Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nitoe mchango kidogo kwenye hotuba hii ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Kwanza kabisa nianze kwa ku-declare kwamba na mimi ni moja kati ya wale wasanii ambao tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba sasa tunatambulika rasmi kwenye Wizara. Lakini nimesimama kwa ajili ya mambo mawili tu au matatu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kumpongeza Mheshimiwa Rais na kumshukuru kwamba nilipoingia mwaka 2005 ndani ya Bunge hili, kwa kweli kulikuwa hakuna namna yoyote au neno lolote kuanzia kwa Waziri au Mbunge aliyezungumzia suala la sanaa. Lakini tulilianzisha na hatimaye Serikali ya Awamu ya Nne ikaweza kulitambua na kuanza kulifanyia kazi. Nitoe pole sana kwa wasanii wengi ambao wamekuwa kwanza ni maarufu kwa kujitahidi wao wenyewe, wamekuwa ni maarufu kwa kufanya kazi katika mazingira magumu, lakini na wengine ambao wana vipaji wameshindwa kuendelea kutokana na taratibu ambazo hazikuwa zinatambuliwa rasmi katika mfumo ambao sasa hivi umewekwa na Rais huyu wa Awamu ya Tano kwa kweli nampongeza na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kasi kubwa ambayo wameianza sasa inayoonekana. Ninapongeza kwamba ameweza kuzindua tamasha la filamu la Kimataifa pale Arusha ambalo naamini tamasha lile ni mwanzo mzuri utakaowapa fursa wasanii wetu kutangaza kazi zao ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo, ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niseme jambo moja, Mheshimiwa Waziri kwamba sanaa haikuwa na Wizara ambayo tumeililia pamoja na wasanii wenzangu ambao tuko ndani ya Bunge hili. Kwa umoja wetu tuliweza kushirikiana kulilia ili sanaa hii sasa iweze kupewa nafasi katika Wizara. Umepewa nafasi sasa, hebu ninaomba kwa sababu inaonekana kuna wasanii ambao wanaonekana labda ni wakubwa sana, wengine ni wadogo sana au kuna ubaguzi. Mimi nataka niwashukuru sana wale watu, vyombo mbalimbali na taasisi mbalimbali ambazo ziliwasaidia wasanii wetu hadi kufikia hapa walipo kwa sababu Serikali ilikuwa haijatia mkono wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vyombo mbalimbali ambavyo vimekuza vipaji vya wasanii hata tukizungumza Diamond, Diamond amepitia kwa ndugu Ruge kwa kweli tunawapongeza, mimi binafsi kuna wasanii wengi wamesaidiwa hata tulikuwa na kina Saida Kalori walisaidiwa, wakakuza vipaji vyao. Ninapongeza vyombo hivyo kwa sababu walihangaika, ndugu Msama alijitolea kuanza kukamata kazi za wasanii ambazo zilikuwa zinaibwa, kwa sababu Serikali ilikuwa haijatia mkono wake pale, kwa hiyo mimi napongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mzee King Kiki ambaye leo tunae hapa, wazee hawa wamepata taabu kubwa, wamehangaika, Serikali haikutia mkono kule kuwasaidia lakini wameweza kufika hapa na wametangaza pia kazi za sanaa na Taifa letu, mimi ninawapongeza wote.
Lakini Mheshimiwa Waziri, tunayo mashirikisho ambayo mashirikisho haya yako manne, kuna Shirikisho la Filamu lina vitengo vyake, kuna Shirikisho la Muziki lina vitengo vyake, kuna shirikisho la Sanaa za Ufundi na Shirikisho la Sanaa za Maonyesho. Ukienda kwa mfumo huu ukapitia mashirikisho haya, hii kuonekana kwamba wasanii sasa wanatengwa, nafikiri haitakuwa na mashiko maana yake hata sasa hivi sina hakika kama umealika viongozi wa mashirikisho haya, sana sana utakuwa umeita watu wachache kuja kuwawakilisha wasanii.
Kwa hiyo, ninaomba ufanye kazi na mashirikisho haya, wao watakueleza ni nini adha na wanahitaji kufanya mambo yapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashirikisho haya yatakusaidia katika mambo mengi, kwa mfano, msanii aliyepo Kigoma, Singida au Mtwara kuwe na branches kule ambazo wao watatambulika kule. Kwa sasa hivi msanii hawezi kukopesheka pamoja na kipaji alichonacho, pamoja na kazi nzuri aliyonayo hatambuliki, lakini anapokuwa ni mmoja kati ya wanachama ambao ni wanachama katika mashirikisho haya, ninaongea kwa kifupi kwa sababu yana mapana na marefu yake lakini yatasaidia sana. Kwa hiyo msanii huyu anaweza akakopesheka kupitia haya mashirikisho, lakini unaweza ukamtambua kupitia pia kwenye haya mashirikisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la COSOTA. Ni kweli nilikusikia kwamba unasema COSOTA ihamie kwenye Wizara yako na sisi tutakuwa na furaha ikihamia kule. Sasa hivi inakusanya mrahaba kwenye vyombo mbalimbali redio, tv, magazeti na kila kitu, lakini nani anasimamia kujua msanii fulani, kuna chombo gani ambacho kinaonesha kwamba wimbo wa mtu fulani umepigwa mara ngapi, gharama yake ni kiasi gani na anatakiwa alipwe nini? Kwa hiyo, tunaomba sana kama COSOTA itahamia kwako tunaamini kabisa utaweza kusimamamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna suala la mikataba la uuzwaji wa kazi za wasanii. Nadhani kwenye mashirikisho haya uweke wanasheria watakaosimamia kazi hizi na mikataba ya wasanii. Wasanii wengi anapewa shilingi milioni 10 anaenda anagawana na wenzake inatoka lakini anaendelea kutajirika yule msambazaji. Simamia haya mashirikisho yatakusaidia kusaidia wasanii hawa waweze kupata kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kuna mmoja amesema kazi za nje. Hebu pigeni kazi za ndani lakini bado na zile zinazouzwa mitaani, sisi tunalipa sticker, tunalipa TRA lakini kuna kazi hazina sticker, zinaharibu soko la wasanii hapa nchini. Tunaomba jamani mipaka, akitaka kuuza basi waende TRA na wao wakalipe zile sticker na utoaji wa sticker uende mpaka mikoani. TRA wapunguze ule mlolongo, waende mikoani ili wasanii wote waweze kupata huduma kule walipo. Hakuna haja ya mtu kutoka Mtwara, Kigoma au Bukoba, aende Dar es salaam kwa ajili ya ku-register kazi yake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninaamini kabisa suala hili utalisimamia barabara.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala jingine nakuomba ujenge Kituo cha Sanaa. Kituo kikubwa ambacho wasanii wote watapatikana pale, watafanya kazi pale, hata kama mtu anataka kufanya nendeni kwenye nchi za wengine mkaone ni namna gani ili hata kama watu wanataka kwenda kumuona msanii fulani, wanajua tukienda kwenye kituo fulani leo kuna maonesho haya, kesho kuna maonesho haya. Lakini na wale wanaotaka kufanya filamu zao kunakuwa na eneo kubwa ambalo linakuwa limetengwa, ardhi tunayo, lakini siyo vibaya hata tukajenga kukawa na kijiji cha wasanii kule, maana sasa hivi ukweli ni kwamba wasanii bado ni maskini sana, tunalo Shirika letu la National Housing, tupeni ardhi, tujenge, dhamana ni kazi zetu, tutalipa! Ili wasanii wapate maeneo mazuri ya kuishi, tupeni ardhi. Mimi ninakutakia kheri, ninaamini na ninakuamini, naunga mkono hoja. Ahsante.