Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi, lakini kipekee nichukue nafasi hii nimshukuru sana Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ndugu yangu Mheshimiwa Innocent pamoja na Naibu Mawaziri wote, lakini niungane na wenzangu waliotangulia kuwashukuru sana TARURA kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Wote ni mashahidi tangu TARURA imeanzishwa kuna mabadiliko makubwa sana kule vijijini kwenye barabara zetu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. Sisi wananchi wa Jimbo la Manyoni Mashariki tunajivunia sana uwepo wake. Ndani ya mwaka mmoja tumepata fedha nyingi sana upande wa fedha za UVIKO, upande wa fedha za afya, lakini maeneo mbalimbali tumepata fedha nyingi sana. Kwa hiyo, tunamshukuru sana na tunaomba mtufikishie salamu hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina hoja kubwa mbili. Hoja ya kwanza naomba nichangie kuhusu mfumo wa miradi ya kimkakati, nitatolea mfano kuhusu ujenzi wa stendi katika Halmashauri zetu,
lakini hoja ya pili ni kuhusu mfumo wa upandishaji hadhi Mamlaka ya Miji Midogo na nitatolea mfano wa Mamlaka ya Mji Mdogo Manyoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyote ni mashahidi kwamba, Halmashauri nyingi hazina stendi za kisasa za mabasi. Mfano mdogo ni Halmashauri yangu ya Manyoni, lakini Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Fedha wana mfumo unaitwa miradi ya kimkakati kwa ajili ya Halmashauri kuomba fedha kwa ajili ya hiyo miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mfumo una mapungufu mengi sana. Mojawapo ya pungufu la huu mfumo kwanza kuna Halmashauri nyingi ambazo hazina uwezo wa kujisimamia zenyewe ziandike yale maandiko, hazina uwezo wa kujisimamia zenyewe zifanye zile stadi kwa mfano environmental impact assessment, feasibility design, detail design, na kadhalika. Ili Halmashauri iweze kupata zile fedha lazima wakidhi vigezo nane na mojawapo ya kigezo ni kama hayo niliyoongea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi Halmashauri zetu hazina man power ya kutosha ya kuandika yale maandiko. Kwa Halmashauri zenye fedha zinahitaji zaidi ya milioni 300 ili kum-hire consultant ambaye atakuja kuandika hayo maandiko. Hili ni tatizo kubwa sana limesababisha Halmashauri nyingi mpaka sasa hivi zimeshindwa kutekeleza miradi ya kimkakati hususan stendi, ikiwepo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwanza namshauri Waziri naomba pitia upya huu mfumo wa miradi ya kimkakati ili uzingatie Halmashauri ambazo zina mapato ya chini Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mlishikilie hili. Pili, tuna taasisi zetu ambazo zina deal na masuala ya ujenzi, NSSF, PSSF, NHC kwanini tusiingienao ubia tukawapa wakajenga wakatuachia tukatumia tukawa tunarudishia kidogo kidogo? Lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na stendi ambazo zitakuwa chanzo cha mapato vilevile tuta-beautify Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la mfumo wa upandishaji hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo. Katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki nina Mamlaka ya Mji Mdogo ambayo iliundwa 2014. Mpaka sasa hivi nina miaka nane tangu Mamlaka ya Mji Mdogo Manyoni imeundwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukishaunda mamlaka ya Mji Mdogo unasimiwa na mtu anaitwa TownShip Executive Officer (TEO), lakini una-dissolve wale watendaji wa vijiji. Mpaka sasa hivi katika vitongoji 30 vinasimamiwa na Wenyeviti wa Vitongoji kwa zaidi ya miaka nane. Hili ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba, kwanza naungana na Wabunge wenzangu, Madiwani wetu wanafanya kazi kubwa sana, Wenyeviti wetu wanafanya kazi kubwa sana, lakini hawa kwa mfano kwenye Mamlaka ya Miji 30 hawana Watendaji wa Vijiji wenyewe wame-substitute role za Watendaji wa Vijiji. Hawa wanalipwa 40,000 kwa mwezi, lakini kwa sababu mapato yanasumbua wakati fulani wanakaa miezi Minne hadi Mitano hawajawahi kulipwa, hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kitu hapa, kwanza; niishauri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kama mnaona hii Mamlaka ya Miji Midogo mliyoianzisha haina tija ni vizuri mkaifanyia tathmini badala ya kukaa nayo miaka 10 hamjaipandisha hadhi. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri unda timu ifanye tathmini ya hii mamlaka ya Miji Midogo mliyoianzisha whether tunahitaji kuendelea nayo au hatuhitaji kuendelea nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili. Kwa Halmashauri yetu ya Manyoni, kwenye Mji Mdogo wa Manyoni nimesema kwamba, ndani ya miaka nane tumekuwa tukiwatumia Wenyeviti wa Vitongoji kutekeleza miradi mikubwa ambayo Mama Samia anatuletea. Hili ni tatizo kubwa…
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Mlaghila. Umesimama kwa Kanuni gani?
T A A R I F A
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 77(1).
MWENYEKITI: Endelea.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, huko kwenye Miji Midogo Madiwani wetu hata siyo tena Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo kwa hiyo, wako pale kama vivuli. Ahsante.
MWENYEKITI: Ukitoa taarifa lazima Kiti kijiridhishe kwamba hii ni taarifa. Kwa hiyo, ni vizuri Waheshimiwa Wabunge tunapotoa taarifa tuipime sana. Mheshimiwa Spika ameshatoa mwongozo kuhusu aina ya taarifa hapa Bungeni.
Mheshimiwa endelea.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na ninaomba unilindie muda wangu. Nilichokuwa nikisema ni kwamba, naungana mkono na Waheshimiwa Wabunge ambao wamependekeza posho za Madiwani zibadilike ziwe mishahara lakini kwa upande wangu mimi naongezea suala la Wenyeviti wangu wa vitongoji vya Manyoni, Mamlaka ya Mji Mdogo wa Manyoni na Wenyeviti wa Vijiji vyote. Kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Manyoni ndani ya miaka nane hawa wame-substitute role ya Watendaji wa Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna Watendaji wa Vijiji zaidi ya 30 katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Manyoni, hili ni tatizo kubwa. Kwa hiyo, ningeshauri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa muangalie kama bado nafasi ya kupandisha hadhi mamlaka ya Mjhi Mdogo kuwa Halmashauri ya Mji ni vizuri sasa tukaongeza posho za hawa Wenyeviti wa vitongoji katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Manyoni. Hili tunaweza tukalifanya kwa nchi nzima, lengo letu ni kuhakikisha kwamba, tunawapa morali kusimamia miradi mbalimbali ambayo fedha tunapewa na Mama Samia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya mimi naomba nirudie kusema namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya na wananchi wa Jimbo la Manyoni tunampongeza sana, tunamuunga mkono na ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)