Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi; na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa yetu ya Kamati ambayo itakuja kwenye Bunge hili. Tunaendelea kuishauri wabunge wenzetu waiunge mkono liwe Azimio la Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nina jambo dogo katika suala zima la ajira. Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana imebeba majukumu makubwa sana katika nchi hii. Suala la ajira sasa limekuwa ni mzigo kwa jamii. Vijana wetu wanasoma na wengi wamehitimu vyuo vikuu lakini nafsi za ajira eneo lililo rasmi zimekuwa ni chache sana, na hata zinapotoka zinakuwa na changamoto. Msemaji aliyetangulia Mheshimiwa Ole-Lekaita hapa amezungumzia ni namna gani bora sasa Serikali ifanye. Mimi naendelea kushauri Serikali ione namna bora ya kufanya mgawanyo wa ajira hizi, aidha kwa mikoa au kwa wilaya na hata kwa majimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapozungumza mwaka 2023 hakuna jimbo ambalo halina wasomi, hakuna jimbo ambalo vijana wake wamekaa wanasubiri wamepata ajira; majimbo yote Tanzania. Hata hivyo, zinapotoka nafasi za ajira utaona tu wametoka kwenye zone fulani au kwenye eneo moja fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo Halmashauri 184; kama nafasi zipo hata kama ni 2000 ukazigawanya kwa hizi halmashauri halafu yale majiji ambayo pengine yanapendelewa zaidi yakaongezewa na manispaa shida iko wapi? Juzi tu hapa tumeona watu wa Idara ya Polisi, wamefanya vizuri sana wamegawanya ajira zile kwa mikoa na kule mikoani wakazigawa kwa wilaya, maana yake zimegusa eneo kubwa. Je, upande wa ajira hizi za walimu na madaktari, wauguzi na maeneo mengine ya Serikali mnashindwaje kuzigawanya katika mfumo huu ambao IGP wa sasa aliyepata nafasi juzi ameonesha njia? Naomba sana Serikali ilione jambo hili kuwa ni la kuigwa na la mfano; ajira hizi zizingatie uwiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge miongoni mwetu hapa hakuna Mbunge kwa inapotoka nafasi za ajira anakosa meseji kumi au kumi na tano za watu ambao wantaka kusaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti ule mfumo wenyewe mimi naona kama hauko sawa, ule ambao unahusika na ajira za watu. Unaambiwa mfumo ndio unachagua, utachagua kutona miaka, lakini unakuta ameajiriwa mtu wa mbele yake wa nyuma ameachwa; na mfumo huohuo unaangalia wanasema huwa tunazingatia miaka unaangalia mtu mwenye miaka mingi ameachwa nyumbani kijana mdogo amechukuliwa. Huu mfumo nini faida yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa Serikali ione changamoto hizi zinaumiza wananchi vijana wetu wanaanza kukosa imani na Serikali yao kwa sababu ya matukio kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili lisilo rasmi la kurasimisha vijana wale wanye ufundi. Hapa kulikuwa na ya wanagenzi wanaitwa na Ofisi ya Waziri Mkuu walikuwa wanarasimisha vijana wale wenye ujuzi, wanawapatiwa mafunzo kidogo na kuwapatia vyeti ili watambulike katika jamii na katika maeneo rasmi ya Serikali pengine ya ajira lakini pa waweze kupata kazi zinazotolewa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limekuwa na faida sana; vijana wengi wamerasmishwa wanaitwa wanagenzi na sasa tunaona matokeo mazuri. Hata hivyo bado liko jambo ambalo leo, na hata jana na juzi hapa tumeona changamoto kubwa zavijana wengi ambao wanategemewa kusaidiwanaserikali yetu hii kupitia wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo. Na kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo inasimamia Wizara hizi zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unachukuaje mtu ambaye hakuwahi kulima? Eti unamchukua akalime, na wakulima wanaolima kila siku wapo, na vijana wa maeneo yale wapo, ardhi iko pale; kwa nini usichukue wale vijana walioko maeneo ilipo ardhi ukawawezesha kutokana na mipango yako ile kuliko kumchukua mtu ambaye maisha yake amekuwa anaangalia katuni na bongo fleva halafu leo unamwambia akalime? Baba yake hakuwahi kulima mama yake hakuwahi kulima leo umwambie akalime inawezekana wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo tunatakiwa tujifunze. Unamchukua mtu ambaye hajwahi kuvua, maisha yake yeye ni kijijini kulima, hajawahi kupiga kasia unamwambia leo eti ukamfundishe uvuvi kwa sababu Serikali ina fedha za uvuvi, umpe na chombo; akizamia kwenye maji kwa kushindwa kuogelea unamsaidia nini mtu kama huyu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unamchukua mtu, eti ume- recruit vijana kutoka JKT ukawapa block farm walime ilhali wakulima wanaolima kila siku wapo? Tunafanya biashara gani hapa? Kuna mambo mengi ambayo tumekosea huko nyuma tujifunze kutokana na makosa hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wafugaji wako huko vijijini kwetu, njoo Itigi watu wanafuga; na hata hapa amezungumza mzungumzaji wa kwanza amesema Itigi walitunga sheria watu wasifuge mifugo mingi; kwa sababu mifugo iko mingi labda ndyio maana wakakosea. Lakini mtu yule ambaye anafuga kila siku unampa elimu gani zaidi ya kumuongezea uwezo? Mjengee josho, muwekee ardhi bora ya malisho, mfundishe kulima nyasi, kesho atazalisha ng’ombe walio bora zaidi na kama ni nyama atauza, kwa nini umchukue mtu kutoka JKT ambaye baba yake hajawahi kufuga na yeye mwenyewe hajui hata tabia ya kukaa na ng’ombe halafu unamwambia aende akafuge?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukaa na binadamu tu hapa lazima ujue tabia za watu sembuse kukaa na mifugo? Wafugaji wapo tuchukue wafugaji wakafanye yale masuala yanayohusu mifugo. Tusichukue watu kwa sababu tu wamepita JKT mme-recruit watu na mna hela mkawape kazi ambayo hawataiweza. Tumeona hili katika Azimio la Arusha, tulichua mashamba tukawapa watu waiokuwa na ujuzi, mashamba yakafa baadaye tukashindwa tukaanza kubinafsisha. Tumechukua viwanda tukawapa watu ambao hawana uwezo leo tunalalamika bado tunataka turudie makosa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu hawana ajira lakini wapo kule vijijini unachukua mtu ambaye alikuwa anakaa mjini amesoma kwa sababu amepita JKT eti akapewe block farm kweli tutafika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tilikuwa na kilimo cha kufa na kupona hivyohivyo kilifeli kwa sababu tulikuwa tunachukua watu ambao si wahusika. Juzijuzi tulikuwa na kilimo kwanza imeletwa imeleta mabovu watu wetu wakawa wanashindwa kulima na matrekta yale hata spea hamna baadaye wakawa na madeni makubwa wanadaiwa na hawawezi kulipa kwa sababu tuliwapa vitu ambavyo havifai. kwa nini tusiwanyanyanyue watu ambao wanaweza kufanya kazi zao? Nenda kule Madaba msaidie mkulima wa Madaba, njoo Itigi msaidie mfugaji wa Itigi afuge kwenye ardhi yake. Kwa nini umchukulie ardhi umpe mtu mwingine kwa sababu tu eti ametoka JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hili jambo tuliache, na Serikali iache kufanya vitu ambavyo ni vya makisio. Hakuna mahali tumefaulu kwenye hilo toka tumeanza na bado tunakwenda kwa sababu pesa zinatengwa na Serikali basi tunataka tuwape watu. Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya vizuri sana wameweka yale vitalu nyumba wakapewa vijana wakaelimishwa na wanendelea kwa sababu waliwapa watu wanaolima. Unampa mtu unamnyanyua kutokana na elimu yake lakini na jinsi jiografia ya eneo husika ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sekta nyingine zipo ambazo bado kuna changamoto kwa vijana, wanatakiwa waendelee kupata ajira hizi lakini namna bora ya kuwawezesha ni kupitia Ofisi hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata pesa zinazotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu bajeti tu ya mwaka jana iliyopita tulitenga bilioni moja tu lakini zilizotoka ni milioni mia mbili na tano asilimia 20. 5, leo tunawasaidiaje vijana wetu? Hebu tuwe serious kwenye hili. Natamani kuona leo vijana wa Tanzania wasilalamike kipindi sisi tuko katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na tuendelee kushauri vizuri kwa maslahi mapana ya jamii yetu tusiende kwa mihemko tuna mihemko ambayo inakuja kutugharimu baadaye.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahaya kuna taarifa
T A A R I F A
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, anaendelea vizuri na mchango wake. Nilitaka nimpe tu taarifa. Amesema vizuri juu bilioni moja iliyotengwa kwenda kwenye mfuko wa maendeleo ya vijana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu lakini hela yote imepelekwa kwenye Wizara hiyo au Ofisi hiyo lakini imetoka milioni mia mbili na tano tu asilimia ishirini au kumi na tisa asilimia 79 haijatoka na hela iko pale. Hii inashangaza, Watanzania vijana wengi wanashida wanasema wamekosa vigezo vya kupewa hela hiyo. Kwa nini hela imeenda sasa? Si ingeendelea kubaki hazina ili iendelee kufanya kazi nyingine?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahaya Massare umepokea hiyo taarifa?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio naipokea taarifa. Ni jambo linalokera bajeti imetengwa na watu wanahitaji wenye mahitaji wapo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa Mheshimiwa Yahaya kuna taarifa nyingine hapa.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilikuwa naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kwa fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya vijana fedha tulizopata ilikuwa ni bilioni moja; na ilikuwa haitoki katika kipindi kile kwa sababu zinatokana na SDL, kwa maana ya fedha ambazo zinachangwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika kutoa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini fedha hiyo iliyotelewa, bilioni moja mpaka kipindi kile cha Bunge lile linakaa katika Bunge la Sita la Saba mpaka sasa tunavyozungumza fedha hizo zilikwishakwenda katika Halmashauri hizo zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha shilingi bilioni moja hakionekani sana katika maeneo kwenda kule kwa sababu inachagiza tu katika mfuko wa maendeleo ya vijana fedha nyingi zinatoka kwenye mfuko ambayo inatolewa kwenye halmashauri zile asilimia nne kwa vijana nne kwa wanawake na mbili kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Sasa hii bilioni moja huwa ni ya kuchagiza kwa vikundi vilivyofanya vizuri zaidi. Mpaka ninavyozungumza sasa tayari fedha hizo zimetoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini urejeshaji wake pia ninayo taarifa kwamba tayari tuna zaidi ya bilioni moja ambayo imekusanywa na Mwenge wa uhuru. Kwa hiyo nilitaka tu kusema hilo, ahsante.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahaya Massare unaipokea hiyo taarifa?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii kidogo ina ukakasi. Kwa sababu, taarifa ya Mheshimiwa Waziri wakati anasoma hapa mbele alituambia kwamba fedha ile waombaji walikosa vigezo, ndiyo taarifa ya Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo ni vizuri tukasahihisha ili tusaidie watu wetu. Tuko hapa kuishauri Serikali kwa maslahi mapana; kwamba inapotengwa fedha itoke na kama haikutoka zije sababu. Vijana wangu wa Itigi kule wanahitaji hizo fedha, hazipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naendelea kuishauri Serikali, kwamba ione namna bora ya kubeba hili ambalo baadaye tunapata dhana kwamba vijana wetu watakuja kukosa imani yao kwa sababu ya hizi changamoto ndogo ndogo. Kule kwenye halmashauri akina mama wanapata zile fedha, kwa kweli hakuna shida, lakini vijana bado ni changamoto. Kwa hiyo tuendelee kusaidia hawa vijana ili nao siku moja wasaidie hili Taifa. Tutakuja kuwa na vijana ambao ni nguvu kazi lakini hawafanyi kazi kwa sababu fursa hizi zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anachukuliwa kutoka JKT anapelekwa Itigi eti akalime, akalime majani. Wale wa Itigi hawapewi. Kweli hii fursa hii haifanani katika sura hii na ndiyo maana tunashauri ajira za Serikali zilenge kwenye majimbo kama alivyosema Mheshimiwa Olelekaita au zije kwenye Wilaya, zitakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja ya Kamati.