Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Bakar Hamad Bakar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye hoja hizi za Kamati zetu tatu ambazo ni Kamati ya PIC, PAC pamoja LAAC. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa zawadi yake hii ya uzima na wa afya njema na kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu jioni hii kuweza kuchangia machache ambayo tumeyaona kwenye Kamati yetu ya PAC.

Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kuitumikia nchi yetu. Kwa kweli tunampongeza sana na tunamwambia aendelee kupiga kazi na sisi tuko nyuma yake, tunamuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mchango wangu leo nitaelekeza kwenye Kamati ya PAC na moja kwa moja nitazungumzia mambo matatu. Jambo la kwanza nitaangalia dosari katika usimamizi na ufuatiliaji wa mikataba. Moja ya miongoni mwa eneo ambalo Kamati yetu ya PAC imetumia muda mrefu kuchambua na kuangalia kwa kina ni eneo la namna gani mikataba yetu tunayoingia kwenye taasisi mbalimbali inavyoweza kusimamiwa na inavyoweza kufuatiliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna dosari nyingi sana kwenye eneo hili na naiomba sana Serikali iangalie upya kwa namna ambavyo tunaweza kusimamia kwa sasa kwa kweli bado tuna changamoto kubwa sana kwenye usimamizi wa mikataba yetu na kwenye ufuatiliaji wa mikataba yetu, jambo ambalo linapelekea hasara kubwa kwa Serikali lakini pia upotevu wa fedha nyingi lakini na ucheleweshwaji wa miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa kupitia maeneo mbalimbali au sekta mbalimbali ambazo zinatekeleza miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tumepata taarifa kwamba Serikali tutaenda kutekeleza miradi kupitia EPC+F pamoja na PPP. Sasa kama hatukuwa makini sana kwenye suala la usimamizi wa mikataba, kiukweli tutaenda kuisababishia Serikali yetu hasara kubwa sana na mabilioni ya fedha yatapotea kupitia mifumo hii ambayo tunakwenda kutekeleza miradi kupitia mifumo mipya hiyo ambayo nimeitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia tu mfano wa fedha ambazo zimepotea. Kwa mfano, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ambapo ilitakiwa ilipwe shilingi milioni 134, imelipwa shilingi milioni 154. Hii ni kwa sababu tu ya usimamizi mbovu na ufuatiliaji mbovu wa mikataba yetu. Ukiangalia pia ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, hali iko hivyo hivyo zimelipwa shilingi milioni 200 zaidi. Kwa hiyo hii ni mifano tu kuona kwamba mikataba yetu namna tunavyoweza kusimamia na namna ambavyo tunaweza kuifuatilia, kwa kweli tuna dosari kubwa na tuna udhaifu mkubwa sana Serikalini kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili niangalie kwenye mwingiliano wa majukumu ya kiutendaji kwenye taasisi zetu, mamlaka mbalimbali na mashirika mbalimbali ambayo yapo Serikalini. Kwenye Kamati yetu sisi hatukatai taasisi kushirikiana, lakini tunakubaliana na jambo hili endapo ushirikiano huo utaenda kuongeza ufanisi, ubora na utaenda kupunguza gharama za utekelezaji wa miradi hiyo ambayo wanaenda kushirikiana. Kwa hali ilivyo sasa, hatuoni kwamba kuna umuhimu kwa baadhi ya mashirika au kwa baadhi ya taasisi kuweza kushirikiana. Kwa sababu kwa mfano tu TAA (Tanzania Airport Authority) pamoja na TANROADS wanashirikiana kwenye ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitegemea kwamba ushirikiano wao utupe ufanisi mkubwa kwenye utekelezaji wa majukumu ambayo wamepeana, utupe ubora kwenye kazi hizo ambazo wanazifanya na gharama pia ziwe chini kwenye mambo haya ambayo wanashirikiana, lakini hali ni tofauti sana. Kwa mfano, kuna hasara ya zaidi ya shilingi milioni 236 ambayo Uwanja wa Ndege wa Dodoma, TAA walienda kuondoa taa uwanjani pale ambazo zilikuwa zinatumia nishati ya jua na wakaweka nishati ya umeme, taa nyingine ambazo taa hizo ziliwekwa na TANROADS. Kwa kweli ni hasara kubwa za Serikali, zaidi ya shilingi milioni 236 zimepotea kwa sababu tu ya ushirikiano dhaifu uliopo baina ya taasisi hizi mbili, TAA pamoja na TANROADS.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizo hizo taasisi mbili zimesababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga, kwa sababu mkataba na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya uliingia baina yake pamoja na TAA, lakini mkataba huo ukataka kupewa TANROADS jambo ambalo ilichelewesha sana utekelezaji wa mradi huu. Tunaiomba sana Serikali, kwenye ripoti yetu sisi tumeshauri kwamba majukumu yote ambayo yanahusika na ujenzi wa viwanja vya ndege yarudishwe kwa taasisi ambayo inahusika na viwanja vya ndege ambayo ni TAA. Kwa hiyo naiomba sana Serikali izingatie mapendekezo haya, izingatie ushauri huu kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo nataka nichangie, ni namna Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inavyoweza ku-operate hapa katika nchi yetu. Tunayo Mifuko mingi ambayo hapa imetajwa kwamba kuna Mifuko zaidi ya 52, lakini tunaona ufanisi na utendaji wake bado ni mdogo. Tunaona kwamba control na usimamizi wa Mifuko hii ni jambo linalopelekewa na sababu ya kutosomana kwa mifumo hii na hivyo mtu anaweza akakopeshwa kwenye Mfuko mmoja na mtu huyo huyo akaenda akakopa kwenye mfuko mwingine bila ya kujulikana kwa sababu mifumo hii haisomani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mtu mmoja anaweza akakopeshwa na zaidi ya Mifuko miwili au mitatu, kitu ambacho kinapelekea mikopo chechefu mikubwa ambayo tumeiona. Mfano wa mikopo chechefu hiyo ni Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, zaidi ya shilingi bilioni 20.1 zimepotea kwenye mifuko…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Hamad Bakar.

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)