Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami kupata ridhaa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ambayo kimsingi inagusa Maisha ya wananchi wa chini, wananchi maskini kabisa wa maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba pamoja na yote hayo mahitaji ya mwananchi maskini, yule mwananchi wa chini kabisa mahitaji yake makubwa huwa ni barabara nzuri ya kumfanya atoke eneo moja kwenda eneo lingine, inamfanya awe na uhakika wa afya, Wizara hii inapoweka zahanati na kuweka kituo cha afya inamsaidia kumtengenezea yule mwananchi maskini mazingira mazuri ya kufika eneo husika, haya yote yanafanywa na Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inapojenga madarasa, inaboresha miundombinu ya elimu inamsaidia mwananchi maskini kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa muktadha huo, ndiyo maana nimesema leo nimepata bahati ya kuwasemea wananchi wanyonge kabisa ambao kimsingi kwa muktadha huo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuliona hilo akaamua kwa upendo mkubwa kupeleka fedha kwenye Wizara hii ili kufanya kazi kubwa kwa wananchi hawa maskini. Mheshimiwa Rais kipekee kabisa nimshukuru sana kwenye Jimbo langu la Rorya nilipokuja mwaka jana kuzungumza kuhusiana na daraja la Mto Mori ambalo linaunganisha Tarafa Tatu, nilizungumza kwa kuamini kwamba wale wananchi maskini wanaotakiwa kufanya shughuli za kibiashara kutoka eneo moja la Tarafa moja kwenda Tarafa nyingine kati ya Tarafa Nne, Tarafa Tatu zinakwenda kunufaika na daraja hili. Mheshimiwa Rais hakusita alinipa zaidi ya 1.5 billion, hivi ninavyozungumza daraja lile linajengwa eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kutambua mchango mkubwa na mchango mkubwa kwa wananchi maskini ameleta fedha kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa madarasa nchi nzima ambao tunaziita UVIKO mimi sitamani tuziite UVIKO, Mimi kwangu nilipata zaidi ya Shilingi Bilioni 2.3, ni kwa sababu alitambua wananchi maskini wakati wanapofika kipindi cha kwenda mashuleni wanachangishwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa yale ili watoto wao waende kusoma, akaamua kumsaidia yule mwananchi wa chini kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraza hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais hakuishia hapo kwenye maeneo mengi kwa kutambua mchango mkubwa wa afya mwananchi maskini Mzee wa kawaida anapougua anahitaji apate huduma ya kwanza ni kupata dawa, akaona ili aweze kumboreshea mazingira hayo akaleta fedha kwenye Majimbo yote ya vituo vya afya pamoja na zahanati. Kwangu peke yake kwa mwaka mmoja wa Mheshimiwa Rais amenipa zaidi ya Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nashawishika kusema kabisa hadharani kwamba Mheshimiwa Rais ameamua kushughulika na wananchi wa chini kabisa, hii ndiyo dhama na dhamira njema ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nirudi kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kutambua pamoja na kutuwakilisha vijana kwenye mchango na namna mnavyofanya kazi, sisi kama vijana hatuna budi kuwapongezeni na kuwashukuru kwa sababu kama kweli msingetimiza haya maana yake mlikuwa mnapoteza uaminifu mkubwa sana kwetu vijana, endeleeni kuchapa kazi kwa mchango huo mkiamini haya yote Mwenyezi Mungu atawajaalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo ninao ushauri wa aina mbili kwa Wizara hii, jambo la kwanza ni commitment yako kwenye Halmashauri, commitment hii uielekeze kwenye usimamizi wa fedha za miradi na hauwezi kuelekeza kwenye usimamizi wa fedha za miradi kama Waheshimiwa Madiwani hawako stable, kama Waheshimiwa Madiwani hawapati posho yao ya kueleweka ningetamani niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliozungumza jana, badala ya kulipwa posho ya Shilingi 350,000 tuone namna gani Waheshimiwa Madiwani wenzetu wanalipwa mishahara badala ya kulipwa posho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni Mheshimiwa Waziri uimarishe sana usimamizi wa kufanyika vikao vya Madiwani. Mathalani kwangu vikao vya sasa vinavyofanyika leo ninapozungumza kinafanyika kikao cha Baraza la Madiwani kujadili robo ya pili ya mwaka wa bajeti, yaani toka mwezi wa Kumi Kikao cha Baraza la Madiwani hakijawahi kukaa kinakaa leo mwezi wa Nne. Sasa tazama hapo fedha zako za miradi nani anayesimamia, ni nani anaehoji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya fedha iliyotakiwa ikae mwezi wa Februari, mwezi wa Januari, mwezi wa Disemba haijakaa inakaa mwezi wa Aprili kujadili mapato na matumizi ya fedha zilizokwenda hizi tunazungumza za Mama Samia za mwezi wa Desemba, Januari na Februari, ni nani anapeleka usimamizi ulio imara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ninakuomba ninajua na ninawaamini imarisheni commitment, wekeni commitment hasa kwa Wakurugenzi, vikao vya Madiwani vifanyike kwa wakati kwa sababu bila vikao vya Madiwani kufanyika kwa wakati maana yake hizi fedha zinazokwenda hazitapa usimamizi imara. Mheshimiwa Rais atakuwa anapeleka fedha, miradi inachelewa kuanza, na hakuna chochote kinachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwenye hili umetuletea fedha kwa ajili ya vituo vya afya na ninashukuru sana Mheshimiwa Rais ametuletea Milioni 500 kwenye Tarafa ambayo haikuwa na kituo cha afya. Watalaam wanakwenda wananchi wameshaamua wapi wanajenga kituo cha afya kwenye Kata husika, wanawaambiwa hairuhusiwi kujenga hapa tumepata mwongozo kutoka Wizarani. Wanazalisha mgogoro mwingine toka mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu, wa nne tunabaki kujadili wapi kiende kujengwa kituo cha afya ile fedha ya Mama Samia maana yake imekuja ndiyo maana tunasema fedha zinakuja za miradi lakini utekelezaji wake unachelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri commitment kwenye maeneo haya uweze kuweza kusimamiwa vizuri ili Wakurugenzi wasikuangushe mwisho wa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili la ushauri kwenye fedha ya miradi ya kimkakati. Mheshimiwa Waziri ni lazima fedha za miradi ya mkakati ziende kwenye Halmashauri ambazo hazina mapato stable, mapato yake hayapo stable mathalani kwangu Rorya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili niweze kuendesha Halmashauri mapato yangu yanategemea aina tatu, moja ni uvuvi, mbili ni kilimo, tatu ni ufugaji. Sasa ninyi Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri wewe unafahamu kwa miaka mitatu hii mfululizo mpaka leo namna ya uvuvi wa nchi hii ulivyoathirika, kuna watu wamefilisika, kuna watu wamekimbia kwenye sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Halmashauri fedha inayokusanywa kwenye uvuvi ni ya wale wavuvi wadogo ambao inasubiri wakavue irudi kupanga mipango mikakati ya maendeleo. Ukienda kwenye kilimo hatuna irrigation scheme yoyote inayofanyika ndani ya Wilaya ile, maana yake anasubiri mkulima mdogo alime mazao yake, akiwa anapeleka kwenye minada ikachukua ushuru ipange miradi ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye ufugaji, leo tunafanya ufugaji ambao ili mwananchi aweze kupeleka mfugo wake kwenye mnada Halmashauri iende ikachukue kodi ichukue fedha ipange miradi ya kimaendeleo. Hatuna mradi mkubwa zaidi ya hii miradi ya kimaendeleo ya ujenzi wa vituo vya afya ambao unazidi Bilioni Moja au Milioni 500 ambao unaweza ku-sustain ukuaji wa uchumi wa Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba kwenye fedha za miradi ya kimkakati, kwa kuwa tayari nimeona imepangwa bajeti peleka fedha kwenye hizi Halmashauri ambazo mapato yake ya Halmashauri hayapo-stable ambayo ukitazama kwa namna muda unavyokwenda itafika mahali hizi halmashauri zita collapse.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama uvuvi unakwenda na umeshuka kweli kweli lini Halmashauri baada ya miaka mitatu, minne, mitano huko mbeleni itaweza kujiendeshaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuleta ombi Mheshimiwa Waziri kutumia fursa ya kwetu sisi ya kimpaka kule Kirongwe. Wilaya yetu imepakana na nchi ya Kenya tukaleta hapa maombi na nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, kwa kulitambua akaamua kutupa fedha kwa ajili ya kujenga one border post - Kirongwe ili tutumie fursa ya kimpaka wa Kenya na Tanzania, lakini kujenga one border post bila kuwa na fedha za kimkakati za kujenga soko pale haitatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe kupitia fedha zako za kimkakati kupitia kuisaidia na kuinusuru ile Halmashauri utupe fedha ili tuweze kujenga soko la kisasa pale mpakani ili tuweze kunufaika na soko la Kenya na Tanzania kwa sababu tayari Wizara ya ardhi imekwishatupa fedha kwa ajili ya kujenga one border post, utakuwa umetusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utupe fedha ya mradi ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya Mika. Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri unapoingia daraja la Kirumi pale mpaka unakwenda Tarime ile yote ni Rorya lakini wewe ni shahidi hakuna stendi yoyote ambayo magari yanaingia kwa ajili ya kulipa ushuru na hakuna stendi yoyote ambayo wananchi wanafaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe kwenye eneo lile kwenye fedha za miradi ya kimkakati nipe fedha angalau tuweze kuweka stendi na soko pale ili tuweze kusaidia vyanzo hivi ambavyo havipo imara vya Halmashauri vya kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo maeneo mengine mengi tu, tuna eneo la Nyanchabakenye pale ukitupa fedha kwenye ujenzi wa stendi bado ninaweza nika- sustain na kuendesha maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie kuhusiana na maeneo ya miradi hii. Tunayo maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri yanaunganisha kati ya Kata na Kata, naomba tupate fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Nyathorogo ambalo linatuunganisha kati ya Kata ya Nyathorogo na Kata ya Tarime vijijini kwa sababu bila kufanya hivyo wananchi wa eneo moja hawawezi kutoka eneo moja kwenda eneo la pili. Ninaomba nipate fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja linalouunganisha Kata mbili Kata ya Kitembe na Kata ya Roche ili angalau kuweza kuwasaidia wananchi wanaotoka eneo la Kata moja na Kata nyingine. Kwa kufanya hivyo kama nilivyotangulia kusema unakuwa umemsaidia na umemkomboa mwananchi maskini ambaye kimsingi anakuwa amelima mazao yake anataka atafute soko la upande wa pili lakini hana namna ya kufika eneo la upande wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu tumeziweka kwenye fedha za miradi ya kimaendeleo utusaidie sana, lakini pale utakapoweza Mheshimiwa Waziri tusaidie pia kutokana na jiografia ya Jimbo la Rorya niliwahi kusema hapa, vituo vya afya vya maeneo ya mpakani mwa Kenya tunazo Kata zaidi ya tatu zinapakana na Kenya hazina kituo cha afya ambacho ni imara. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri angalia Kata ya Roche, Kata ya Goribe na Kata ya Bukura kama wanaweza sehemu mojawapo kupata kituo kizuri cha afya, Kata hizi zote tatu zinapakana na nchi ya Kenya lakini wananchi wa mpakani hawa hawana namna ya kupata kituo cha afya maeneo yale, hawana huduma hiyo. Kwa hiyo nikuombe maeneo haya kupitia zile Kata za kimkakati tupate kituo maeneo yale ili kuboresha na kudumisha maeneo yale ya kiuchumi ili angalau wale wananchi wanapopata shida kwenye sekta ya afya waweze kupata mahali pengine pa kuweza kupata matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe la mwisho, kupata fedha za miradi ya dharura zipo barabara ambazo nimeziwakilisha kwa Mkurugenzi wa TARURA. Tuna barabara moja ya kutoka Shirati kwenda Minigo hii barabara hivi tunavyozungumza haipitiki kutokana na mvua zilivyonyesha. Tuna barabara moja ya kwenda Kuruya kwenda Marasibora, Randa kwenda Masike, Masangura kwenda Koryo, Nyamusi kwenda Panyakoo pamoja na Shirati. Barabara hizi ninavyozungumza Mheshimiwa Waziri hazipitiki na kwa sababu tumekwishaleta maombi ya fedha ya dharura ili angalau kwa kipindi hiki mvua inavyonyesha wananchi wetu waweze kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri niweze kupata fedha kwa ajili ya uboreshaji huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya machache nakushukuru sana naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)