Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Pia nikushukuru wewe kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kwa kusema kwamba Maafisa Maduhuli kwa maana ya Wakurugenzi wanalo jukumu kubwa sana la kuhakikisha kwamba kila senti inayopitia katika mikono yao kwa maana ya halmashauri iko katika mikono salama. Jukumu hili ni la kisheria na linawataka wao kuhakikisha kwamba wanafanya kila kinachowezekana kuhakikisha kwamba fedha ya Mtanzania au kwa maana ya fedha ya wananchi inalindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu gani? Mimi kama Mjumbe katika Kamati ya LAAC, tumekuwa tukihojiana na halmashauri mbalimbali. Katika halmashauri 34, tuliweza kuhojiana na Kamati nne ambazo zilifanyiwa ukaguzi maalum kwa maana ya special audit. Tulivyohojiana na Kamati hizi, tulikuta kwamba kuna upotevu wa fedha nyingi sana ya Serikali. Kwa mfano, katika halmashauri nne, moja wapo ikiwa ya Dar es Salaam kwa maana ya Ubungo, Kigamboni, Ilemela pamoja na Iringa. Halmashauri hizi kwa pamoja zilipoteza takriban shilingi bilioni 9.055 kama ifuatavyo: -
(a) Halmashauri ya Ubungo ilipoteza takribani shilingi bilioni 4.9;
(b) Halmashauri ya Kigamboni ilipoteza shilingi bilioni 1.1;
(c) Halmashauri ya Ilemela ilipoteza shilingi bilioni 2.9; na
(d) Halmashauri ya Iringa ilipoteza takribani shilingi milioni 124.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla ndiyo kama hiyo amount niliyoisema hapo. Fedha hizi zimekuwa zikipotea vipi kwa namna moja au nyingine, kunakuwa na njama zinazofanyika kuhakikisha hizi fedha zinapotea. Njia mojawapo ni ya kurekebisha au kubadilisha miamala pamoja na tarakimu za ankara. Njia nyingine ni ya kufuta ankara pamoja na miamala hiyo na njia nyingine pia ni ya kuweka miamala ambayo haistahili maana yake miamala ambayo siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ni nini? Kwa kufuta miamala hiyo lakini pia na kurekebisha tarakimu za miamala pamoja na ankara kunakusudia wao kupata kiasi kidogo kwenye ripoti, kwamba ionekane kuna fedha ndogo kwenye ripoti lakini wakiwa wana fedha nyingi mkononi, hivyo kuwafanya waweze kutumia fedha hii kwa makusudio ambayo hayakukusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye hilo, ni kwamba ile ya kuweka miamala isiyostahiki, lengo ni kufanya financial statement kwa maana ya ripoti iwe impaired, yaani ionekane kwamba haina sifa ya kuweza kutumika wakati ikihitajika, kama mtu anashtakiwa. Kwa hiyo hayo yote tunaona kwamba ni makusudio ovu ambayo yanatokana na watendaji ambao siyo waaminifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha hilo, kuna jambo lingine ambalo limeashiria pia upotevu mkubwa wa fedha. Zile pale zilikuwa tayari zishapotea lakini hizi ni kiashirio cha upoteaji. Kwa mfano, ukienda moja kwa moja kwenye halmashauri ambazo nimezitaja, kwa Halmashauri ya Ubungo kwa mfano. Kumekuwa na ubadilishaji wa miamala yenye thamani ya takribani shilingi milioni 156. Halikadhalika kumeripotiwa madeni hewa kwa maana ya madeni ya uongo ya takribani shilingi milioni 976. Vilev vile kumeripotiwa pia madeni yasiyokuwa na viambatanisho au madeni yasiyokuwa na justification takribani ya shilingi bilioni 1.076.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mweka Hazina wa Halmashauri ya Ubungo kwa wakati huo, jina tunamhifadhi yeye alimdanganya Auditor kwa kusema kwamba amekusanya takriban shilingi bilioni 33.4, lakini kiuhalisia baada ya kufanya reconciliation ikaonekana kwamba ameweka benki kiasi cha shilingi bilioni 31.4 pekee, hivyo ni kwamba kuna kiasi cha takribani shilingi bilioni mbili ambacho kilikuwa hakieleweki, kimepotea. Inawezekana kwamba kweli alikusanya lakini fedha hii ikawa imetumika isivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ripoti hiyo hiyo kwenye Halmashauri ya Ubungo ambapo iliripotiwa kiasi cha takribani shilingi milioni 829 ambayo mdaiwa wa halmashauri alikwenda akailipa benki moja kwa moja. Kitu cha kushangaza fedha hii ilitolewa siku hiyo hiyo kwa mfumo wa cash, kwa maana ya fedha taslimu. Sasa hapo unaweza ukaona jinsi gani mambo hayo yanavyokwenda. Kuliripotiwa pia kiasi cha mapato ambacho kilikuwa ni takribani shilingi milioni 623. Fedha hii ilikuwa ni mapato ya halmashauri lakini haikuripotiwa, yaani ilikuwa imeripotiwa pungufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala lingine la adjustment imefanyika, kwa maana ya marekebisho ya miamala. Kwenye Halmashauri ya Kigamboni kulikuwa na marekebisho ya takribani shilingi bilioni 10.8. Kwenye Halmashauri ya Ilemela kulikuwa na marekebisho yanayofanana na hayo ya takribani shilingi bilioni 8.7. Kulikuwa na fedha ambayo imeripotiwa ambayo yenyewe ilikuwa imefutwa kwenye POS kwa maana ya system za ukusanyaji takribani shilingi milioni 554. Halikadhalika kulikuwa na fedha pia imeripotiwa kwamba fedha hiyo haikupelekwa benki, takribani shilingi milioni 627. Kwa ushahidi huu unaweza ukaona ni kwa jinsi gani fedha za Serikali zinavyopotea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, nini kifanyike? Kwa hali ya sasa hivi jinsi ilivyo inaonekana kabisa utaratibu unaofanyika kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa maana ya Auditor, jinsi anavyoripoti haioneshi kama kutakuwa na dalili ya tatizo hili kwisha. Kwa sababu gani? Yeye anavyokwenda kukagua anaenda moja kwa moja kukagua halmashauri, akishakagua yeye anaripoti kwa Bunge kwa maana ya Kamati ya LAAC na Kamati zingine. Akisharipoti pale, anatoa copy kwa Serikali akiiambia Serikali mambo ambayo amekutana nayo lakini kwa kuishauri marekebisho yafanyike wapi na wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, akisharipoti huku LAAC, sisi kama wasimamizi wa Serikali tunafanya majadiliano kama hivi na mwisho wa siku hatuna maamuzi ya kufanya ya kumchukulia mtu hatua. Yaani tumekuwa hatuna meno. Kinachofanyika sasa, sisi tunaishauri tena Serikali, tunawaambia kwamba fanyeni marekebisho, chukueni hapa, fanyeni hapa. Jambo ambalo ni kama vile mtoto aliyekosea, jirani amekosewa halafu anamwambia mwenye mtoto amuadhibu mtoto wake kwa kosa alilolifanya. Sidhani kama kitu kama hicho kinaweza kikafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa hali hiyo, tatizo ni nini? Nashauri kama tatizo ni sheria, naiomba Serikali kufanya jitihada ya kuileta hiyo sheria hapa kusudi tufanye mchakato wa kuirekebisha, kusudi Bunge liwe lina maamuzi sahihi ya kuweza kumwajibisha mtu yeyote yule au chombo chochote kile ambacho kimekutwa na ubadhirifu wa fedha za umma, la sivyo tutakuwa tukiongea hapa kwa mtindo huu na ndivyo ilivyo miaka nenda, rudi tunakuwa tukisema hapa fedha zinapotea, fedha zinapotea, hakuna action yoyote inayochukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, unasema kwamba TAKUKURU waende kufanya uchunguzi, wanaenda kufanya uchunguzi vipi wakati tayari uchunguzi ulishafanyika. Kwa mfano, uchunguzi uliofanyika wa special audit. Ule ni uchunguzi sahihi ambao una ushahidi wa kuweza kumpeleka mtu mahakamani. Inakuwaje uchunguzi unaostahili kumpeleka mtu…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mchungahela kwa mchango mzuri.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)