Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipatia fursa hii ya kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Watendaji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kuimarisha muungano wetu, lakini pia kuweka mazingira yetu sawa ili sisi kama binadamu tuwe tunaishi kwa amani kabisa.
Mheshimiwa Spika, nitajielekeze zaidi kwenye maeneo makuu mawili. Eneo la kwanza nitazungumzia suala la muungano nae neo la pili nitazungumzia suala la mazingira.
Mheshimiwa Spika, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muungano wa nchi mbili, kati ya Zanzibar pamoja na Tanganyika. Jana tu ndiyo tumehitimisha miaka 58 ya muungano wetu wa Tanganyika pamoja na Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huwa kila mwezi tunapata taarifa kupitia BOT ambazo zinatambua uchumi wa Zanzibar pamoja na uchumi wa Tanzania Bara, lakini la kustaajabisha taarifa zinapokwenda nje ya nchi kwa maana ya kwenye taasisi za kifedha, World Bank pamoja na IMF taarifa hizi haziendi kwa sura ya kuitambua Zanzibar. Naomba sana, uchumi wa Zanzibar ni mdogo na ni uchumi ambao ni wa Kisiwa, naomba sana kupitia Wizara hii lazima iangalie ihakikishe kwamba, tunapopeleka taarifa za kifedha lazima kuwe kuna figure sura ambayo tayari itaonekana Zanzibar na uchumi wake.
Mheshimiwa Spika, kila mwezi, kila mwaka, IMF pamoja na World Bank wanatoa taarifa namna ya uchumi, wenyewe wanaita Economic update, kwa Zanzibar haitambuliki. Zanzibar ni sehemu ya kisiwa, lakini pia ni nchi ambayo tayari imeunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naiomba sana Wizara yako Mheshimiwa Jafo kuhakikisha kwamba, Zanzibar zinapokwenda taarifa basi uchumi wa Zanzibar unatambulika kwa sura ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende eneo la pili, eneo la mazingira. Niwapongeze sana watendaji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwa upande wa Tanzania Bara. Ikumbukwe kwamba, eneo la mazingira ni eneo ambalo linajumuisha upande wa pili wa Zanzibar. Tunashangaa sasa hivi kuna miradi ambayo inatekelezwa Zanzibar kwa muda wa zaidi ya miaka mitano, lakini fedha Zanzibar hazifiki kwa wakati. Ukiulizia Zanzibar wanalalamika kwamba, fedha zinaganda Tanzania Bara, Tanzania Bara na huku wanasema kwamba, fedha zinafika Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfano mzuri, leo hii kuna mradi ambao unatekelezwa Wilaya yangu ya Kaskazini Unguja kwenye vijiji zaidi ya vitatu. Kuna Kijiji ambacho kinaitwa Mbuyutende, kuna Kijiji ambacho kinaitwa Matembwe Kijini, kuna Kijiji ambacho kinaitwa Juakuu. Fedha zimetengwa nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ikolojia, lakini cha kuchangaza mpaka leo hii zaidi ya miaka mitano miradi ile bado haijakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi tulienda na Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kuna baadhi ya vifaa vimenunuliwa, kuna ununuzi wa boti, boti limenunuliwa zaidi ya Milioni 46. Ni jambo la kustaajabisha na la kushangaza kabisa, boti moja limenunuliwa zaidi ya Milioni 46 haiwezekani hata siku moja, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia tathmini ya sisi ambao tayari tumezaliwa kandokando ya bahari, lakini pia ni wavuvi, boti moja linanunuliwa zaidi ya Milioni 12 siyo Milioni 46. Naiomba sana Wizara yako, Wizara ya Muungano kuhakikisha kwamba, kwenye matumizi ya fedha lazima tuende tukaangalie vizuri. Fedha zinapotea kwa upande wa Zanzibar, lazima tukae tuhakikishe kwamba, fedha zinaenda kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia jambo la pili, kuna ujenzi wa majiko sanifu, jiko moja limejengwa zaidi ya shilingi Laki Saba kwa gharama ya kawaida. Kiuhalisia ukiliangalia jiko moja ni sawasawa na Shilingi Laki Mbili. Upotevu wa fedha ni mkubwa sana, fedha ambazo zinaenda Zanzibar hakuna usimamizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba sana Wizara yako Mheshimiwa Waziri, kwenye fedha ambazo zinaenda Zanzibar za Muungano, zinapoenda Zanzibar Wizara yako ihakikishe ndiyo inasimamia ile fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumefika Zanzibar tumewahoji watu wa Wizara ambao wanashughulika na masuala ya miradi hii hawana majibu. Tunajiuliza nani msimamizi wa fedha hizi ambazo zinakuja Zanzibar? Majibu hakuna kuhusiana na fedha ambazo zinaenda Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa vile muda ni mdogo naomba niishie hapo. Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)