Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. JOSEPH A. THADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara hii nyeti ya Katiba na Sheria. Awali ya yote niipongeze sana Serikali na Wizara, hasa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya kazi nzuri ambayo wamefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria; kwa hiyo chini ya Kanuni ya 117 ya Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2020 nilipata fursa ya kutembea pamoja na kamati kuangalia miradi mbalimbali ya maendeleo ya Mahakama, iliyoko chini ya Wizara hii. Na kwa kweli, lazima nikiri kwamba, tumeona maendeleo makubwa sana katika uboreshaji wa sekta ya utoaji haki. Tumeona majengo ya kisasa kama ambavyo wenzangu wameeleza, tumeona uboreshaji mkubwa sana wa mifumo ya TEHAMA, pamoja na vitu vya kisasa kama hii Call Centre ambayo inawasaidia wananchi kupeleka kero zao.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeona ushirikishwaji wa wadau wengine. Kwa mfano kitendo cha kuwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kupewa ofisi ndani ya Jengo la Mahakama, ili watu wote wanaohitaji msaada wa kisheria waweze kuupata palepale, hayo ni mapinduzi makubwa sana yanayodhihirisha kwamba Serikali ya Awamu ya Sita haifanyi maigizo kwenye suala zima la utoaji haki. Wako serious kwamba, tunataka nchi iende kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nadhani ni jambo ambalo linaeleweka tu kwamba, umuhimu wa sekta ya utoaji haji katika kukua kwa uchumi na utulivu wa nchi. Pamoja na kwamba, Mahakama haiuzi na kununua, lakini wanaouza na kununua hawataweza kuuza na kununua kama Mahakama na sekta ya utoaji haki kwa ujumla haifanyi kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo hayo mazuri tunaendelea kushauri tu kwamba, Serikali iendelee kuwekeza katika sekta ya utoaji haki. Kwa mfano, tumekwenda vizuri katika hivi vituo jumuishi ambavyo ni Mahakama Kuu na Mahakama za Wilaya, lakini bado hatujafika vizuri kwenye Mahakama za mwanzo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika Jimbo langu la Mwanga tumepata jingo la Mahakama la kisasa ambalo liko katika hatua za mwisho kabisa za umaliziaji, lakini kwenye kata 20 ambazo tunazo tuna Mahakama za mwanzo tano tu. Sasa wananchi wengi ni wanufaika zaidi wa Mahakama za mwanzo kuliko hizi Mahakama nyingine huku. Na bahati mbaya kwa utaratibu wa sheria ni kwamba, hata kama Mahakama ya Wilaya au Mahakama Kuu iko ukumbini mwako, lakini kama shauri lako inabidi lianzie Mahakama ya Mwanzo lazima ukaanzie kule. Kwa hiyo, pamoja na kuwa na hizi Mahakama nzuri za katika ngazi ya wilaya na Mahakama Kuu, lakini kuna umuhimu sana wa kuwekeza katika Mahakama za Mwanzo ambako ndiko wengi waliko.

Mheshimiwa Spika, na huku kwenye Mahakama za Mwanzo, au tuseme mahitaji ya watu wengi zaidi yanayoleta kero kubwa yako zaidi kwenye masuala ya ardhi na haya masuala ya familia, kama vile ndoa, talaka, mirathi, n.k.

Mheshimiwa Spika, sasa yako mambo mawili hapa ambayo ningependa kusema. La kwanza ni kwamba, hata tunapokwenda kuwekeza kwenye Mahakama za Mwanzo tuangalie pia kuwajengea uwezo mahakimu walio kwenye Mahakama za Mwanzo juu ya suala zima la sheria za ardhi pamoja na hizi sheria zinazohusiana na mambo ya mirathi na ndoa, n.k. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na suala la sheria zinazohusiana na mambo ya mirathi na (family law), tatizo kubwa kwa kweli, liko kwenye sheria za kimila ambazo hasa ndizo ambazo zinasumbua watu wengi kule chini. Na bahati mbaya ni kwamba, utaratibu wa marekebisho wa zile sheria haupo kupitia Bunge, ila uko kupitia kwenye Halmashauri za wilaya kwa kupitia ile sheria inayoitwa Judicature and Application of Laws ACT, Kifungu cha 12. Ni vizuri hilo eneo likafanyiwa kazi kwa sababu, tunaweza tukawa na miundombinu mizuri sana ya Mahakama, n.k., lakini watu wanatumia sheria za kimila kufanya mambo yao huko na kwa hiyo mateso yataendelea huko chini wakati sisi huku tunabakia na facilities zetu ambazo ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni kuhusu suala hili la Mahakama za Ardhi. Tunaweza kuwa na Mahakama za Wilaya nzuri sana, lakini bahati mbaya ni kwamba, katika level ile ya chini ya wilaya ukiwa na shauri la ardhi lazima uende Mahakama ya ardhi kwanza. Sasa Mahakama za ardhi ziko chache sana, mimi nashukuru Napata Mahakama nzuri ya Wilaya, lakini bado ukiwa na tatizo la ardhi lazima uende Same kwa sababu Mahakama ya ardhi pale haipo. Ni vizuri ikafanyika kama ilivyofanyika kwenye Mahakama Kuu.

Mheshimiwa Spika, hapo awali ilikuwa hata ukiwa kwenye Mahakama Kuu ilikuwa lazima uende kwenye Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, lakini nafikiri mwaka 2010 Mheshimiwa Jaji Mkuu alipitisha circular, tena namshukuru sana kwa hilo, kuzipa Mahakama Kuu mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ardhi, Mahakama kuu zote, Kitengo cha Ardhi pamoja nah ii Mahakama Kuu ya kawaida. Kwa hiyo, nadhani tunahitaji kulifanya hilo katika ngazi ya wilaya pia, ili wananchi waweze kutumia huu uboreshaji ambao unafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la muhimu ni kwamba, tunaweza tukaboresha Mahakama sana lakini tusipoboresha wale washiriki na wadau wa hii sekta ya utoaji wa sheria kama magereza na polisi, bado matatizo yatakuwa palepale. Na kwa bahati mbaya sana lawama huwa zinaenda kwa Mahakama tu wakati ambapo Mahakama mwisho wa siku naweza nikasema ni kama computer kwa hiyo, lazima ulete ui-feed, iweze ku-process na kutoa matokeo. Sasa hayo yanafanyika kwa hawa wadau wengine kama polisi, n.k. Kwa hiyo, ni vizuri maboresho haya yanapofanyika kwenye Mahakama yaende pia kwenye maeneo mengine.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH A. THADAYO: Mheshimiwa Spika, hivi ni kengele ya kwanza au ya pili? Ya kwanza, ahsante.

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa nasisitiza hilo kwamba, ni vizuri maboresho haya yanapokwenda kwenye Mahakama yaende pia kwa hawa wadau wengine. Ukienda kwenye baadhi ya magereza, kama Gereza la Kirumi lililoko katika jimbo langu kwa kweli hali ni ya kusikitisha. Jengo lenyewe ni dogo na ardhi ni ndogo pia, hawana hata mahali pa kupanuka au hata pa kuendesha shughuli kilimo, lakini pia hawana magari na vitu vingine. Kwa hiyo tusipoboresha hawa wadau ni kwamba hata Mahakama zenyewe zitakuwa haziwezi kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, la mwisho nizungumzie kuhusu suala la utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya haki zao kwenye Katiba na Sheria nyingine.

Mheshimiwa Spika, naona kengele imelia; niombe tu kuunga mkono hoja pamoja na kwamba, nilikuwa na hoja ya muhimu kidogo kwenye eneo hilo. Ahsante sana. (Makofi)