Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Namshukuru Mwenyezi Mungu pia kunipa nafasi ya kusimama. Naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa usimamizi mzuri wa Serikali yake yote mpaka tunaona jinsi ambavyo Wizara hii inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Deo kwa kazi nzuri sana wakishirikiana na watendaji wote wa Wizara husika katika kufanikisha malengo ya kuboresha utumishi huu wa umma.
Mheshimiwa Spika, jukumu kubwa ambalo ofisi hii inalo ni kuhakikisha kwamba Utumishi wa Umma unaendelea kuzingatia suala zima la misingi ya utawala bora. Misingi ya utawala bora ni kufanya kazi kuzingatia sheria, sera na taratibu mbalimbali walizojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sitatofautiana na wenzangu wengi walionitangulia; Serikali Awamu ya Sita katika mwaka huu tunaomaliza imeonyesha dhamira ya dhati kabisa ya kuboresha maslahi ya Watanzania ambao ni Watumishi wa Umma. Naepuka kurudia vyote walivyosema wenzangu kwa habari ya mishahara, upandishaji madaraja kufuta kodi ya Bodi ya Elimu ya Juu kwenye mishahara yetu, kupunguza kodi ya mshahara mpaka 8%, na mambo kadha wa kadha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala zima la upandishaji wa madaraja, wamevunja rekodi kwa maana ya mambo yote ambayo ameahidi Mheshimiwa Rais kwenye mwaka uliopita kupitia bajeti yake, kwa asilimia kubwa sana yametekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo yote mazuri yaliyotekelezeka, tunaendelea kutambua hali tete ya uchumi duniani unavyokwenda pamoja na adha mbalimbali za kivita. Pia tunatambua anguko la kiuchumi katika sehemu mbalimbali duniani, lakini pamoja na yote hayo, watumishi wa nchi yetu bado wanaendelea kuomba suala zima la upandishwaji wa mshahara kulingana na pato letu, basi liendelee kuzingatiwa pale itakapowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mishahara hii tunashauri itakapopandishwa pale itakapowezekana, basi iwe kama zamani, izingatie suala zima la living wage, yaani mtu mshahara wake umsaidie kupanga mwezi mzima kula tarehe moja mpaka tarehe 30. Kwa nini? Sasa hivi mtumishi wa kawaida anapata mshahara mpaka tarehe 10, 15 umekwisha. Hii inapelekea kumpa msongo wa mawazo na inasababisha magonjwa mbalimbali hasa yasiyoambukiza ambayo pia ni mtihani mkubwa kuyagharamia. Hata hivyo naipongeza Serikali kwa kujiandaa kuja na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika utawala bora ni kusimamia suala zima la sheria, sera na taratibu walizojiwekea waajiri na watumishi. Hii pia inajielekeza katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba Serikali na Chama cha Mapinduzi inatumbua umuhimu wa vyama vya wafanyakazi ili kuleta mahojiano kati ya waajiri pamoja na waajiriwa kuboresha utumishi mahala pa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo basi, tunashauri Wizara hii iendelee kusimamia kwa ukaribu utawala bora katika sehemu mbalimbali kati ya waajiri ili wafanyakazi wawe na uhuru wa kujiunga na vyama vyao bila vizuizi. Pia maslahi yao mbalimbali yaweze kuzingatiwa na kusimamiwa kupitia vyama vyao, kwani mtu mmoja mmoja sio rahisi kuhudumiwa. Kwa hiyo, naomba Wizara izingatie kwamba mahali pa kazi pote, watumishi wawe na uhuru wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi na Mabaraza yawe huru ili wafanyakazi waweze kufumuka na kueleza changamoto zao.
Mheshimiwa Spika, hakuna sheria inamruhusu mfanyakazi mmoja atoke na kuleta changamoto yake. Hii inapelekea migomo ambayo siyo halali. Kwa sababu vyama vya wafanyakazi ndiyo pekee vinaruhusiwa kuendesha mgomo. Sasa kama wafanyakazi hawapati nafasi ya kueleza mambo yao kwenye Vyama vya Wafanyakazi wataeleza wapi? Vyama vya Wafanyakazi vikipata tatizo vinapeleka kwenye Tume ya Usuluhishi na ikishindikana, kwenye Mahakama Kuu, kwenye Kitengo cha Kazi. Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi inaweza kusema sasa nendeni kwenye mgomo.
Mheshimiwa Spika, natoa mfano wa madereva Tanzania. Madereva wana changamoto zao mbalimbali. Hivi ninavyozungumza na wewe kuna hatari ya mgomo, lakini ni kwa sababu waajiri wengi wamekuwa hawawapi uhuru wafanyakazi kujadili mambo yao kwa utaratibu. Hii inapelekea watu wachache kuanzisha migomo kinyume na utaratibu. Kwa hiyo, ofisi hii naishauri kupitia suala zima la utawala bora, basi isimamie masuala mazima ya wafanyakazi katika vyama vyao mahali pa kazi ili kuepusha misuguano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali, awamu iliyopita imetoa ajira za kutosha na sasa ziko ajira karibia 30,000. Kwa upande wa Idara ya Afya, mgawanyo wa ajira umekwisha. Mimi ninayo document, ajira zimeshagawiwa zote katika Wizara ya Afya, ila nina jambo moja nilisemee ambalo huwa nina interest nalo na nitakuwa sijawatendea haki nisiposema huku ndani.
Mheshimiwa Spika, nimezungumzia sana suala la Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili ya Milembe. Nimesemea sana hili suala mbali ya upungufu wa watumishi, vifaa na kadhalika. Tunaishukuru Serikali sasa imepanua hospitali katika suala zima la magonjwa mahututi pamoja na Emergence Department. Pamoja na upanuzi huo, lakini katika mgawanyo huu ile Hospitali ya Milembe haijapewa mtumishi hata mmoja. Ninashauri katika mgawanyo wa watumishi wa afya, hebu warudie tena, kwa sababu wako wanaojitolea katika hospitali hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii huduma ni nyeti, watu wengi wakienda kwenye ajira, ikifika wakati wa kusoma, wanaondoka, wanasoma kozi nyingine. Hawa-specialize kwenye suala zima la afya ya akili, lakini watu wanaojitolea wapo pale, sasa ajira zimetoka wameona pia Milembe haijawa located. Kwa hiyo, nawashauri kama wenzangu kwamba suala zima la ajira tuliangalie kutokana na umuhimu wa sehemu husika.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kabisa ni suala zima la ajira Wahadhiri wa Vyuo Vikuu. Nashauri kama inawezekana, Sekretarieti ya Ajira kama iwe kama zamani, iachie sasa vyuo viajiri especially watu ambao ni academic staff. Wanaweza wakaajiri technical staff lakini academic staff wawaachie kwa sababu TCU inashauri, angalau mtu mwenye GPA 3.5 aajiriwe, lakini Sekretarieti ya Ajira inasema
3.8. Kwa hiyo, unakuta Vyuo vya Umma vinakosa watu ambao wamewa-train wenyewe na wanawafahamu. Pamoja na kwamba wana GPA hiyo, lakini wanawafahamu kwamba uwezo wao ukoje. Angalau academic staff kama itawezekana Sekretarieti ya Ajira iwaachie basi vyuo waajiri wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia ikiwezekana, maprofesa wetu muda wao wa kustaafu uwe angalau miaka 60 ili wapewe mikataba baadaye ya kuendelea. Watu hawa ni watu wazima lakini wana experience kubwa na wameona mengi, siyo rahisi kukosea. Tunawahitaji kwenye vyuo katika uboreshaji wa kupata Watanzania ambao wana ujuzi wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema machache hayo...
SPIKA: Mheshimiwa Kaijage, naona Mheshimiwa Dkt. Paulina Nahato amesimama. Ni taarifa, utaratibu ama nini? Washa kisemeo.
T A A R I F A
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba academic staff ambao wanafundisha, umri wao wa kustaafu ni miaka 65 na sio 60. Ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kaijage, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, siipokei. Nilikuwa nilikuwa nashauri kama itawezekana, waweze kustaafu at age ya 60, halafu waanze kupewa mikataba kuanzia 60 kwenda juu mpaka watakapochoka wenyewe, kwa sababu ni watu muhimu sana na wana uzoefu na uelewa mkubwa. (Makofi)
SPIKA: Sasa Mheshimiwa Kaijage ngoja tuliweke vizuri. Kwanza walikuwa wanastaafu miaka 60, Serikali ikapandisha mpaka miaka 65. Sasa kwa mchango wako, unataka Serikali irejeshe 60 halafu iwaachie mpaka huko mbele au ianzie hiyo 65 isogeze mbele?
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ianzie 60 halafu waendelee mpaka watakapo choka wenyewe, kwa mikataba lakini ndio wazo langu.
SPIKA: Ni sawa. Nilitaka tu niliweke sawa ili uwe umemwelewa huyo aliyekuwa anatoa taarifa. Kwa hiyo, endelea na mchango wako.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. (Makofi)