Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngorongoro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Awali ya yote niwashukuru sana Wizara nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya, wakiwepo watendaji wote, TAKUKURU Pamoja na Katibu Mkuu, mwalimu wangu Dkt. Laurean Ndumbaro na wote ambao wanafanya kazi hizo kwenye Wizara. Pia nipende kusema kwamba Wizara hii wanafanya kazi nzuri sana, na kuanzia Awamu hii ya Sita. Mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Halmshauri nimeona kazi kubwa iliyofanywa watumishi kule wanaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha nyuma watumishi walikuwa wanafanya kazi ili mradi tu, watumishi walipopandishwa vyeo pamoja na kubadilishiwa madaraja naona sasa wanafanya kazi kwa morale. Kwa hiyo niiombe Wizara iendelee kufanya kazi hiyo. Nimeona kwamba mmepanga kuwapangisha watumishi wengine madaraja pamoja na kuwapandisha vyeo. Niombe kwamba tuendelee kutumia sheria zetu tulizonazo ili wasiwepo watumishi ambao wataachwa bila kupandishwa vyeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na pia niiombe Wizara, kwamba kuna watumishi wa kati tunafanya zoezi la kuwapandisha vyeo pamoja na madaraja, kuna watumishi ambao waliachwa niombe wizara mtoe nafasi tena kwa watumishi hao ili wapate nafasi kama watumishi wengine ndani ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwenye ajira ambazo zimetangazwa kuna maeneo ambako watumishi wamekuwa wakiondoka. Kwa mfano halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mwaka jana walipoajiriwa walimu waliajiriwa watumishi ambao ni walimu 10; walimu nane walikuwa wa shule za msingi na walimu wawili walikuwa ni shule za sekondari. Kwa bahati mbaya wale watumishi walishaajiriwa nyuma wakaacha ajira za Serikali. Kwa hiyo wakati wanaingizwa kwenye mfumo ilionekana kwamba wale watumishi hawawezi kuajiriwa tena. Kwa hiyo badala na halmashauri yetu kunufaika na watumishi 10 wale watumishi walirudishwa mpaka leo hawajulikani walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niiombe wizara kwenye ajira hizi tunaomba replacement ya zile nafasi 10 pamoja na watumishi wengine kwa sababu kwenye halmashauri yetu ya Ngorongoro watumishi wengi wanaondoka kwa sababu ya mazingira.
Mheshimiwa Spika, na ili kutatua tatizo hili nishauri Wizara, kwamba tuangalie maeneo ya pembezoni. Nakumbuka siku moja Mbunge Mheshimiwa Kandege alizungumza kwa maeneo ya Nkasi na Rukwa na maeneo mengine; kwa miaka ya nyuma Serikali kupitia mradi wa Mkapa Foundation kuna maeneo kama haya ambayo walikuwa wanapewa motisha walikuwa wanaajiriwa na Mkapa Foundation ili watu kufanya kazi kwa mkataba wa Serikali. Jwa hiyo maeneo kama halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na maeneo mengine ya pembezoni tuwape kipaumbele ili angalau maeneo yale wananchi nao wapate huduma.
Mheshimiwa Spika, Lakini kuna maeneo mengi sana mwaka 2017 Serikali iliwaondoa watumishi wa darasa la saba kwenye ajira. Wengine waliondolewa kwa haki na wengine waliondolewa kwa kuonewa. Nitoe mfano ya watumishi waliondolewa na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro; watumishi wenyeji 63 wengi wao waliajiriwa miaka 1993 na wengine waliajiriwa kabla ya mwaka 2004 lakini wote waliondolewa kwenye ajira na inaonekana hilo kulikuwa na chuki kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niombe Wizara ifanyie kazi malalamiko ya watumishi hao; na nimuombe Waziri, kwamba niwalete watumishi hao waje kuaonana na wewe pamoja na Katibu Mkuu ili mshughulikie matatizo yao, na wale wenye sifa warudishwe kazini.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna watumishi wengine wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro, nao waliachishwa kazi. Kulikuwa na mkataba ambao Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro pamoja na Baraza la Wafugaji waliingia mabkubaliano kwamba wale watumishi wa Baraza la Wafugaji walitakiwa kuajiriwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro; lakini baadaye waliomba kibali utumishi; kiuhalisia walikuwa na bajeti lakini baadaye wakasema utumishi wamenyimwa kibali. Kwa kuwa tayari Baraza la Wafugaji ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa na Sheria ya Bunge hapa hapa; kwahiyo mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri na watumishi hawa nao waangaliwe.
Mheshimiwa Spika, Serikali yoyote duniani ina kazi ya kuhakikisha kwamba huduma kwa wananchi zinatolewa. Na ili watumishi nao waweze kufanya kazi ni lazima wawe na maslai mazuri ili waweze kufanya kazi masaha yote yanayotakiwa. Kwa hiyo niendelee kuishauri Wizara, kwamba tuwaangalie watumishi, hasa kupokea malalamiko yao kwa wakati na kufanyia kazi kwa wakati. Unakuta kwamba kuna malalamiko yameletwa wizarani, mtu anasubiri miezi sita, sijui tunafanya nini mpaka miezi sita inapita bila kufanyiwa kazi? Tunatakiwa kwamba watumishi wanapoleta malalamiko yao yanatakiwa kufanyiwa kazi kwa specified time; siyo mtu anakuja Dodoma anatoka, Kikoma anatoka Arusha, kila wakati anakuja Dodma hapati majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeona kwamba mmeanda mfumo wa kupokea malalamiko, lakini wakati mwingine watumishi hawapati majibu yao kwa wakati. Niombe Wizara kufanyia malalamiko kazi kwa wakati wale wahusika wapate majibu yao kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono kwa asilimia 100.