Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama kutoka Wizara ya Utumishi na ambao kwa kweli wapo chini ya Mheshimiwa Rais mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza na TASAF niigusie kidogo ili baadae sabufa ikifunguka nisije nikasahau jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri nilimuomba watu wa TASAF pale Mvumi kuna kitendo kibaya sana kilifanywa pale, walengwa wa TASAF wanagawiwa fedha zao halafu mgambo wakasimama dirisha la pili, halafu wakaanza kuwachangisha mchango kwamba nishike mkono wanachangia elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo nimemlalamikia Mheshimiwa Waziri na Naibu wake bahati nzuri nawashukuru sana wamelifanyia kazi na nimeona barua kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa TASAF kwamba zile pesa zirudishwe kwa wale walengwa wa Kijiji cha Mvumi Mission na walengwa wote wa Wilaya ya Chamwino ambao walikatwa fedha zao kwa mchango ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nilitaka kushangaa sana mgonjwa badala ya kupewa drip halafu kuna watu wengine wenyewe ndiyo wanamtoa maji sasa. Sasa niombe Mheshimiwa Waziri tamko liwe la haraka utakapojibu hapa, hebu jambo hili lifanyike haraka ili wale walengwa warudishiwe pesa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina mambo machache sana, moja ni mgawanyo wa ajira. Tukisema tutegemee mtandao peke yake jamani nataka niwaambie sijui kuna nini kinatokea hata kwenye mtandao, mtandao wakati mwingine unaruka watu maskini, huwezi kuamini mimi nitakupa ushahidi hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna mgao wa net, yaani pale Mvumi mission wote wenye uwezo wa kati majina yao kwenye mtandao yamesomwa nikiwepo Mbunge kupata net ya bure lakini vipofu na wasioona wote hawamo mtandao umewaruka. Sasa hili la ajira tukisema tuombe online kuna vijana wafamilia maskini hawatakaa wapate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri, kwa sababu Taifa hili tunafahamiana, hizi ajira zitolewe kiwilaya au zitolewe kijimbo. Ukizishusha kama zilivyo ukasema Jimbo fulani limepata ajira nane Mbunge na watu wake pale na sifa wanazo, wataajiriwa watu ambao tunawafahamu, lakini kila zikitoka ajira watu unaowajua kwenye Jimbo lako hawamo na wenye sifa hawamo. Jamani nina mashaka na mtandao unakwepa watu maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kulizungumza, tukiwa mgawango wa ajira kiwilaya au kijimbo tutamaliza hayo matatizo kwa sababu nchi nzima itaajiriwa mara moja utakuwa umewapata watu kutoka nchi nzima.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Dah, kaka yangu yaani leo niko vibaya. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde, Kanuni inasema kwa idhini ya Spika atatoa taarifa, kwa hiyo sijaidhinisha bado.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya naendelea, ndiyo nimesema aniache kidogo leo nina mambo mazito, Mheshimiwa Tabasam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ninalotaka kulizungumza hapa, kipaumbele cha ajira wapewe wale ambao wanaojitolea. Kuna watu wanajitolewa, wana miaka mingi wanafanya kazi ya kujitolea kwenye kila Idara, hao ndiyo wapewe kipaumbele cha kuajiriwa kwanza, lakini tukiwaweka kwenye kapu moja, wanaojitolea wanakosa wanapata watu wengine. Nchi yetu ina wastaafu... (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam.
T A A R I F A
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji, mtandao wenyewe leo ni siku ya tatu umezimwa, unapatikana mijini tu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde, endelea.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sasa niwaombe watoa taarifa wengine watulie, nataka kuzungumza mambo makubwa ya nchi.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea.
MWENYEKITI: Unaipokea, ahsante, endelea.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, watu wanaofanya kazi ya kujitolea ndiyo wapewe kipaumbele cha kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina wastaafu aina nyingi sana, ina wastaafu ambao wametumikia Serikali, lakini bahati mbaya sana ina wastaafu ambao hawajawahi kufanya kazi popote, yaani yeye anazaliwa, anatakiwa ajifundishe kilimo anaingia kazini, anaingia kusoma, akishamaliza kusoma anaomba kazi hapati, kila akiomba kazi hapati, kwa hiyo kilimo hajui, kuchunga hajui na kazi aliyosomea hana. Huyu tunamweka kwenye kundi gani? Hawa katika uzee ndio tunashauri wapewe kiinua mgongo cha wazee ili waweze kuishi, kwa sababu Tanzania ni ya kwao na sisi ndiyo tumewanyima hiyo ajira. Qualifications anazo lakini mpaka anazeeka hajawahi kuzitumia mahali popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka niende kwenye suala la Utawala Bora. Nchi yetu imeweka vizuri sana masuala ya Utawala Bora kisheria lakini kuna baadhi ya vyama, kwa mfano pale Zanzibar ACT-Wazalendo tunashirikiana nacho kwenye Utawala Bora, sisi tuna Rais, tuna Serikali, wao wana Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini nimemsikia Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Zitto, anamnanga Mheshimiwa Magufuli kana kwamba Zitto hashiriki kwenye Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nataka niliseme, Mheshimiwa Magufuli aheshimiwe, Zitto aelewe kwamba suala la kufiwa ni suala kubwa. Haiwezekani tuache kwenye utawala bora kulizungumza suala la Magufuli kusemwa vibaya na mimi sitaacha. Mheshimiwa Zitto anatutaka tunaompenda Mheshimiwa Magufuli tukazikwe naye. Zitto ndugu zangu amewahi kufiwa na mama yake, mimi sitaki kuingia huko, mama wa Zitto ni mama yangu mimi, ametangulia, mimi nimewahi kufiwa na baba yangu, lakini ACT wamewahi kufiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Zitto analazimisha sisi tumseme vibaya Maalim Seif, hatuwezi, hatuwezi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninapoongea hapa Waislam mmefunga, dini inakataza kuwasema vibaya marehemu, Zitto ni Muislam anajua. Zitto ametukosea sana Watanzania, Zitto atuombe radhi Watanzania, Zitto amemkosea sana mama Magufuli, Zitto ameikosea sana familia ya Magufuli. Hili jambo siyo sawa. Ndugu zangu tusifikiri kwamba kumsema vibaya Magufuli kutatusaidia, hawezi kujibu, hayupo. Kama ulikuwa na tatizo naye maliza utakuja kukutana naye kwa Mwenyezi Mungu. Mtu akishatangulia, kitabu chake kinafungwa tunamwachia Mwenyezi Mungu kuja kutoa hukumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje watu mnakuwa waoga Viongozi wakiwepo hamsemi, wakiondoka ndiyo mnasema, huu ni uoga uliyopitiliza. Mtu mmoja tu alisema kwa vitendo kwamba yeye hawezi kufanya kazi na Magufuli, Nyalandu aliachia ubunge hapa akaondoka, lakini wote tuliobaki hapa ni watu wa Magufuli na tumefanya naye kazi na tulikuwa tunamsifu. Hivyo ndivyo ambavyo tunatakiwa tumsifu Mheshimiwa Samia na ndiyo kazi tunayofanya hapa, tusiweke unafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie, hawa watu ambao sasa hivi wanamsema vibaya Mheshimiwa Magufuli na kumsifu Mheshimiwa Samia ni wanafiki wakubwa. Mheshimiwa Samia akiondoka watamsema vibaya hivyo hivyo, hivyo hivyo, ni bora mimi Lusinde ambaye niko wazi na siwezi kuacha, haiwezekani!
Kwa hiyo nchi yetu ili iendelee na utawala bora hawa watu tunashirikiana nao, Viongozi waliokufa wale ni watu wazito, Maalim Seif amefanya kazi kubwa, Mheshimiwa Magufuli amefanya kazi kubwa. Sasa ukisema kwamba wanaompenda Mheshimiwa Magufuli wakazikwe na Mheshimiwa Magufuli maana yake nini? Hii ni kashfa kubwa sana. Zitto aliombe radhi Taifa hili, awaombe radhi familia ya Magufuli na asirudie tena kufanya mambo ya kipuuzi kama hayo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lusinde.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoma imeisha, sasa sabufa ndiyo lilikuwa limefunguka.
MWENYEKITI: Hitimisha hoja yako kwa dakika moja, dakika zako zimeshakwisha.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.