Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, moja kati ya maeneo ambayo yanahitaji sana kusaidiwa ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwenye maelezo yao kwenye Kamati mbalimbali ambazo wamefika na kwa mujibu wa taarifa ya Kamati yetu ya Bunge inayosimamia Wizara hii ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahitaji ipewe fedha kwa ajili ya kwanza, mafunzo maalum kwenye maeneo ya Uandishi wa Sheria; Pili, kwenye eneo la masuala ya utawala; na Tatu, ni katika eneo la mikataba. Kwamba wanahitaji wapewe fedha kwa ajili ya mafunzo maalum kwenye hayo maeneo matatu niliyoyataja.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nisizungumzie hili la Uandishi wa Sheria na naomba pia nisizungumzie hili la masuala ya utawala, nataka nizungumzie hili la eneo la mikataba.

Mheshimiwa Spika, kutoiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutoipatia fedha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili wataalam wake wakapate mafunzo kwenye eneo hili la mkataba ni gharama kubwa sana kwa nchi yetu. Fedha ambazo walikuwa wameomba Milioni 300, kutokuwapa Milioni 300 ni gharama kubwa sana kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, wakati naendelea kuelezea nitatoa mfano kwa nini ni gharama sana kwa nchi yetu, kwa maana hiyo nimesimama hapa siyo tu kuchangia, lakini kulishawishi Bunge kwamba ni lazima tusimame kidete kuhakikisha kwamba Serikali inapeleka fedha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuwapeleka Wataalam wetu wajifunze mambo ya mikataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusipo-train watu wetu kwenye eneo hili la mikataba nchi yetu itashindwa kunufaika na rasilimali tulizonazo. Hivi sasa kama Taifa tunajielekeza kwenda kuwekeza kwenye LNG, tunajielekeza kwenda kuwekeza kwenye Uchumi wa Blue ambao ni Uchumi wa Bahari. Kote huku tutatakiwa kuingia mikataba mbalimbali, tusipoiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Sheria, tutaishia kuwa watazamaji na rasilimali zetu hatutanufaika nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu ili niijenge hoja yangu vizuri na Bunge hili liweze kunielewa kwa nini nasisitiza tupeleke fedha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Milioni 300 iliyokuwa imeombwa na majibu ya Serikali yamekuwa tu ni mepesi, eti ukomo wa bajeti umefikia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano ninaotaka kuutoa ni kwamba, majuzi Serikali yetu iliingia mkataba na kampuni ya Baker Botts ya Uingereza kwa ajili ya kutusaidia ile Government Negotiation Team itakayopatikana, kwenye hili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi kuwa Mkuu wa Government Negotiation Teams ambazo zitakuwa zinatengenezwa. Sasa kampuni hii ya Baker Botts ikitufanyia kazi kwa miaka miwili tunailipa Dola Milioni Tatu na Nusu hiyo ni takriban Bilioni Nane ya kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafanya hivyo kwa gharama tu ya kushindwa ku-train watu wetu! Umeombwa Milioni 300 unashindwa ku-allocate, halafu uko willing kulipa Bilioni Nane kwa kampuni moja kwa mkataba mmoja, this is ridiculous. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaingia mkataba wa aina hiyo tukiwa na facts hizi zifuatazo: Nchi yetu ina Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali toka mwaka 1961 miaka 60 sasa; Nchi yetu imeshakuwa na Geology Department kwenye University of Dar es Salaam toka mwaka 1974 which means tuna wataalam wa geology, tuna wataalam wa mambo ya Oil and Gas na ambao pengine hawapo nchini kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, nilibahatika wakati mmoja kwenda Texas - Marekani nikakutana na Watanzania wengi sana wenye utaalam wa mambo ya Gas and Oil, sasa tunapoingia mikataba hii halafu kwa kisingizio tu cha kusema eti hatuna wataalam! Tusiwe tunajiangalia kwenye Wizara za Serikali kwamba kama hatuna mtaalam ndiyo tuna- assume nchi nzima haina wataalam. Tujengeni utamaduni wa kuwatumia watanzania wenzetu ambao wana ujuzi hata kama wako nje ya nchi, we can access them! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea haya tumeingia mkataba huu tukiwa na TPDC, Shirika ambalo lina wataalam wa Oil and Gas, Shirika lipo toka mwaka 1969, lina miaka 53 tunaongelea jambo hili tukiwa tunayo Faculty of Law ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo ilianza hata chuo chenyewe kabla hakijaanza mwaka 1961, ina miaka 61.

Mheshimiwa Spika, wataalam wote hawa tunao wamefika mpaka level ya PhD, eti leo kwenye mkataba Watanzania hatuwezi kusimama kusema mpaka tutafute mtu atusemee, atufundishe cha kusema, atufundishe ku-negotiate, ilihali tuna wataalam wa kwetu! Tunalipa fedha halafu tumeacha kupeleka halafu tumeacha kupeleka bajeti kwa wataalam wetu kuwa-enhance what is this? Tumuungeni mkono Mheshimiwa Rais yeye ameshaonyesha njia nasi wasaidizi wake twendeni tumuunge mkono.

Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapa, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)