Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kuchangia wizara hii ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Nitambue michango ya Wabunge wote ambao wamezungumzia kuhusu ajira na changamoto ambazo zinawakuba watumishi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wengi wamezungumzia kuhusu ajira, nami nitashauri kidogo. Pamoja na kwamba changamoto ni ya nchi nzima, lakini changamoto hizi zinatofautiana kulingana na mazingira. Nkasi peke yake ina mapungufu ya watumishi 1939, Nkasi peke yake. Sasa tunaomba hii keki ya Taifa inavyogawanywa waangalie na mazingira ambayo yameathirika zaidi, sisi kuwa pembezoni mwa nchi isiyo kama kila kitu kinachokuja tunaangaliwa mwishoni; ni vizuri tuangaalie hii keki kwa mgawanyo mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita zaidi kwenye Utawala Bora. Tunapozungumzia neno lenyewe Utawala Bora tunazungumzia utawala wa sheria, demokrasi, utu na haki za binadamu. Nikiwa nazungumza hapa mimi ni Mbunge pekee niliyetangazwa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tanzania Bara. Nisikitike kusema; nazungumza hapa tayari haya malalamiko ambayo nakwenda kuyazungumza nimeshazungumza na Waziri Mkuu na mimi ni Mbunge halali nilichaguliwa na kutangazwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza najua kwamba inapotokea DC kwenye eneo lake anamwakilisha Rais na Mkuu wa Mkoa anamwakilisha Rais kwenye eneo lake la mkoa. Leo ninapofanya mkutano kama Mbunge wa Tanzania na mwananchi wa Tanzania, DC anaamrisha watumishi wote waliopo Wilaya ya Nkasi wasitoe ushirikiano. Waziri Mkuu anajua; nashukuru alinipa nafasi ya kunisikiliza, lakini hakuna jambo lolote limefanyika mpaka leo. Tunapozungumza demokrasi, ili uende kwenye Utawala Bora lazima tujue na hapa kuna haja niwashauri vizuri, tusirudi kwenye mambo yaliyotokea Arusha au Hai. Lazima kuwepo na chombo maalum kitakachokuwa kinafuatilia mwenendo wa hawa Ma-DC wetu na Wakuu wa Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Watumishi wa Umma wanapata mishahara kutokana na kodi za Watanzania bila kuangalia vyama vyao. Leo unapomzuia mtendaji, Mkuu wa Idara kwenda kwenye mkutano wa Mbunge aliyechaguliwa; naamini Waziri Mkuu kama ingekuwa mimi ni Mbunge wa CCM angekuwa amechukua hatua mpaka leo. Nazungumza kwa uchungu mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inafikia mahali naambiwa kwamba, Diwani kwa sababu katika Kata 17 kwenye Jimbo langu nina Madiwani wanne wa CHADEMA, 13 ni CCM na kwenda kwenye mkutano kutoa fedha Mfuko wa Jimbo anaambiwa Diwani wa CCM asishiriki mkutano wangu na wale walioshiriki wamepewa adhabu ya kutoa boksi tatu za marumaru. Leo mimi nimekuwa chanzo cha kujenga ofisi za Chama cha Mapinduzi? Kwa nini natendewa hayo kama Mtanzania? Utawala Bora uko wapi? Jambo hili halifurahishi hata kidogo kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi ukiangalia Katiba yetu leo tunayoitumia, huyu anayeteuliwa kuwa DC kwa Mujibu wa Katiba anakwenda kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Hakuna chombo ambacho anakwenda kujifunza; anaweza kutumia kinywa chake kuondoa amani ya hilo eneo kwa sababu hajui mambo yanayohusu ulinzi na usalama. Kipindi cha nyuma walikuwa wanajitahidi wanawaandaa viongozi, leo wanachukua watu hawana sifa ya kuitwa Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama. Unapomwambia Mtumishi asiende kwenye Mkutano wangu na mimi ni Mbunge nikitumia nguvu ya umma nini kinatokea? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upendo wa Taifa langu, niliombe tena Bunge, niombe tena Waziri Mkuu…
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge Aida Khenani, kwamba masuala haya ni ya kisheria. Tuna Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao inaainisha kinagaubaga kwamba kuna sheria ambazo zimetungwa zinazotoa mamlaka ya uendeshaji wa shughuli za Serikali. uteuzi wa Wakuu wa Wilaya unatokana na takwa la Kikatiba, lakini pia majukumu yao yameainishwa kwenye sheria ya Regional Administrative Act. Kifungu cha 14 na katika Sheria hiyo inaelekeza sifa za Mkuu wa Wilaya, lakini pamoja na hayo kuna vetting wanafanyiwa kwa hiyo hawachaguliwi tu ili mradi, kwenye masuala ya usalama wanajua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, katika jambo ambalo amelizungumzia kuhusu allegation ya mambo ambayo ametendewa ya kiutawala katika wilaya yake; kama amekwisha kuwasilisha kwenye Mamlaka vivyo angesubiri sasa hatua ziweze kuchukuliwa kuliko kutuhumu tena mara mbili.
NAIBU SPIKA: Ahsante, dakika mbili zimekwisha. Je, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, namuheshimu sana kaka yangu na tulikuwa naye CHADEMA, afanye kazi anayoijua amepewa na kuaminiwa na aliyemteua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kama changamoto ni Katiba ndiyo maana tunasema tunahitaji Katiba mpya. Tusifikiri Katiba Mpya kuhusu uchaguzi tuangalie na aina ya watu kama hawa ambao nawazungumzia leo. Kama shida ni Sheria au ni Katiba kuna haja sasa ya kuitazama Katiba mpya ambayo itakwenda kuleta mabadiliko ya kupata viongozi wanaokwenda kuendesha nchi kwa kufuata sheria, kanuni na utaratibu wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushauri; la kwanza kuna haja ya kuwa na semina elekezi kwa hawa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya baada ya kuteuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili, kuna haja sasa ya kubadilisha approach ya kuwapata hao ma- DC na Wakuu wa Mikoa kuliko ilivyo sasa. Kama Mkuu wa Wilaya anaweza kwenda Kamati ya Ulinzi na Usalama na bado hana mafunzo yo yote yanayohusiana na ulinzi na usalama ni hatari kwa Taifa letu. Yamekuja kufahamika leo yaliyofanyika Hai, mambo yameshaharibika, hatutaki yarudie. Nazungumza leo kama Mbunge wa Nkasi yanayoendelea kule kama msipochukua hatua kama Mbunge na mzaliwa wa pale; tutatumia nguvu ya umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza inavyowezekana, nimetoa taarifa inavyowezekana, lakini wapo kimya, naamini kama ni matatizo yake wachukue hatua ila kama wamemtuma watamuacha aendelee kufanya anayoyafanya leo. Sikukusudia kuzungumza haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye TASAF. Upande wa TASAF nimpongeze Waziri pamoja na Naibu wake; wamekuwa wasikivu sana, lakini kuna changamoto pia ya kupata wanufaika wa TASAF. Mwongozo ulivyo na watendaji kule chini hawafuati kama mwongozo unavyotaka. Wanapita Wenyeviti wa Serikali ndiyo wanaandika watu badala ya kwenda kupigiwa kura kwenye mkutano wa hadhara kwa kuwa wananchi wanafahamiana, wanajua nani ana sifa nani hana sifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye TASAF hiyo, umekuwa sasa ni utamaduni kwa wale wanufaika kwa kuwa lengo ni kuwatoa kwenye umaskini, ile siku ambayo wanatakiwa wakapokee hiyo fedha ya TASAF wanalazimishwa kukatwa bima, nani aliwaambia bima inalazimishwa? Kama mtu anapewa 40,000; 70,000 anakatwa bima na kibaya zaidi, wengi wao wanaokatwa hiyo fedha ni wale ambao wapo kwenye msamaha wa matibatu wameshafikisha miaka 60. Kwa hiyo, hakuna tofauti na mwingine ambaye anaweza kuiba fedha za Watanzania. Kuna haja ya kuchukua hatua kwa watu ambao wamefanya hivyo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hoja anayoizungumza ni kweli kabisa na ndiyo maana kwa sasa Serikali imekuja na approach mpya juu ya fedha za TASAF kuzielekeza kwenye miradi ya kimkakati kwa mfano barabara, zahanati, shule ili wanufaika wengi zaidi fedha hizi zikawasaidie na zisiwasaidie watu wachache kwa faida ya watendaji wasiokuwa waaminifu. Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khenani, taarifa hiyo unaipokea?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba niendelee naamini wenye changamoto hizo...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khenani kwa mujibu wa kanuni zetu.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naikataa kwa sababu wanaopata shida…
NAIBU SPIKA: Wewe unasema siikubali, basi.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, siikubali, naomba niendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza haya kwa sababu mtu kama anajua umuhimu wa bima apewe elimu juu ya bima. Akipewa ile fedha yake anayeuza maandazi akauze maandazi, azungushe ile fedha kwa sababu ndiyo lengo la kumtoa kwenye umaskini; kama alikuwa anaweza kula mlo mmoja aweze kula milo mitatu. Kwa namna nyingine kama anaweza kufanya biashara akazungusha akipata faida atakwenda kukata bima, wasiwalazimishe watu kukata bima na lengo la mfuko huu wa kusaidia kaya maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira hayo ninayoyazungumza leo. Leo wamebadilisha utaratibu wa simu kwamba wale watu wanaotakiwa kunufaika na TASAF watumie simu, kama mtu hana uwezo wa kula milo mitatu anaweza kununua simu ya Sh.50,000? Anaweza kununua simu ya Sh.30,000? Nafikiri kuna haja ya kubadilisha approach, turudi kwenye lengo la kuwasaidia wananchi wetu kuwatoa kwenye umaskini kwenda angalau kwenye kiwango cha kati kwa kuwa ndiyo lengo la fedha hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira hayo ambayo nimeyazungumza aidha watendaji wa Wizara ndiyo wanafanya vibaya huko chini, ni wajibu wa Wizara kufuatilia mwenendo unaoendelea huko chini, yawezekana wanachokiubiri siyo hicho kinachoendelea huko chini. Natambua wanafanya kazi kubwa sana, lakini haitakuwa na maana kama wanafanya kazi kubwa hapa ndani ya Bunge halafu huko chini maagizo yakienda hayatekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye hoja nyingine ambayo ni suala la kukaimu kwa hawa watumishi. Halmashauri ya Nkasi inaongoza kwa watu ambao wamekaimu zaidi ya miaka mitatu. wakati mwingine Wakurugenzi wanashindwa kuwapa utaratibu mzuri watumishi hawa na kupelekea kukosa haki zao za msingi. Kwa sababu, kukaimu siyo shida sana, lakini je, wanakaimu kisheria? Wanapewa barua na Katibu Mkuu? Maana anaambiwa tu kaimu, mwisho wa siku anasema nadai fedha yangu, wanamwambia ulikaimu kinyume na utaratibu. Sasa kwa nini anakosa haki kwa kosa la watu wengine? Kuna haja ya ninyi kufuatilia vizuri ili haki za hao watumishi zipatikane.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa sababu ya muda, kustaafu siyo dharura. Toka mtu anaajiriwa, mnajua kwamba huyu mtu atastaafu. Labda mtu aliyekufa. Kwa hiyo, tuache visingizio... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)