Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Napenda kuanza kwa kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha anaweka mazingira wezeshi yatakayosababisha kufikia usawa wa kijinsia katika siasa hapa nchini kwetu Tanzania. Nasema hivi kwa sababu, ndani ya mwaka mmoia wa uongozi wake Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameunda Kikosi Kazi cha Taifa ambacho kimepewa jukumu la kupokea maoni na kutoa ushauri juu ya hali halisi ya demokrasia ya vyama vya siasa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, na ninakumbuka kati ya vitu ambavyo amekuwa akisisitiza kwa kikosi kazi hiki ni kuhakikisha kwamba, wanaangalia pia kwa jicho la kipekee suala zima la usawa wa kijinsia kwenye siasa kuanzia kwenye vyama vya siasa vyenyewe. Nami nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan juu ya umuhimu wa kufanya hivi kwa sababu, kwa mujibu wa Ripoti ya Uchaguzi Mkuu Tanzania ya Tume ya Uchaguzi NEC kati ya wagombea 11,933 waliogombea nafasi mbalimbali kuanzia Urais, Ubunge, Udiwani, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ni asilimia 7.5 tu ndio walikuwa wanawake ilhali idadi ya wanawake waliojiandikisha kupiga kura ni asilimia 53 ya wapiga kura wote.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili. Takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zinaonesha pia asilimia kubwa ya wanawake waliopitishwa na vyama vyao kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi huwa wana fursa kubwa zaidi ya kushinda.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mwaka 1995 CCM ilikuwa na wagombea wanawake saba kwenye majimbo na wanawake saba wote walishinda. Mwaka 2000 wanawake wa CCM ambao waligombea kwenye majimbo walikuwa 13 na kati ya hao 12 walishinda. Mwaka 2005 kulikuwa na wagombea wanawake 19 na kati ya hao 17 walishinda. Mwaka 2010 kulikuwa na wagombea 24 na kati ya hao wagombea 19 walishinda. Mwaka 2015 kulikuwa na wagombea 24 na kati ya hao 18 walishinda kwa upande wa CCM na kwa upande wa CHADEMA kulikuwa kuna wagombea 13 na sita walishinda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii inadhihirisha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa sana wa kushinda kwenye chaguzi endapo watateuliwa. Hivyo, dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikia usawa wa kijinsia inawezekana kabisa endapo tutaweka mikakati thabiti ya kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kabisa kuwa binadamu wote ni sawa mbele ya sheria na kila mwananchi anayo haki ya kushiriki katika masuala ya umma, yakiwemo ya uongozi wa Taifa. Aidha, Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 imegusia umuhimu wa vyama vya siasa kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia wanapotunga na kutekeleza sera zao, wanapoteua wagombea kwa ajili ya uchaguzi na uchaguzi wa viongozi ndani ya vyama.
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na kwamba, sheria ya vyama vya siasa imeweka mazingira haya wezeshi, bado matakwa haya yanakuwa ni magumu kutekelezeka kwa sababu, yanamfanya Msajili wa Vyama vya Siasa anakosa meno ya kuvilazimisha vyama vya siasa vitekeleze usawa wa kijinsia. Kwa hiyo, ili tuweze kufikia dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na usawa wa kijisnia kwenye siasa, yapo mambo ya msingi ambayo lazima yafanyike. Kwa hiyo ningependa kuishauri Serikali yafuatayo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza Sheria ya Vyama vya Siasa liwekwe takwa la kisheria kwamba kila chama cha siasa kiwe kina sera ya usawa wa kijinsia. Jambo la pili, kama ambavyo kwenye Katiba na kama ambavyo kwenye Sheria ya Serikali za Mitaa pia kwenye Vyama vya Siasa viweke kiwango ambacho aidha kati ya asilimia fulani ya wagombea ambao watateuliwa na Vyama vya Siasa wawe wanawake. Vilevile katika mapato ambayo Vyama vya Siasa wanapata kupitia ruzuku, Vyama vya Siasa viweze kutenga kiwango fulani cha fedha ambacho kitakwenda kuwainua na kuwajengea uwezo na kuwasaidia wagombea wanawake.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni katika Sheria ya Uchaguzi huwa kunatokea matendo mengi ya ukatili wa kijinsia wa aina mbalimbali ikiwemo ukatili wa kimtandao pamoja na matusi na kufedheheshwa wakati wa kipindi cha kampeni wakati wa uchaguzi na hasa baada ya uchaguzi. Kwa hiyo, Sheria ile pia ya uchaguzi iweke wazi adhabu ambazo zitatolewa pale ambapo kutakuwa kuna udhalilishaji na ukatili wa kijinsia wa aina yoyote ile kwa wagombea wanawake. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Neema Lugangira kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Salome Makamba.
T A A R I F A
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Neema Lugangira kwamba, Sheria ya Uchaguzi inataka ujapofanyiwa makosa yoyote ya kimaadili upeleke kama ni kosa la jinai kwa sababu udhalilishaji wa kijinsia ni kosa la kijinai, unatakiwa upeleke kwenye mfumo wa kijinai ambao kiuhalisia inaweza ikachukua mpaka uchaguzi unaisha bado kosa lile halijafikiwa hatma. Kwa hiyo, nakubaliana naye kabisa kwamba Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi iseme clear kama kumetokea kosa la jinai, basi mtu aliyemfanyia mwenzie kosa la unyanyasaji wa kijinsia apewe adhabu kupitia Kamati ya Maadili ambayo inasimamia uchaguzi na moja kati ya adhabu hizo ziwe strict iwe ni mtu huyo kuenguliwa katika kugombea.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana nae kabisa. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Neema Lugangira.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kumalizia naomba kusisitiza na kuishauri, nashukuru sana naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili.
SPIKA: Ngoja. Mheshimiwa Neema mimi ndiyo naongoza kikao usiwasikilize hao wanakupoteza, kwa sababu mimi sijakuuliza kwa sababu yeye alichofanya hapo amechangia hajakupa wewe taarifa. Mheshimiwa Neema Lugangira malizia mchango wako.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kumalizia napenda kusisitiza na kuishauri Serikali kwamba ilete ile Sheria ya Vyama vya Siasa na iifanyie maboresho ili Msajili wa Vyama vya Siasa aweze kuwa na meno ya kuvisimamia Vyama vya Siasa vyenyewe kutekeleza na kuimarisha na kufikisha usawa wa kijinsia kwenye siasa. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanaweka angalau asilimia fulani ya wagombea katika nafasi zote za uchaguzi kuwa wanawake, pia Vyama vya Siasa viwe vina sera ya usawa wa kijinsia na vilevile katika Sheria ya Uchaguzi iweke wazi adhabu ambazo zitachukuliwa pale ambapo mgombea yeyote mwanamke iwe katika mchakato wa kampeni, uchaguzi na hata baadaye anapofanyiwa aina yoyote ya ukatili wa kijinsia, ikiwemo wa kimtandao ni hatua gani zitachukuliwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)