Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja mbili zilizotolewa kwa siku ya leo.

Kwanza kabisa nipongeze Kamati mbili zilizowasilisha taarifa yao hapa siku ya leo, lakini kazi kubwa ya Bunge ni pamoja na kutunga sheria, lakini Katiba yetu imekasimisha madaraka, imelipa uwezo Bunge hili kukasimisha madaraka

katika mamlaka nyingine za Kiserikali. Lakini kwa bahati mbaya sana mamlaka zetu zilizopewa jukumu hili la kutunga sheria ndogo katika maeneo yao zimekuwa zikitunga sheria ambazo hazina uhalisia kulingana na maisha halisi ya Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hayo na nitaendelea kuelezea haya kwa kutumia mifano michache. Mfano Sheria ya Ushuru wa Nyumba za Kulala Wageni katika Manispaa ya Temeke; sheria hii iliyotungwa pale inaweka katazo kwa wageni kulala katika chumba kimoja na kulalia kitanda kimoja, wageni hawa ambao ni wa jinsia moja, lakini sheria hii haikuzingatia watu wenye mahitaji maalum, sheria hii haikuzingatia kwamba kuna ulazima, kuna mazingira ambayo yanamlazimisha mtu kulala katika kitanda kimoja watu wa jinsia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, mama amekuwa akisafiri na mwanaye, hakuna namna unamzuia mama yule kulala na mtoto wake, lakini pia kuna mgonjwa anayehitaji msaada kutoka kwa msaidizi wake, huwezi kumzuia kulala katika kitanda kimoja au chumba kimoja na huyo msaidizi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwneyekiti, hivyo sheria hii katika utekelezaji wake inaleta ukakasi kwa sababu unapoenda kutekeleza sheria ya namna hii wapo wananchi watakaoumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaelewa maisha ya Mtanzania halisi yalivyo, wakati mwingine inawalazimu watu wa jinsia moja kama ni mama na mtoto wake kulala chumba kimoja ili kuokoa gharama, lakini ukisimamia sheria hii maana yake yule mtu ataingia gharama zisizokuwa na msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kupitia uchambuzi wa Kamati yetu pia tumegundua Sheria ya Afya ya Usafi wa Mazingira katika Halmashauri ya Nsimbo; sheria hii imeweka katazo kwa mtu yeyote kuuza vyakula kwa kubeba kwenye ndoo, kwenye sufuria hata kama imefunikwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelewa maisha ya Watanzania wetu, lakini hebu fikiri maisha ya Mtanzania ambaye ni mama ntilie, unamwambia usihifadhi chakula kwenye sufuria, hata kama umefunika, asihifadhi chakula kwenye ndoo hata kama imefunikwa. Unampa maisha gani huyu Mtanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sheria hii ukienda kwenye utekelezaji wake huwa ni mgumu sana. Ni mgumu kwa sababu mlaji wa hii sheria unaenda kumpa adhabu zisizokuwa na msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika Halmashauri ya Msalala kuna sheria ya Ukusanyaji na Kuzoa Taka; sheria hii inaweka katazo kwa mwananchi ambaye atatupa taka hovyo ambacho ni kitu kizuri, lakini sheria hiyo imetamka kwamba mwananchi au kaya lazima iwe na chombo cha kuhifadhia taka chenye mfuniko, lakini sheria haijatamka kwamba chombo hicho ni chombo cha aina gani? Na ni mfuniko wa aina gani, lakini sheria haielekezi baada ya kukusanya zile taka, akishamaliza kukusanya anapeleka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa mazingira halisi ya kijijini tunaelewa kwa watu tuliotoka kijijini, kaya zote za vijijini wanachimba mashimo ya taka, ili kuhifadhi takataka. (Makofi)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Iddi Kassim?

T A A R I F A

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa Taarifa mchangiaji kwamba sheria hizi, mamlaka haya ambayo tumeyakasimu kwenye Halmashauri zetu, utaratibu wa kutunga sheria hizi haufuatwi, hasa kuwashirikisha wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Halmashauri ya Msalala ni Halmashauri iliyo katika maeneo ya vijijini na hivyo ninashauri sheria hii ifanyiwe marekebisho kwani haitatekelezeka kwenye maeneo hayo, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Regina unapokea Taarifa?

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo Taarifa kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii kwa uhalisia wake unaona ni kwa namna gani kwanza wananchi wanaenda kunyanyasika. Halmashauri ya Msalala haina gari la kubebea taka, wakati huo umetunga sheria kwamba kila kaya wahakikishe wana chombo cha kuwekea taka. Sasa baada ya kuweka hizo taka watazibeba kwenda wapi? Dampo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiitizama kwa undani hii sheria, mamlaka hizi zinazotunga sheria zinatunga sheria ambazo hazina uhalisia kulingana na wakazi wa eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sheria nyingine ni Sheria ya Ada na Ushuru katika Halmashauri ya Mvomero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inaeleza kwamba ada ya kibali cha upimaji wa afya, maana yake kila mtu anayehitaji kibali cha kunyunyiza viuatilifu atapata kibali kwa gharama ya shilingi milioni moja. Kama kibali tu anaenda kupata kwa shilingi milioni moja, anapotaka kutoa huduma kwa wananchi atatoa kwa gharama gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Halmashauri lazima ipange gharama ambazo hata yule ambaye amepata kibali tayari anapotaka kutoa huduma kwa wananchi atoe gharama ambazo hazitamuumiza mwananchi huyo. Katika uchambuzi wetu wa Kamati kulingana na huu udhaifu uliojitokeza katika mamlaka waliyopewa, jukumu la kutunga sheria ndogo bado kuna haja ya Bunge sasa kufikiria upya namna ya kuendelea kusimamia hizi mamlaka ili wasije wakatutungia sheria ambayo inaumiza wananchi wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema haya kwa sababu sheria hizi mpaka kufika kwetu kwa Wabunge tayari kule imeshaanza kutumika, jambo ambalo wananchi wameshaanza kuumizwa na hizo sheria na mpaka hatua ya kukataza au kuondoa ile sheria ije iwafikie wananchi, tayari wananchi wengi wameshapata madhara makubwa.

Kwa hiyo, ombi langu ni kwamba Bunge hili tuna jukumu kubwa bado la kuendelea kusimamia hizi mamlaka tuliowapa jukumu la kutunga hizi sheria, ili wananchi wetu wasiendelee kupata madhara makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikifika hapa niseme naunga mkono hoja, lakini nikushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)