Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Kwanza kabisa napenda nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa ya moyo wangu kumpongeza na kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu kipenzi, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza utawala bora. Kwa kadri tulivyofundishwa utawala bora una misingi yake. Msingi wa kwanza wa utawala bora ni utawala wa sheria na hii ndiyo nyumba ya kutengeneza sheria, humu tulimo. Msingi wa pili wa utawala bora ni kuheshimu haki za binadamu, msingi mwingine ni mgawanyo wa madaraka (check and balance). Sasa mimi nilitaka angalau nipite kidogo kwanza katika kulitazama suala la utawala bora na hasa katika siku za karibuni tangu Rais wetu ameanza kazi rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichukue nafasi hii kusema kwamba yalikuwepo mambo ambayo katika utendaji wa kawaida, wengi tulikuwa tunayalalamikia na tulikuwa tunataka yatazamwe; nayo ni haki za binadamu hasa katika suala zima la mtu kushtakiwa na process nzima ya mashtaka yake na hata kufikia Mahakama kutoa maamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nafasi hii, napenda kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameonesha nia kubwa ya kusimamia misingi ya utawala bora. Inawezekana tukawa ni watu tunaosahau kwa haraka, lakini wapo watu walikuwa wamekaa rumande kwa makosa mbalimbali kwa muda wa miaka mitano, sita hadi miaka saba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais huyu amekuja kusema hapana, haiwezekani, huu siyo msingi wa utawala bora. Amefika mahali ametaka upande wa mashtaka uangalie kama watu hawa hakuna ushahidi wa kutosha waruhusiwe wawe huru. Wamekuwa huru wakiwemo viongozi wa madhehebu ya dini, wafanyabiashara na wananchi mbalimbali. Hata wale waliokuwa wamefunguliwa mashtaka, wengine wamefika mahali wamesema, wayatazame hayo mashtaka na upande wa mashtaka ukajiridhisha kwamba baadhi ya watu wanaweza wakafika mahali wakaachiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wanasiasa wako walionufaika kutokana na uamuzi huo wa Serikali, akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe. Napenda wenzangu tusisahau mambo haya mema yanayofanywa katika kuimarisha misingi ya utawala bora. Nami hapa napenda niendelee kuwatia shime Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu wa Wizara hii, najua ni watu wazuri, wachapakazi wazuri, lakini endeleeni kusimamia misingi hii ya utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka ieleweke vizuri kwamba jukumu mlilopewa la utawala bora linakwenda zaidi ya Wizara yenu, kwa sababu mambo yanayohusu utawala bora mengine yanafanywa hata na Wizara ambayo siyo Wizara ya Utumishi na Utawala Bora. Ukienda Wizara ya Mambo ya Ndani, wanasimamia mambo mengi sana ya utawala bora; na huko mkiacha, watachafua sifa ya Wizara yenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru niliwahi kumsikia mzee wetu Mheshimiwa George Huruma Mkuchika akiwa Waziri wa Wizara hiyo, siku moja akiwaambia Wakuu wa Wilaya kwamba jamani, mnapofika mahali mkaanza, nitakuweka ndani, nitakuweka ndani, mkamate mweke ndani, hamchafui image ya Wizara nyingine, mnachafua ya Wizara yangu mimi ya Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, nawajua ninyi ni watu mahiri, watu wasikivu, watu wanyenyekevu na marafiki wakubwa wa wananchi na Wabunge, nawaomba sana muwe na wivu mnapoona Wizara nyingine katika kutekeleza majukumu yake inakiuka misingi ya utawala bora. Usifike mahali mkakaa kimya mkasema haya yako kwenye Wizara nyingine. Wawe ni Ma-DC wawe ni Ma-RC wawe Watendaji wa Kata, sijui wa vijiji, wakikosea misingi ya utawala bora, wanachafua image ya Wizara yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka tunacho chombo hapa cha Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB). Chombo hiki kimeendelea kufanya kazi yake vizuri ingawa sisi wenyewe ndio tunakikamata mikono na miguu ya kufanya kazi. Tuliongeza makosa ya rushwa kutoka makosa saba mpaka kufikia 24, lakini katika makosa yote hayo ni kosa moja tu ndilo ambalo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa inaruhusiwa kulipeleka moja kwa moja Mahakamani. Makosa mengine yote ni lazima wapeleke Ofisi ya Mashtaka, yaende kwa DPP, ndiyo yapate kibali kwenda Mahakamani. Huku ni kuwashika miguu na mikono Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri wakati sasa umefika, mje hapa na Miswada ya Sheria inayowaongezea nguvu PCCB kufanya prosecution ya kesi zao nyingine za makosa ya rushwa Mahakamani moja kwa moja. Kwa mfano, leo tuna matumizi ya nyaraka kwa udanganyifu, yaani wapo watu ambao wanafanya manunuzi, wanatoa risiti feki, wanaziweka katika matumizi ya Serikali na wanachukua fedha nyingi ya Serikali. Hili ni moja ya kosa, lakini PCCB hata wakimkamata mtu huyu ni lazima wapeleke kwenye Ofisi ya Mashtaka ya Serikali ili iende kwa DPP kupata kibali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la ufujaji na ubadhirifu…

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa anayechangia kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 22 cha Sheria ya National Prosecution Service Act, Sura ya 430, Mkurugenzi wa Mashtaka ameendelea kuwateua Maafisa wote wenye sifa ndani ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuendesha mashtaka pale anapoona inafaa; na amekuwa akifanya hivyo kila mwaka.

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Ng’enda, unaipokea taarifa?

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea na ninadhani inaboresha mchango wangu. Nataka madaraka hayo ya DPP yaondoke ili hawa watu wa PCCB waweze kwenda moja kwa moja. Ni nzuri na ninashukuru kwamba hiyo ni hatua muhimu, lakini tunataka madaraka haya, mpaka upeleke kwa DPP au DPP ndio amteue, hapana. Tufike mahali PCCB iwe na uwezo wa kukamata na kupeleka Mahakamani moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hilo, kuna matumizi mabaya ya madaraka na yamefika mahali yanahujumu uchumi wa Taifa letu kwa kiasi kikubwa sana. Wapo watu wamefika mahali wanatumia vibaya madaraka katika kutoa tender na vitu vingine. Unaangalia rushwa ya mtu kupokea na kutoa, lakini hii ndiyo rushwa mbaya zaidi. Rushwa nyingine zimefika mahali majengo yanajengwa chini ya kiwango. Tuwaruhusu PCCB na tuwaongezee nguvu; na ikiwezekana tuwaongezee vile vile wataalam, maana sasa hivi unakuta mtu wa kufanya valuation ya majengo yuko Makao Mkuu. PCCB Kigoma wakiwa na tatizo, wamwombe kutoka Makao Makuu. Tuwaongezee nguvu ili ikiwezekana watu hawa wapatikane katika maeneo ya Mikoa na waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo nataka kulizungumzia ni suala la utumishi; upandishaji wa madaraja watumishi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, hebu angalieni kwenye Halmashauri zetu, kumekuwa na matatizo makubwa. Maafisa Utumishi wetu kwenye Halmashauri wanafika mahali hawawapendekezi baadhi ya watumishi wenye haki ya kupandishwa madaraja. Inatokea hivi na inafika mahali mpaka mnakwenda mwaka wa fedha umempita; na wanafanya hivyo wakati mwingine kwa hila; wakati mwingine mpaka watazamwe tazamwe ndiyo waweze kuwapendek0eza. Kwa hiyo, wapo watumishi wenye haki ya kupandishwa madaraja ambao hawapandishwi kwa sababu tu Maafisa Utumishi kwenye Halmashauri hizo hawatekelezi wajibu wao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)