Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nianze na pongezi, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anatumia mbinu mbadala kuitangaza nchi huko duniani na kutuletea faida kubwa sana Watanzania. Na hivi karibuni tu mtaanza kuona faida ya ile Royal Tour ambayo imezinduliwa wiki iliyopita kule marekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili nimpongeze sana Waziri na timu yake kwa jinsi ambavyo amewasilisha vizuri hotuba yake hapa Bungeni, lakini vilevile kwa namna walivyojipanga kuboresha mambo mbalimbali katika utumishi wa umma na utawala bora. Kwenye hotuba tunaambiwa hapa kwamba, Serikali itaboresha upimaji wa utendaji, lakini vilevile wanaanzisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ambao utaunganisha watekelezaji wote kuanzia Serikali za Mitaa mpaka Serikali Kuu. Hapo kwa kweli, nawapongeza sana, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu umejikita hasa kwenye maeneo matatu, mawili hasa. Katika kupima utendaji tunapima nini? Na katika ufuatiliaji na tathmini tunafuatilia nini? Na tunatathmini nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi sana ambayo yanafanyika katika hayo maeneo mawili lakini kwa muhtasari unaweza ukayachanganya changanya ukaweka katika sehemu tatu kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza tunapima uelewa au kwa Kiingereza wanaita clarity, uelewa wa nini, tunapima uelewa wa sera, uelewa wa sheria, uelewa wa kanuni, uelewa wa miongozo mbalimbali inayotolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama watumishi wanaelewa vizuri Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo tunategemea kwamba wasikosee, tunategemea kwamba akija mkaguzi yoyote akute kila kitu kiko vizuri. Sasa kama uelewa uko chini basi tiba yake ni mafunzo kazini, kwa nini? Inawezekana huyu mtu alikuwa anaelewa sera zamani, alikuwa anaelewa sheria, anaelewa kanuni, anaelewa taratibu lakini kuna wakati anasahau. Kwa hiyo ni muhimu kumkumbusha kupitia mafunzo kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni kweli kwamba kila Wizara, kila Taasisi itakuwa na bajeti yake ya mafunzo, bajeti hiyo ni kubwa kiasi gani na itatoa itatoa mafunzo gani, hii Wizara ndiyo inatakiwa iratibu. Wizara hii inatakiwa iratibu mafunzo yote yanayofanyika huko kwenye Wizara mbalimbali na Taasisi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba watumishi wanauelewa wa kutosha wa nini wanatakiwa kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda sehemu ya pili nikumbushe mafunzo umuhimu wake, wale watu wa dini wanajua kwamba Bibilia iliretemka zamani sana Quran iliteremka zamani sana, lakini karibu kila siku watu wanakumbushwa maandiko ya dini, vilevile hata Serikali inatakiwa lazima kukumbushana masuala hayo ambayo nimeyatamka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ni mazingira wezeshi ya kazi au waingereza wanasema conducive environment. Kuna vipengele vitatu hapo, kipengele cha kwanza kabisa ni rasilimali fedha. Hapa Bungeni tunapitisha bajeti kwenye Wizara mbalimbali, kwenye Taasisi mbalimbali, kwenye Idara mbalimbali tunapitisha bajeti hapa, lakini ni kiasi gani bajeti ile inateremka kwa watekelezaji inatakiwa ipimwe. Sasa hiyo kwenye ufuatiliaji na tathmini hiyo ni lazima iwe mada kubwa kabisa katika kazi, fedha imeenda kiasi gani, imepokelewa lini imetumikaje, imetumika kwenye kazi gani? Kuna ufanisi gani umepatikana? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ni rasilimali watu. Kama hatuna rasilimali watu wa kutosha kwa maana ya idadi ya watumishi inayojitosheleza tusitegemee ufanisi wa kazi. Kwa hiyo, eneo hili nalo lazima lifuatiliwe vizuri na lipimwe. Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam Jiji ambalo linaongoza kwa ulipaji wa kodi hapa nchini, kama TRA pale Dar es Salaam wanahitaji watumishi 1,500 halafu kwa sasa hivi wako 700 ina maana ni chini ya 50% usitegemee ufanisi mzuri wa TRA. Ndiyo maana juzi wameongeza watumishi 300 kwa ajili ya Kariakoo tu peke yake, hili suala la idadi ya watumishi ni la muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Sikonge nina vijiji 71, katika vijiji 71 nina VEO ambao ni substantive, ambao wameajiriwa Serikalini ni VEO 30, ina maana sina VEO 41! Unategemeaje ufanisi wa kazi kwenye Serikali za Mitaa namna hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwezi Agosti, mwaka jana Halmashauri yangu imeomba kibali Utumishi cha kuajiri watumishi 821 hadi leo hatujapata kibali hata cha mtumishi mmoja ukiacha wale wengine ambao wanakuja kupitia Wizara zingine, kupitia TAMISEMI, kupitia Afya na kupitia Wizara zingine. Tumeomba watumishi 821 hatujapata hata mmoja. Kwa hiyo, ufanisi wetu kwa kweli huwezi kuupima vizuri kama tuna shida ya watumishi namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha tatu tunapima uwepo na matumizi ya vitendeakazi working gear, vifaa gani vinahitajika ili watumishi waweze kufanyakazi kwa ufanisi. Kwa hiyo, Wizara hii tunaitegemea ifuatilie na kipengele hiki, vifaa gani vitendea kazi gani vinahitajika ili watumishi wafanye kazi zao kwa ufanisi, kama tunategemea ufanisi mzuri ni muhimu kipengele hiki kiwekewe nukta na Waziri Mheshimiwa Jenista Mhagama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya tatu ambayo tunaipima ni umahiri au weledi wa kazi (competence). Najua hiyo kengele ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, competence huwa hatuipimi kwa idadi ya vyeti alivyonavyo mtumishi. Unaweza ukakuta mtu ana-PhD lakini anashindwa weledi wa kazi na mtu ambaye ana cheti. Kwa hiyo, weledi wa kazi tunaupima kwa namna mtu ambavyo anatimiza majukumu yake ndani ya wakati halafu ana ripoti matokeo ya kazi yake, anayaripoti kwa mkubwa wake ndani ya kabla hajaulizwa, huyo ndiyo anafanyakazi zake kwa weledi. Lakini mtu ambaye kila siku ni wa kusukuma Sukuma, mtu ambaye kila siku lazima aulizwe ndiyo atoe taarifa, huyo siyo mweledi kwenye kazi. Kwa hiyo, tunapompima mtumishi kama ana weledi wa kutosha kwenye kazi tunapima je anaipenda kazi yake? Positive attitude kwenye kazi, lakini kinyume chake hapo sasa kuna utoro, kuna uzembe na mengine mengi sana. Kwa hiyo competence hujengwa zaidi na mambo yale mawili ya kwanza niliyoyataja yaani uelewa pamoja na mazingira wezeshi, kama uelewa na mazingira wezeshi ni duni huwezi kutegemea watumishi wawe mahiri kwenye kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndiyo misingi mikuu ya kupima utendaji na vilevile kupima kama kweli tunafuatilia vizuri taasisi zetu na kama tunafuatilia Serikali vizuri. Tumeshauri mara nyingi lakini mimi leo nimefarijika sana hapa, kwa jinsi ambavyo Waziri ametamka hapa Bungeni kwamba sasa Serikali inaenda kuandaa mfumo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini, hii kitu namna hongera sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)