Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili namimi niweze kuchangia machache katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Kabla sijaenda katika mchango wangu wa leo, naomba nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri Mheshimiwa AG pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kazi nzuri kwa kweli ambayo wanaifanya. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, nimeshiriki katika ziara kwenda kukagua miradi ya maendeleo iliyopo chini ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba kwa macho yangu nimeona value of money na nichukue nafasi hii kuwapongeza kwamba fedha ambazo zimetengwa, hakika Mahakama wamezitendea haki na value for money inaonekana kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo sasa, niende kwenye mchango wangu ambao utakijita kwenye Fungu namba 55 kwa maana ya Tume ya Haki za Binadamu. Tume ya Haki za Binadamu ndicho chombo pekee ambacho kimeundwa na Serikali ili kuhakikisha kinalinda, kinasimamia haki zote za binadamu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa lugha nyingine ikiwa kuna namna yoyote ya haki za binadamu kutokufuatwa au kuvunjwa, nchi haiwezi kuwa katika hali ya usalama. Nayasema haya ili kuonesha namna gani ambavyo chombo hiki au Tume hii ya Haki za Binadamu ni chombo muhimu sana, lakini kwa masikitiko makubwa sana niseme Tume hii imekuwa ni Tume mfu. Nayasema haya na niliyasema hata ndani ya Kamati yangu ya Katiba na Sheria, nikasema Tume hii ni Tume ambayo imekuwa ikionekana au naweza nikasema imekuwa ikifufuka wakati wa bajeti kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tume hii haisikiki kabisa huko kwa wananchi ambapo inapaswa kusikika. Tume hii imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi ambao umeidhinishwa au ni jukumu lake la kimsingi kikatiba kuhakikisha wanasimamia na wanalinda haki za binadamu zisivunjwe. Pamoja na majukumu mengine Tume hii ina wajibu wa kutembelea katika magereza, kutembea shuleni, kutembea katika vituo vya Polisi kuhakikisha wanalinda na wakati wanalinda wanaangalia, je, haki za Watanzania zinalindwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba Tume hii haifanyi kazi na naweza kusema kwamba haifanyi kazi kabisa kwa sababu hatuisikii. Nayasema hayo kwamba ni mfu, ukiangalia bajeti ya mwaka wa fedha ya maendeleo ya mwaka 2021/ 2022, bajeti ya maendeleo ilitengwa Sh.373,000,000 tu na fedha hizi hazitokani na mapato ya ndani, ni fedha ambazo zinatoka kwa donors. Sasa inasikitisha kwamba haki za watu wetu zinalindwa na watu wa kutoka nje, yaani Serikali haioni kama ina wajibu wa kutenga bajeti tena bajeti ya kutosha kuhakikisha Tume hii sasa inakwenda kufanya kazi yake kwa uaminifu, kwa uadilifu, lakini pasipokuwa na kikwazo cha bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Dar es Salaam tukihesabu kuna shule ngapi, tukihesabu kuna vituo vya Polisi vingapi, tukayahesabu na magereza ukiangalia hii bajeti ya Sh.373,000,000 haiwezi kutosha hata kwa mkoa mmoja! Kama kweli Tume inafanya kazi fedha hizi sio tu kwamba hazitoshi nchi nzima hata mkoa mmoja hazitoshi. Hata hivyo, kuonesha kwamba Tume hii ni mfu mwaka huu wa bajeti imetengwa Sh.260,000,000 tu na hizi fedha ni kutoka nje, hakuna mpango mkakati wa Serikali kuona umuhimu wa kulinda haki za watu wake au wananchi wake ni mpaka tusaidiwe na donors kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza inawezekana kweli umezaa mtoto, mtoto wako unampenda sana, unalala naye nyumba moja mlango haufungi, unategemea jirani aje kumfungia mlango mtoto wako na bado unaamini mtoto wako yupo salama, ni jambo ambalo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuonesha namna gani ambavyo Tume hii ya Haki za Binadamu ni mfu na huwa inafufuka wakati wa bajeti kama hii, tunafahamu, tunatambua kwamba yamekuwepo matukio mbalimbali ya watu kutekwa, watu kuuawa na wengine mpaka leo hawajawahi kuonekana, mfano wa Azory Gwanda, Mfano Benny Saa Nane, alitekwa mpaka leo hajaonekana, hatukuwahi kusikia Tume hii ikisimama kutekeleza wajibu wake wa kukemea, wa kulaani na hata kushtaki angalau taasisi au watu wanaosadikiwa kwamba walishiriki katika uvunjaji wa haki za binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sio tu hilo lakini wapo Watanzania wenzetu ambao walitekwa lakini wakapatikana, yaani mtu anatekwa halafu anarudi, ana uwezo wa kuelezea wapi alikuwepo nani alimkamata, kilikwenda kilirudi, watu hao wakaonekana, mfano Mo Dewji, lakini tunaye mwingine Roma Mkatoliki, walitekwa wakarudi wakapatikana, Tume hii haijawahi kusikika inalaani, haijawahi kusikika angalau inatoa tamko au basi angalau kufuatilia hata kwenda kufungua kesi, kwa sababu ni wajibu wa Tume hii inapobidi kufungua kesi against taasisi au mtu ambaye inasemekana amefanya uvunjifu wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine kuonesha kwamba hii ni Tume mfu, hivi karibuni yametokea matukio makubwa katika Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Tanga, Jeshi la Polisi linatuhumiwa kuua Watanzania. Ni kiongozi wa nchi Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye alisimama juu ya mlima akapiga kelele, kwanza akalaani, akakemea na akatoa maelekezo nini kifanyike kwa ajili ya uvunjwaji wa haki za binadamu, lakini Tume hii ambayo leo hii ipo hapa inahitaji tupitishe bajeti iko kimya imekufa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)