Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria. Mchango wangu utajikita kwenye Fungu Na. 35 la Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa maana ya DPP.

Mheshimiwa Spika, Kamati imeeleza nini imebaini kwenye Ofisi hii. Moja katika mambo makubwa ambayo imebaini ni kwamba Ofisi ya DPP ni Ofisi muhimu sana katika masuala ya utoaji haki, lakini bajeti ambayo imetengwa kwa ajili ya ofisi hii ni ndogo sana katika kukidhi mahitaji ya upatikanaji haki kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili hoja yangu ieleweke, naomba Watanzania wafungamanishe Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na dhana au Dira ya Tanzania ya kujenga uchumi kwa kupitia viwanda na biashara. Utakubaliana nami kwamba moja ya vivutio vikubwa vya uwekezaji na biashara nchini ni utawala wa sheria. Kama hakuna utawala wa sheria, hatutaweza kuvutia uwekezaji wa aina yoyote nchini.

Mheshimiwa Spika, wataalam wanasema, hatuwekezi biashara pale ambapo pana utawala wa viongozi, bali pale ambapo pana utawala wa sheria. Hapa ni mkazo juu ya utawala wa sheria dhidi ya utawala wa viongozi. Tanzania tumepiga hatua kubwa sana kwenye eneo hilo. Awamu hadi Awamu Tanzania imefanya transformation kubwa kutoka kwenye utawala wa viongozi kwenda kwenye utawala wa sheria. Hilo limejidhihirisha sana katika utawala wa Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Awamu hii ya Sita, tumeona namna Mheshimiwa Rais ameendelea kuweka mkazo wa ku-transform mfumo wetu wa utawala ili tuwe na utawala wa sheria ambao utatoa haki kwa Watanzania wengi, lakini pia itafungua fursa za kukua kibiashara. Miongoni mwa mambo ambayo tumefanikiwa sana katika kipindi hiki kifupi; moja, ni zaidi ya Watanzania milioni moja na nusu wamepata huduma ya ushauri wa sheria katika Wiki ya Sheria. Haya ni mafanikio makubwa. Lingine ni uteuzi wa Majaji. Ili kutoa huduma, ni Majaji katika Mahakama ya Rufani tisa na kufanya jumla ya Majaji wote katika Mahakama ya Rufani kufikia 21. Ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na uteuzi wa Majaji katika Mahakama Kuu Majaji 21 wameteuliwa na hivyo Majaji katika Mahakama Kuu kufikia 82. Hii ni hatua kubwa sana katika utoaji wa haki nchini. Sasa tuna Mahakimu 245, hayo ni mafanikio makubwa sana katika Awamu hii. Siyo hayo tu, unaona kwamba Mahakama imepanua wigo wa utoaji haki na imewapeleka Mawakili sasa waweze kutoa huduma kwenye Mahakama za Mwanzo ili kuwafikia Watanzania walio wengi ambao wanategemea sana Mahakama hizi za Mwanzo ili kupata huduma ya upatikanaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye Mahakama zetu ni hatua kubwa sana ambayo ni lazima tuiweke kwenye kumbukumbu za Taifa letu katika Awamu hizi zinazofuatana. Tumeona kuna mafanikio makubwa kwenye ujenzi wa majengo ya Mahakama, lakini pia Ofisi ya DPP imezidi kupanua huduma na sasa ina ofisi karibu katika Mikoa 26 za Kimahakama, lakini Wilaya 14. Hayo yote ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika, nilitamani kabla sijatoa ushauri na mapendekezo yangu niwapongeze sana, kwanza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; Waziri wetu, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu Waziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu nzima ya Wizara hii kwa kazi kubwa ambazo wamezifanya na mafanikio ni makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio haya makubwa ambayo nimeyaeleza bado tuna changamoto kubwa sana ya kuwafikia Watanzania walio wengi huko chini kwenye Mahakama za Mwanzo, ikiwemo Madaba, maeneo yote ya Songea Vijijini, hatuna huduma za uhakika zitakazompunguzia Mtanzania gharama ya kwenda kutafuta haki. Leo Ofisi ya DPP ina ofisi katika wilaya 14 tu, maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba, katika wilaya nyingine za Tanzania zinazobaki mashitaka mengi yanaendeshwa na watu ambao hawana sifa ya kuendesha mashitaka. Askari Polisi ndio wanaokamata, Askari Polisi ndio wanaopeleleza, lakini ndio wanaoshitaki, haki ya Mtanzania itapatikana vipi kama utaratibu huu utaendelea hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rai yangu ni kuiomba Serikali iiongezee fedha Ofisi ya DPP ili iweze kufika katika maeneo yote ya Tanzania, ili iweze kuwafikia Watanzania wanyonge ambao uchumi wao unategemea kulinda haki zao za ardhi na maeneo ya biashara. Watu wananyimwa haki za kufanya biashara katika maeneo mbalimbali, lakini hawana namna ya kutafuta haki hizo kwa sababu wanaotakiwa kulisimamia hilo hawana uwezo wa kufika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ninasema haya kwa Ushahidi. Mpaka mwezi Februari, 2022 kesi za jinai zilizosimamiwa na Ofisi ya DPP ni 42,138 katika hizo ni asilimia 28 tu ya kesi zote zimepatiwa ufumbuzi, hizo nyingine zote zimebaki. Tunawasaidiaje Watanzania kumaliza changamoto hizo kama Serikali haipo tayari kuongeza fedha kwenye Ofisi ya DPP?(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, lakini naiomba Serikali iiangalie ofisi hii. Ahsante sana. (Makofi)