Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya mimi kuchangia au kutoa mawazo yangu kwenye hoja za kamati zilizowasilisha ripoti zao za mwaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Kamati ya Sheria Ndogo. Kwa hiyo zilizoko mezani ni taarifa za mwaka za kamati mbili naomba mchango wangu niuelekeze wenye Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jukumu na mamlaka ya kutunga sheria za nchi hii ni mamlaka ya Bunge. Hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Ibara ya 4 ikisomwa sambamba na Ibara ya 64 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake yote. Kwa hiyo, mamlaka yote ya kutunga sheria za nchi hii yako kwenye chombo hiki cha Bunge ambacho sisi tunakitumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Katiba hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikatoa mamlaka ya kukasimu madaraka hayo ya Bunge kwa vyombo visivyokuwa Bunge ili vilisaidie Bunge kutengeneza Sheria kwa ajili ya kuleta mustakabari mzuri wa maendeleo ya wananchi wa Tanzania. Hiyo ipo kwenye Ibara ya 97(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaratibu unatolewa kwenye sheria za nchi (principal laws), ambapo kwenye Sheria ya Tafsiri ya Sheria CAP 1 kwenye Kifungu cha 37 na 38 kinatoa utaratibu, vipi vyombo visivyokuwa Bunge vitatunga Sheria na vitapita katika utaratibu gani. Kwa hiyo, baada ya sheria kutungwa, kwa utaratibu uliopo, sasa kwa sheria zetu ni kwamba zitaingia mtaani na zinaanza kutumika baada ya kupata sahihi za waliopewa mamlaka ya kutunga sheria; aidha mawaziri au wakurugenzi, kwa zile sheria zinazotoka kwenye taasisi, na baada ya kutangazwa kwenye gazeti rasmi la Serikali, sheria hizo zinaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa utaratibu ni kwamba Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo inakuja kukutana na sheria hizo wakati sheria zikiwa zimekwisha ingia mtaani na zinafanya kazi. Sasa sisi tunatekeleza wajibu wetu wa kisheria wa kuzisimamia na kuzipitia sheria hizo ili kuona kwamba tuliowakasimu madaraka hayo hawayavunji? Hawayatumii wanavyotaka wao? Huo ndio wajibu wetu namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zinavyokuja mbele yetu sisi tunazipitia halafu tunatoa mapendekezo yetu na marekebisho kwa hizo taasisi zilizotunga kanuni hizo. Kwamba tunapoona sheria hizo zimevunja aidha Katiba au sheria mama au haziendani na uhalisia, tunawambia nendeni karekebisheni au nendeni kafuteni hii wekeni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumezuka tabia ambayo si nzuri kidogo na ni lazima kama Bunge tuikemee. Maazimio ya Bunge kwa Serikali ya kurekebisha baadhi ya kanuni tunazowambia hayarekebishwi. Hilo ni jambo baya sana sana sana sana; kama taasisi hatutakiwi tuliache hata siku moja. Tuiachie Serikali wasirekebishe marekebisho tunayowapa aidha Kamati au Bunge zima linapofanya Maazimio baada ya Kamati kuleta taarifa yake ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo tumeyabaini kwamba tangu kikao cha Bunge la 5, 6, 7 mpaka leo Bunge la 10 hayajarekebishwa; bado yako mtaani na yanaumiza watu. Kuna kanuni hazifai kabisa hata kuziona, ziko mtaani na zinaumiza watu. Kwa sababu hizi kanuni tunazozipitia ndiyo maisha ya watu ya kila siku huko mtaani na wananchi wetu. Kwa hiyo sisi tunaposema zikarekebishwe kunapita zaidi ya miezi 6, 7, 8 hazijarekebishwa hivi tunategemea nini? Ni kanuni zinaendelea kuumiza watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi nataka nitoe mfano mmoja. COSOTA walituletea kanuni moja hivi, walikuwa na kanuni yao inaitwa Copyright and Neighboring Right Regulation GN 137. Kwenye kanuni yao hiyo COSOTA walikuwa wana kipengele kwenye Kanuni ya 3 (2) na (3); ya kwamba mikataba yote ya wasanii wa nchi hii wanayoingia aidha na taasisi au ma-promoter au mtu yeyote lazima mikataba hiyo ipite COSOTA. Sasa walivyokuja kwenye kanuni tukawauliza mnataka kutibu nini? Mbona kama vile sheria itashindwa kutekelezeka? Unataka msanii aliyeko Geita Vijijini achukue mkataba wakati Geita hakuna hata Ofisi ya COSOTA aulete Dar es salaam ili wewe uje uipitie wewe nani? Mnataka kutibu nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakatuambia malalamiko yamekuwa mengi sana ya wasanii kuwa wanadhulumiwa kwenye mikataba, hawajui, wanasaini mikataba wakiwa hawavijui vipengele. Kwa hiyo sisi tunataka tuwasaidie wasanii. Hata hivyo, behind wameweka kila mkataba watakaoupitia wata-charge asilimia moja ya value ya mkataba huo iende COSOTA ili wao wapate hiyo nafasi ya kutibu. Tukasema hii sio sahihi. Msanii akiona iko haja ya mkataba wake anadhulumiwa atatafuta mwanasheria. Kama ninyi COSOTA kama taasisi ya Serikali mnataka kusimamia msiweke ulazima, anayetaka aje, lakini si lazima. Kuna wengine wameshatoka huko wana wanasheria wao binafsi, unamlazimishaje aje COSOTA? kwa hiyo, toka Mkutano wa Tano jambo hilo halijarekebishwa hadi leo. Lipo hivyo na linaendelea kuumiza wasanii wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria tukishasema, tukishatoa maazimio kuna tatizo lingine la kukaa muda mrefu sana kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Zinakaa kwa muda mrefu zikisubiri uhakiki au zikisubiri zipate GN. Ziko sheria za tangu Mkutano wa Sita na wa Saba mpaka leo. Serikali wakija kwenye Kamati yetu tukiwauliza mmefikia wapi kwenye kurekebisha yale mliyoambiwa mrekebishe na Bunge? Wanakwambaia sheria sisi tulikwisha rekebisha zilishapata saini ya Waziri lakini hadi leo zipo kwa Mwanasheria Mkuu hazijapata GN au nyingine zinasubiri uhakiki. Si sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo kanuni za halmashauri ndogo ya hifadhi ya mazingira ya Itigi. Kanuni hizi kwa mfano zilikuja na mapendekezo kwamba mtu yeyote anayekaa kwenye Halmashauri ya Itigi anayetaka kufuga, atafuga kwa idadi ambayo halmashauri itamwambia afuge. Kwa hiyo, walivyoleta kwenye sheria yetu tukawaambia hii sio sahihi, haiwezejkani kuwa hivi. Kwa nini halmashaurri mumpangie mtu mifugo? Hata kama mnataka ku-control mazingira mnaweza kuweka kwenye kanuni idadi ya mifugo mnayotaka lakini si maamuzi ya Mkurugenzi au Mtu yeyote kwenye halmashauri Kwenda kusema sasa wewe ng’ombe fuga 50, wewe utafuga 30, wewe kuku fuga hivi, si sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukawambia kwamba nendeni karekebisheni. Wamekuja kwenye Kamati ya Bunge hili tunauliza mmefikia wapi? Wanasema sisi tumekwisha saini rasimu ya marekebisho lakini hadi sasa rasimu hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti, iko kwa Mwanasheria Mkuu haijapata GN Number. Hili ni jambo ambalo linaendelea kuwaumiza wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano ipo mingi sana kwa sababu zinakuja kanuni nyingi ambapo kanuni nyingine hazitekelezeki, kanuni nyingine wanaleta masharti ambayo yamepitwa wakati. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni lazima tuchukue hatua kama Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ikishamaliza kufanya kazi yake na taarifa yake ikishasomwa ndani ya Bunge, Bunge linatoa maazimio ya jambo hilo likarekebishwe, likafanywe; sasa wewe unakuja kwenye Kamati kuja ku-negotiate Maazimio ya Bunge wewe nani? Bunge lishasema nenda karekebishe, karekebishe si wakati tena wa kuja kutuambia sisi tulivyoona hii ilikuwa si sahihi. Wabunge wote hawa 396 jambo hilo baada ya kuliazimia waliona si sahihi nyie watu wawili tu wa Wizara mkalione ni sahihi kweli jamani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naunga mkono hoja kwa taarifa zote mbili. Ahasante sana.