Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali kusimama katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza Wizara, nimpongeze Waziri wa TAMISEMI, Naibu Mawaziri wake, Katibu Mkuu, Mtendaji wa TARURA na Viongozi ambao wako chini ya Wizara ya TAMISEMI. Wizara ya TAMISEMI ndiyo inayotafsiri maisha ya Watanzania ya kila siku. Wizara hii ni kubwa sana ina majukumu mengi na ndiyo maana iko chini ya Ofisi ya Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia fursa hii kumpongeza Rais wetu kipenzi, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Tumeona mambo mengi ameyafanya na aliahidi kuendeleza miradi. Miradi inatekelezwa na miradi mingine tunaiona ameanzisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuwa ni mbunifu wa mambo mengine tofauti, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutoa vipaji tofauti tofauti kwa watu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache ambayo nitayaongelea, kwanza kuhusu Kanuni zinazotoa asilimia 10 ya mikopo katika Halmashauri zetu. Kanuni zinazotumika kwa sasa hazimnufaishi sana mwananchi kwa sababu zimejikita katika Halmashauri husika. Mtu anapoomba mkopo yeye anaruhusiwa kufanya biashara kwenye Halmashauri hiyo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Dar es Salaam, watu wa Dar es Salaam hatuna mashamba tunategemea biashara na biashara kwa asilimia kubwa pale ni watu wanaoshughulika na biashara ndogo ndogo. Karibu asilimia 80 ya wana Dar es Salaam wana shughulika na biashara ndogo ndogo, lakini wana nia ya kufanya biashara katika kilimo, wanapotaka kuomba fedha kwa ajili ya kwenda kulima hawapewi kwa sababu Kanuni zinakataa. Kwa sababu, yeye anakopa Manispaa labda mfano Ilala au Ubungo lakini shamba lake liko Bagamoyo Kanuni zinamkataa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa Serikali ni hiyo moja, Wizara ni moja, Halmashauri ya Bagamoyo, Halmashauri ya Ilala iko chini ya TAMISEMI. Sasa Kanuni hizi ni kikwazo sana kwa watu wetu kuweza kunufaika na mikopo na ndiyo maana hii mikopo marejesho yanakuwa hafifu kwa sababu watu wamekariri kufanya biashara ambazo hazina tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta achukue mtaji aende kununua samaki ferry, biashara ya kuuza soksi, biashara ya kuuza handkerchief haziwezi kumtoa mtu, haziwezi kusaidia. Tutawafukuza tutawanyang’anya ndizi kila siku tusipobadilika na tusipobadilisha kanuni zetu, katika kutoa mikopo tutakuwa tunaimba wimbo usiokuwa na mwisho. Ninaiomba Wizara izingatie haya ibadilishe hizi Kanuni zetu
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee upungufu wa watumishi katika Halmashauri zetu na nitaongelea watumishi wale wenye fani ambazo zinachochea kipato au fani ambazo zitasaidia Halmashauri kupata kipato zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna fani ya Wahandisi, Wasanifu Majenzi, Wakadiriaji Majenzi, Mabwana Afya, Mabibi Afya, Wachumi na Wakaguzi wa Fedha. Fani hizi zikitumika vizuri zitasaidia kuleta mapato katika Halmashauri zetu, lakini ni wachache, hawapo ni wachache sana. Halmashauri ni kubwa huduma ni nyingi shughuli ni nyingi miradi ni mingi lakini watenda kazi ni wachache. Utakuta ndiyo maana majengo yanaanguka watu wanajenga kwa kukosa vibali kwa sababu watumishi ni wachache, mapato yanakosekana kwa sababu watu wanajenga, hawana usimamizi na ubora wa majengo nao unakuwa hafifu. Naiomba Serikali izingatie hayo katika masuala ya ajira katika kada hizi ambazo nimezisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali imesema kwamba inaongeza ajira kwa walimu, madaktari, wauguzi lakini fani hizi kwa kweli tunaomba vijana wetu wachukuliwe. Wengi wamemaliza Vyuo Vikuu wapo, Waziri mhusika tunaomba mzingatie haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu kuwapanga wamachinga, naipongeza Serikali na Mheshimiwa Waziri juzi umechukua hatua za haraka tunakupongeza sana. Wewe ni mnyenyekevu katika level yako, lakini watu wenu kule kwenye Halmashauri na wale Mgambo na wasimamizi hawana utu. Ni lazima tuseme tunapata lawama sana, simu ni nyingi sana, lakini wewe tunakutambua wewe ni mnyenyekevu ni msikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini watu wa chini yako sio wanyenyekevu kwa wananchi? Waende kusikiliza wananchi hawa ndiyo waliotuweka madarakani, ni lazima twende tukasikilize shida zao na tuzitatue kwa kutumia utu na kuwaheshimu. Ninaomba sana mzingatie hayo kwa sababu tunapata vikwazo sana na tunajua mengi. Wabunge wanajua mambo mengi sana. Kwa hiyo, wewe unatusikiliza, Wabunge wanasikiliza watu wao lakini watekelezaji wa kule chini baadhi yao wanatukwamisha. Kumsaidia Mheshimiwa Rais ni kuwa mnyenyekevu kwa wananchi kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza baadhi ya Mikoa wananyenyekea sana wananchi lakini wengine wanatukwamisha ni lazima tuseme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilishuhudia mwananchi anabomolewa kibanda mvua inanyesha, ana Watoto, Mgambo sijui wamelogwa na nani mgambo wa Jiji, hawatekelezi kwa utu wanatuangusha sana. Naomba Serikali izingatie hayo, iwahudumie wananchi kwa kuzingatia utu wa mwanadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu ni wasikivu hawana taabu watatii, lakini pia biashara ndogondogo kama magenge kule waruhusiwe kufanya kazi kwa kuzingatia usafi, kwa kuzingatia kupangwa, kwa sababu mtu hawezi kutoka kitongojini akaenda Buguruni kununua nyanya ya Shilingi Mbili. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa ahsante sana.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru lakini tusiwasahau Madiwani wetu wanafanya kazi nzuri sana. Posho zao na maslahi yao yaboreshwe. Nakushukuru. (Makofi)