Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa dada yangu Mheshimiwa Mhagama kupata uteuzi huu katika Ofisi hiyo, lakini pia mdogo wangu Ndejembi kupata nafasi hiyo nina imani wanakuja kufanya kazi kwa weledi kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimpe ushauri Mheshimiwa dada yangu Mhagama katika jambo la kwanza; namwomba sana atengeneze clinic za kusikiliza matatizo ya wastaafu katika nchi hii, atengeneze Makamishina Wasaidizi waende katika mikoa, wazee wastaafu wanapata shida sana, wanatembea na mafaili, mtu anakwenda kustaafu ana mwaka mmoja hajalipwa mafao yake. Sasa hili ni tatizo kubwa sana. Serikali inapata dhambi bila kujua tuna shangaa mvua hainyeshi, kwa sababu kuna watu wamedhulumika haki zao, hizo zinaitwa dhambi baridi. Kwa hiyo, wawatendee haki hawa wastaafu, mtu ameajiriwa, amefanya kazi Serikali miaka 40, halafu bado unamwomba akulete salary slip ya kwanza aliyoajiriwa nayo, akuletee barua ya uteuzi, ana miaka 40 ameitunzaje hiyo kitu. Sasa hii ni hatari kubwa sana, hizi dhambi hebu waziache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akiweka makamishna wakasikiliza, wanatoka katika wilaya anakuja, kwa mfano, akitoka Sengerema katika Jimbo langu anakwenda Mwanza nauli Sh.3,000 anapeleka hoja zake pale, anasikilizwa, anarudi na wale makamishna waje pia katika Makao Makuu ya Wilaya wanasikiliza kesi za wastaafu. Kwangu kuna askari mmoja ana miaka 40 amefanya kazi Serikalini halafu amekosa pesa za kumsafirisha kurumrudisha kwao, hazipo. Sasa hii ni tatizo kubwa sana, ametumikia kwa uweledi na kwa uaminifu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mheshimiwa Waziri ni suala la hawa watumishi ambao ni Makatibu Tarafa na DAS. Sasa ifikie katika nchi hii tubadilishe huu Muundo wa Utumishi hawa wapo kwa Mheshimiwa Waziri kwenye utumishi lakini asilimia 98 wanafanya kazi TAMISEMI. Hebu waangalie huu muundo haujakaa vizuri, wanaishi kwa shida, wanafanya kazi, ni watumishi wa Wizara ya Utumishi, lakini wakati huo wanafanya kazi za TAMISEMI, wakiamka asubuhi ni kazi za TAMISEMI, lakini mwajiri wao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais. Sasa hili ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bajeti zao, unakuta Katibu Tarafa ana Kata 13, hana pesa za madaraka, lakini waliopo chini yake Mkuu wa Shule, sijui nani, Waratibu, Watendaji wa Kata, wote wana fedha za madaraka, Katibu Tarafa hana, hana Ofisi Katibu Tarafa na hao Makatibu Tarafa wanahitaji wasaidizi, lazima wapate Makatibu Muhtasi wale wa kuwachapia barua zao, lakini wawe na matarishi wa kupeleka zile barua pia, Wahudumu wa Ofisi, sasa hao Makatibu Tarafa wanakaa kule kama nani, lakini wanafanya kazi kubwa sana za kumsaidia Mheshimiwa Rais, wao ndiyo wa kwanza kupata taarifa, wanapeleka kwa Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya anapeleka kwa Mkuu wa Mkoa, inafika sasa waheshimike hao Makatibu Tarafa. Makatibu hao hawana usafiri na kama wana usafiri hawana mafuta. Kwa hiyo, Mkurugenzi hawajibiki kumpa mafuta yule Katibu Tarafa, sasa hili ni jambo ambalo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ma-DAS wetu sisi pia wanaishi kwa hisani ya Mkurugenzi wakati yeye DAS ndiyo anatakiwa akamsimamie Mkurugenzi katika utendaji wake wa kazi. Hili naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie na kwake sina mashaka yoyote, hili atafanikiwa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kupata mafunzo Wakurugenzi wanaitwa sana, wao ndiyo watendaji, kwa miezi mitatu anaweza akaja Dodoma mara sita, lakini DAS ambaye ndiyo msimamizi wa shughuli zote za wilaya kupata mafunzo Mungu nihurumie sijui wanakuja lini kupata mafunzo, sasa hili ni tatizo. Akiitwa Mkurugenzi kupata mafunzo basi na DAS aitwe, kwa sababu ndiyo mtendaji wa shughuli za kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili ambalo nataka nizungumze na Mheshimiwa Waziri katika kukushauri, ni suala la TASAF, TASAF imekuwa ni mtihani mkubwa katika nchi hii. Waheshimiwa Wabunge wote anaowaona hapa katika majimbo yao wana malalamiko ya TASAF. Kwa kuwa yeye ni Waziri na ana Naibu Waziri basi mmoja ashughulike na kutembea nchi nzima kuona matatizo ya hawa wazee wetu wanaopata misaada hii ya TASAF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu siyo mzuri unaambiwa kwamba wazee wanalipwa kwa mtandao, mzee hajui kusoma na kuandika, halafu leo alipwe kwa kutumia mtandao, pesa ya swadaka tena inakwenda kudhulumiwa umeshaona wapi. Serikali inatoa msaada na ule msaada unakwenda kuibwa tena. Sasa hili jambo la TASAF liangaliwe, hawa wazee wetu kwa sababu tayari tumeshawaweka katika huo mfumo.
Vilevile wanaokwenda kupewa hizi pesa za TASAF kuna wengine wana nguvu, lakini ni ndugu wa mtu Fulani, hilo ni tatizo na unaambiwa kwamba kwa sababu labda ni balozi wa CCM, hana sifa kwa sababu anafanya kazi kama balozi wa CCM au sijui balozi wa chama gani? Haiwezekani kwa sababu kile ni cheo ambacho anacho hakina mshahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la watumishi nimesikia humu Wabunge wanalalamika kwamba watumishi wa kike wanakuwa hawakai katika maeneo yao, hapa natoa tu ushauri kwamba, wazungumze na watu wa Ustawi wa Jamii waliopo kule katika wilaya, lakini nataka nimshauri pia Waziri atuambie na sisi Wabunge kule waache malalamiko haya kwa sababu ukisikia mtumishi anahama kwamba eti hakuna huduma muhimu hasa hawa mabinti wa kike wanaokwenda katika maeneo kama Walimu, Manesi na watu wengine kwamba hakuna huduma muhimu, siyo huduma hizo ni huduma za kifamilia, waolewe kule tuwaambie watu wetu waoe.(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakwenda kufanya mkutano kwenye kata anayelalamika, Diwani analalamika Mheshimiwa Mbunge wanakuja watumishi wanaondoka, analalamika Mwenyekiti wa Kijiji, sasa unamwambia mbona ninyi mna tatizo…
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya taarifa.
T A A R I F A
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naheshimu mchango wa kaka yangu Tabasamu, mabinti au wafanyakazi wa kike hawahami kwa hicho anachokisema, wengi wanapata shida mazingira magumu ya kazi ikiwepo nyumba na gharama za usafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, halipo suala la uchumba au kuolewa hapa. Ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasamu, unapokea taarifa?
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa hii, kwa sababu ninachotaka kukwambia, akisikia kwamba mazingira magumu, ni haya ya kifamilia. Mwanamke akipata hayo, hawezi kukimbia wala kuondoka kwa sababu ya nauli. Kwa hiyo, ushauri wangu, hawa wananchi huko kwenye Majimbo yetu wasichague wakaweka ukabila kwamba amekuja Mzaramo asiolewe na Msukuma, waoeni Wasukuma. Hii massage mimi ndio napeleka. Amekuja Mgogo, eti kwamba kaletwa hapa Nurse Mgogo, muoeni huyo Mgogo. Kwa sababu utafiti uliopo kwanza ni kwamba familia ya Walimu, watoto wa Walimu ndio wanaofanikiwa kuliko Walimu. Sasa leo mnakuja kulalamika kwamba Mheshimiwa Waziri… (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna Mheshimiwa Mbunge amesimama. Mheshimiwa Esther Matiko, umesimama kwa kanuni gani?
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, akija Mnzanzibari aolewe.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam!
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Naam.
T A A R I F A
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa...
MWENYEKITI: Umesimama kwa kanuni gani?
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kwa kanuni ya 77 kutoa taarifa.
MWENYEKITI: Endelea.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa Mheshimiwa Tabasam taarifa kwamba wanaoomba kuhama ni both sides, wanaume kwa wanawake, lakini anapojielekeza kwa wanawake, nimpe tu taarifa tu kwamba nature ya wanawake ilivyo anaweza akavumilia muda mrefu hayo anayoyasema bila kuathirika kuliko wanaume walivyo. Kwa hiyo, naomba ajenge hoja yake bila kudhalilisha jinsia nyingine. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wakati Mheshimiwa Mbunge anazungumzia kuhusu kuhamisha watumishi, wengine unakuta tayari wako kwenye ndoa zao, wanataka wahame wawafuate wenzi wao. Kwa hiyo, ajenge hoja bila kuweka udhalilishaji wowote ule. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam, unapokea taarifa hii aliyoisema Mheshimiwa Matiko?
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo hoja yake. Siipokei kabisa taarifa yake. Naomba ulinde muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wanaume wanaokuja katika maeneo yetu vijijini, nao wanakosa watu wa kuwaoa kwa sababu tu kwamba amekuja Mmasai pale au amekuja Mzaramo kule Usukumani, na huyo Mzaramo aruhusiwe kuoa Msukuma, ndiyo haja yangu mimi. Watumishi watabaki kuwepo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naona hizi taarifa zinakula muda wangu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam muda wako umekwisha. Nakuongezea dakika moja kwa ajili ya kuhitimisha hoja yako. Kaa chini Mheshimiwa Bulaya.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la watumishi, Serikali itaajiri watumishi 32,000. Ushauri wangu ni kwamba katika hao watumishi 32,000 tunayo Majiji yetu saba, wapewe mia tatu, mia tatu; na Makao Makuu ya Wilaya tupewe mia mbili mia mbili. Huko ndiyo tunafanya upekuzi, tutawajua watu wetu. Huu ndiyo Utaifa. Habari ya kuingia online halafu wanaenda kuajiriwa watu wa mkoa mmoja, hatukubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana kwa mchango huo. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.