Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata fursa hii leo kuchangia taarifa ya Kamati yetu ya Katiba na Sheria. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai mpaka sasa, na jana nimeongeza mwaka mwingine, mwaka ambao mwaka umeinifanya nitafakari mambo mengi sana, leo hii nataka nizungumze na Bunge hili Tukufu lakini na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu fika kwamba Tanzania yetu inachukua hatua mbali mbali za kusaidia watu wenye ulemavu. Nafahamu fika Serikali imeleta mwongozo mzuri juu ya kuimarisha, kusaidia hali ya watoto ya watu wenye ulemavu. Hata hivyo, naomba niliambie Bunge hili Tukufu hali ya watu wenye ulemavu ni ngumu zaidi kuliko tunavyofikiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika likizo ya ya mwezi wa 11 na wa 12, nilipata kufanya ziara kwenda katika vituo mbalimbali vya watu wenye ulemavu. Mambo niliyoyaona kule ni magumu sana hata kuayelezea. Mfano tu mzuri nichukue hapa Kongwa nilenda katika Kituo cha Mlali, nimekuta kuna watoto wenye ulemavu wa viungo wako pale wanalelewa na Kanisa Katoliki la pale Mlali. Hali niliyokuta pale inatia huruma sana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wamepelekwa pale kwa ajili ya kupata huduma ya afya ya kunyooshwa viungo mbalimbali lakini pia kupata huduma ile ambayo kuna madaktari wa KCMC na madaktari wengine kutoka nje ya nchi wanakuja pale kwa ajili ya kusaidia au wanajitoa. Wazazi wamekuwa wakipeleka watoto wao pale lakini wazazi wengine wameshindwa kwenda kuwaona watoto wao katika vile vituo kwa sababu kile kituo kina chaji shilingi 130,000 kwa ajili ya mtoto kupata huduma katika eneo lile. Sasa najiuliza, kwa Mtanzania wa kawaida anaweza kumudu hii shilingi 130,000 kwa ajili ya mtoto wake kupata huduma katika kituo kile? Mtanzania wa kawaida kila mwezi, 130,000 anaweza? Hilo ni swali la kujiuliza sisi Wabunge humu ndani ambapo katika maeneo yetu vituo kama hivi vipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuangalia tu, mzazi anayeshindwa kulipia hiyo anamwacha mtoto wake pale anaondoka harudi tena kumwona, watoto wanatelekezwa katika vituo vile kwa sababu huyu mzazi anaona fika kabisa kwamba mimi sina hii fedha, naendaje pale. Nitakabidhiwa huyu mtoto, nitawezaje kumhudumia? Ningeomba sana Serikali iangalie hili jambo kwa upande wa pili waone kabisa zaidi. Wazazi wanaozaa watoto, wenye watoto wenye ulemavu wanapata shida ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mama yangu aliwahi kuniambia wakati nazaliwa, kabla baba yangu hajaja kuniona hospitali. Kuna mtu aliwahi kumuuliza kwamba hivi, unafikiri Shabani ataweza kumpokea huyu mtoto? Atamkubali kweli? Hii ni changamoto ambayo wazazi wengi wanakutana nayo, lakini cha kushangaza baba yangu aliponiona alinifurahia na kunikumbatia na leo hii nimefika hapa nilipo. Kwa sababu familia yangu iliweza kunikubali na kunilea na leo hii mimi sijioni kama ni mtu mwenye ulemavu; na watu wengi humu ndani wananiambia kwamba wewe mbona siyo mlemavu? Ni kwa sabau nimelelewa vizuri na familia ambayo ilinikubali na changamoto zangu na kunilea hadi nilipofika hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuangalie, ni familia ngapi zinamudu? Akina mama wengi wamekuwa wakitelekezwa na mababa kwa ajili ya kuzaa watoto wenye ulemavu na wanabaki na watoto wale wanawalea wenyewe. Wanapata shida nyingi mno. Leo hii Bunge hili, hapa akija mtu mwenye ulemavu wanatoa huduma ya msaidizi, kwa sababu wanafahamu fika kabisa huyu mtu mwenye ulemavua ana changamoto, hawezi kujihudumia mwenyewe lazima apate msaidizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tujiulize, yule mzazi ambaye yupo nyumbani, amezaa mtoto mwenye ulemavu, ni msaidizi gani, ni familia gani au ni ndugu ugani ambaye anaweza akakaa na huyu mtoto ambaye ana ulemavu atakulelea wewe? Ina maana huyu mzazi hana budi akae nyumbani, aweze kumlea huyu mtoto, amhudumie mwingine hawezi hata kujilisha mwenyewe. Hawezi hata kuoga mwenyewe. Je, Serikali inamfikiria vipi huyu mama ambaye hawezi kufanya shughuli nyingine zaidi ya kumlea mtoto wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa naona kabisa Serikali ione namna na haja ya kuona fika kabisa kwamba waone hawa wazazi either watafutiwe wasaidizi, kwamba Serikali ichukue jukumu la kulea au watafute namna ya kuwawezesha hawa wazazi waweze kupata fedha kupitia zile asilimia mbili. Asilimia mbili ile isaidie akina mama ambao wana watoto wenye changamoto ya ulemavu waweze kujikwamua kiuchumi ili tuone namna gani tuweze kuona hawa watu waweze kulea watoto wao, waone fika kabisa na wao ni part ya Tanzania hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri upo pale katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mtu mwenye ulemavu akifika pale anapata msaidizi kwa siku analipiwa shilingi 10,000. Anapata bajaji ya kwenda kumpeleka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Hivi vitu vyote tunafanya juu huku. Bunge linafanya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinafanya; lakini vipi huku chini kwenye ngazi ya familia? Kwa sababu kama huyu mzazi ameweza kutelekezwa na mwanaume kwa ajili ya kulea, ndugu pia wanaweza kuona kwamba huu ni mkosi kwenye familia yetu. Analeaje huyu mtoto?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, Bunge hili naamini kabisa, watu wote sidhani kama kuna mtu ambaye hajawahi kufuatwa na shida za watu wenye ulemavu; na ukiangalia fedha ya jimbo haiangalii kusaidia watu wenye ulemavu. Watu wanaingia kwenye mifuko yao kusaidia watu wenye ulemavu. Juzi tumepata takwimu ya sensa lakini bado majibu hatujayapata ya kujua idadi gani ya watu wenye ulemavu ambao wapo katika hii nchi ili Serikali sasa iweze kusaidia. Sasa tunahitaji zile takwimu ili tujue katika kila jimbo kuna watu wangapi wenye watoto wenye ulemavu wanawalea ili sasa Serikali ione haja na Bunge hili lishauri namna gani ya kusaidia hawa wazazi wenye hawa Watoto?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii naamini kabisa jambo lolote likija whether kwa kukatwa tozo, whether kwa kukatwa mishahara yetu sidhani kama kuna mtu humu ndani ataweza kuwa na sauti ya kusema kwamba jambo hili hapana, wananchi watakasirika kwa ajili hawataki kuhudumia watu wenye ulemavu. Sasa hivi tumeona kabisa watu wanatafuta namna ya kujikwamua kiuchumi wanatumia watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna tamthiliya ya Juakali. Ukiangalia mazingira ya ile tamthiliya mule ndani Mtu ana NGO yake anaita watu wenye ulemavu anatengeneza story apate fedha halafu anajinufaisha yeye na familia yake. Yale ndiyo maisha halisi ya huku nchini, siyo tamthiliya ile. Kuna mzazi mwingine ana mtoto wake mwenye ulemavu amemficha ndani, anashindwa namna ya kutoka kwenye jamii, anaona ni aibu, anaona ni mikosi. Hivi vitu si kwenye tamthilia, ni maisha halisi ya Watanzania. Sasa Bunge hili lione namna halisi ya kusaidia watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais. Amekuja na huu mwongozo, ni mwanzo mzuri mno, Serikali mmeanza vizuri mno. Sasa kwa Serikali hii mama, kama Mheshimiwa Rais unanisikia, ninakuomba usije kuondoka katika Serikali hii kama haujatatua shida za watu wenye ulemavu kuona namna gani ya kusaidia. Kwa sababu ukiangalia idadi ya watu wenye ulemavu katika nchi hii ni wachache mno na Serikali hii ikiipa kipaumbele, hatushindwi kitu. Kuna kampuni nyingi tu ambazo zinafanya kazi katika nchi hii. Kuna fedha nyingi wanazo, CSR sijui nini na nini. Mfuko wa watu wenye ulemavu ni muhimu kulea watoto wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Bunge hili Tukufu, endapo sheria hii itakuja muiunge mkono, kwa sababu naamini kila mtu hapa ni mlemavu mtarajiwa. Kwa sababu naamini kuna Wabunge humu ndani wamekuja wakiwa wazima na sasa hivi ni watu wenye ulemavu na leo hii sisi tuna watu tunawazaa humu ndani, tutazaa watoto wenye ulemavu. Leo hii tukitengeneza msingi mzuri au tathmini nzuri ya watu wenye ulemavu kuishi vizuri, tunajitengenezea sisi wenyewe na kizazi chetu cha baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)