Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie taarifa ya mwaka 2020/2022. Kwanza napongeza Kamati zote tatu kwa mawasilisho yake mazuri. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC, nitachangia yale ambayo tumeyaongelea katika Kamati yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika maeneo matatu. La kwanza ni changamoto ya mitaji katika taasisi; ya pili, ni TANAPA na ya tatu ni mali ghafi katika viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na changamoto za mitaji. Tunalo Shirika la TEMESA. Shirika hili linafanya kazi ya kutengeneza magai ya Serikali yaliyo mengi pamoja na kampuni. Serikali imewekeza mtaji na linajiendesha mpaka sasa hivi shirika hili linasuasua, limekuwa na madeni makubwa ambapo Serikali hii ambayo imewekeza, imeikopa taasisi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka dakika hii TEMESA inadai shilingi milioni 45.39. Haiingii akilini kwamba sasa hivi kule ambako tunategemea tupeleke magari yetu TEMESA wao wanafika mahali hata vipuri vya kutengenezea magari yetu hawana. Wanashindwa hata kutoa gawio katika Mfuko wa Serikali kuu kwa kuwa hawana fedha za kuendeshea taasisi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uchambuzi wa Kamati tunaishauri Serikali ihakikishe kwamba inalipa madeni yote ya TEMESA na kuhakikisha kwamba inatengeneza utaratibu mzuri ambao utakuwa ni utaratibu wa prepaid yaani tengeneza, lipa, ili kuhakikisha kwamba madeni mengine hayazalishwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia TEMESA, nakuja katika Shirika la Hifadhi, TANAPA. Wabunge wengi wamesimama kuongolea suala la TANAPA. Mwanzo TANAPA ilikuwa ina hifadhi 16, mpaka sasa hivi ina hifadhi 22, lakini kwa bajeti ile ile ambayo ilikuwa inaendeshea ikiwa na hifadhi 16.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kwa sasa ongezeko la hifadhi sita halitatosheleza bajeti ya kuendeshea shirika hilo. Ikumbukwe kwamba kuna changamoto mbalimbali ambazo barabara zetu zinazoingia katika hifadhi siyo rafiki, hivyo zinahitaji kufanyiwa ukarabati ili kuleta tija hasa watalii wetu wanapokuja kutembelea wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto nyingine ambayo ni maji. Serikali inabidi ijipange katika kujenga mabwawa ili kuepusha ule utamaduni ambao naweza nikauita utamaduni wa wanyama kutoka katika hifadhi na kuja katika makazi ya watu na baadaye kuleta athari ya watu kufariki na kuharibiwa mali zao. Kamati imechambua kwa kina, inaishauri Serikali ihakikishe kwamba inaongeza fedha za kutosha katika shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika viwanda vyenye changamoto ya mitaji. Nichangie kuhusu Kiwanda cha Ngozi cha Kimataifa cha Kilimanjaro kilichopo Manispaa ya Moshi Kata ya Karanga. Tulienda kutembelea kiwanda hicho, tulifika tukaona jinsi walivyo na vitu vizuri, na bahati nzuri pia walishakuja kutembelea Bunge wakaleta bidhaa zao tukaziona. Cha kusikitisha ni kwamba kiwanda hicho hakina malighafi za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Halmashauri zetu, Watanzania tunachinja sana ng’ombe na mbuzi. Ni vizuri Serikali ikajipanga sasa kupitia Halmashauri zetu, sekta ya mifugo wakahakikisha kwamba ngozi zile ambazo zinachinjwa zinahifadhiwa vizuri ili hatimaye ziweze kuja kuuzwa katika viwanda vyetu ili viweze kufanya kazi na vilete tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)