maendeleo kwenye nchi yetu. Pia, tuna changamoto kubwa sana ya ajira kwa vijana. Vijana tunao wengi na tuliahidi kwenye ilani CCM kwamba tutatengeneza ajira zisizopungua milioni nane kufikia mwaka 2025. Hata hivyo, tumejiainisha kupitia Ilani ya CCM kwamba tutaenda kutoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya yote ambayo tumeyafikiria na tumeyapanga yatawezekana tu kama maeneo mawili makubwa ndani ya Serikali tutaweza kuyafanyia kazi. Kwanza ni kutengeneza mapato ya kutosha. Kuhakikisha kwamba tunakuwa na mapato ya kutosha kwa Serikali yetu kuweza kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ni la msingi pia ni kudhibiti matumizi yasiyo sahihi na kuchukua hatua kali kwa wote ambao wametumia vibaya fedha za Serikali. Sasa nataka niguse maeneo machache tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kuhusiana na miradi ya maji ambayo imekaguliwa. Mwenyekiti wa Kamati amezungumza hapo kwamba kuna matatizo makubwa ambayo tumeyaona ndani ya miradi ya maji. Hii ipo kwenye eneo pana la utambuzi wa mradi, designing ya mradi na utekelezaji wake. Inaonekana kama hatuna National Water Supply Master Plan. Ni kama tunabahatisha tu kulingana na vyanzo vidogo vidogo ambavyo tunavipata kwenye maeneo ili tu-address tatizo kwenye maeneo kule. Matokeo yake tunajikuta tunatumia fedha nyingi za Serikali kufanya miradi midogo midogo ambayo siyo endelevu, na hata mingine inapelekea kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napendekeza kwamba tuwe na Master Plan ya Kitaifa, tuainishe vyanzo vikubwa, vichache, na tupeleke fedha kwa ajili ya kwenda kuibua miradi ile mikubwa na kusambaza maji kwenye maeneo yote kupitia miradi mikubwa kuliko miradi hii midogo midogo ambayo tunatumia pesa nyingi ambayo siyo endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tuna Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini pale chini tuna Kijiji cha Mlalo, Lower Rufiji, maji yanapoelekea Baharini kutoka kwenye Bwawa, ni maji ambayo tayari yameshatumika kwenye Bwawa. Designing ambayo inafikiriwa kufanyika sasa hivi ni kutoa maji pale, kupeleka Kibiti, Ikwiriri, Mkuranga Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tulifikiri kwamba ilitakiwa ifanyike comprehensive designing ili kuwe na Northern Circuit au Northern Zone na Southern Zone ili maji yale ya Bwawa la Mwalimu Nyerere pia yaweze kuelekezwa kwenye Mikoa ya Lindi na Mtwara, ili kuhakikisha kwamba tunatatua kabisa tatizo la ukosefu wa maji Lindi na Mtwara, kwa sababu tu tunacho chanzo cha uhakika wa maji kwa upande wa Rufiji. Kwa hiyo, tukifanya hivyo itatusaidia sana kupunguza gharama na pia kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile miradi mingi imetekelezwa ikiwa na variations nyingi. Tunalazimika kulipa fedha nyingi kutokana na usimamizi mbovu na uwajibikaji mdogo wa watumishi wa umma kusimamia hii miradi. Hii tumekuwa tukiizungumza sana na kwa kweli labda tujaribu kufikiria kama Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maswali yetu ambayo tulikuwa tunawahoji hata Maafisa Masuhuli, tulikuwa tunawauliza, hii business as usual, comfort zone ambayo watumishi wa umma wanayo na kinachoitwa security kwa watumishi wa umma kwamba huwezi kufukuzwa kazi kirahisi ndani ya Serikali, tuendelee nayo au twende kwenye ajira za mikataba ambayo ni performance based? Kwamba ukisababisha hasara kwa Serikali, unaondoka. Kuliko ilivyo sasa wako kwenye comfort zone, kumfukuza mtumishi ni kazi ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tuliangalia eneo la uingizaji wa mapato. Kwenye kuingiza mapato, tuliangalia eneo la utalii, bahati nzuri Mheshimiwa Vuma amezungumza hapa, ingawa tutatofautiana naye kidogo kwa jinsi ambavyo tulikuwa tumeona sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kufanya mahojiano na watu wa utalii wakiongozwa na Afisa Masuhuli wa Wizara ile, tulibaini kwamba hawana mkakati wa wazi wa kukuza utalii kwenye eneo letu. Pia kuna ushirikishwaji mdogo au uratibu mdogo ndani ya Serikali na sekta ya utalii na sekta nyinginezo ambazo shughuli zao kwa namna moja au nyingine zinaathiri shughuli za utalii. Kwa hiyo, tulikuja kuona kwamba hata wakiomba bajeti, unawapa kwa ajili ya kazi ipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Tanzania ni ya pili baada ya Brazili kwa kuwa vivutio vingi vya utalii; kuanzia utamaduni (culture), mpaka vivutio vyenyewe vya kwenye mbuga. Tuna kila kitu; ukienda kwenye beach tourism, kwenye kila kitu, lakini idadi kubwa ya watalii ambayo tumewahi kuipata ni watu milioni moja laki tano sijui na ishirini na mbili elfu sijui na ngapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni idadi ndogo mno ukilinganisha nchi kama ya Ufaransa ambayo imeweza kuingiza watu milioni 89.4 kwa mwaka; ukienda Hispania imeweza kuingiza watu milioni 83.7 kwa mwaka; ukienda Marekani milioni 79.3 kwa mwaka ambao hawana kabisa vivutio kama tulivyo navyo sisi, lakini wameweza kuvutia watu mamilioni kwa mamilioni. Sisi tumevutia watu milioni 1.5, tena hao milioni 1.5 kuna double counting humo ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna conference tourism. Kuna watu wanakuja tu kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanahesabika kwamba ni watalii. Wanakuja kwa ajili ya mikutano ya SADC, wanahesabika kama ni watalii. Sasa hivi JKCI tunatibu watu. Watu wanatoka Malawi wanakuja kutibiwa pale JKCI Muhimbili, nao tunawahesabu kwamba ni watalii. Ni watalii wangapi wametokana na mipango hasa ya Wizara ya Utalii na implementation yake katika eneo hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni maeneo ambayo tungeweza kuingiza fedha za umma ambazo siyo za kikodi (non-tax revenue). Ni public asset ambayo tunayo na hatuitumii. Kwa kweli tunasikitika kwamba tunavyo vyanzo kabisa vya kuweza kuingiza fedha, lakini hatuvitumii kuingiza fedha. Hii inapelekea pressure kubwa kwa Waziri wa Fedha, inabidi ahangaike kutafuta mikopo. Mikopo ya sasa hivi, concession loans zinapungua na non-concession zinaongezeka, ambapo baadaye tutakuja kutengeneza burden kubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tuna vyanzo vya uhakika vya kuongeza fedha ambazo ni non-tax revenue ambazo ni za kwetu. Mungu ametujalia hivi vyanzo vya kutuingizia kipato kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napenda kusisitiza kwamba sisi kama Bunge tuitake Serikali kuangalia upya mifumo ya usimamizi wa shughuli za Serikali ikiwemo watumishi wa umma. Watumishi wa umma hawawajibiki ipaswavyo. Tumelipa variations nyingi kwenye miradi ni kwa sababu tu kuna mtumishi mmoja au wawili hawakusaini GN mapema, basi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi ule wa Terminal Three, wakati tunaangalia Viwanja vya Ndege, tumemlipa BAM ile construction company ya Netherland faini ya Dola milioni 20 baada ya ku-negotiate. Walimtoza Dola milioni 50, ambayo ni sawa sawa na Shilingi bilioni 54 kwa sababu tu ya uzembe wa mtu mmoja au wawili walioko pale TRA na hazina kupitisha GN. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango mzuri. Ahsante sana.

MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)