Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Dr. Eliezer Mbuki Feleshi

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuendelea kuhudumu kwa nafasi ambazo amependa tuendelee kuwemo humu kuwahudumia Watanzania. Nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mahsusi kwa leo kwa jinsi ambavyo anasimamia utawala wa sheria na utawala bora. Pia nikushukuru sana wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti na uongozi wote wa Bunge kwa kuhakikisha kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatimiza wajibu wake kwa Katiba na kwa mujibu wa kanuni ambazo zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri, Mawaziri wengine waliopo hapa pamoja na watendaji wote Serikalini. Nimshukuru Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na viongozi wote ambao kwa upande wa Serikali wanahakikisha kwamba haki inatendeka kwa mujibu wa Katiba. Aidha, niishukuru Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge pamoja na Kamati ya Bajeti ambazo nimekuwa nikifanya nazo kazi kwa jinsi ambavyo zimekuwa zikichakata mambo mbalimbali na kuhakikisha kwamba Bunge lako pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi yangu na wengine, zinatekeleza wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitatenda haki nisipoishukuru sana Ofisi yangu kwa kuanza na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Watumishi wote kwa jinsi ambavyo wao kama sehemu ya Wizara ambayo inaratibu mashauri yote kwa mujibu wa instrument ya Wizara wanasaidia kuhakikisha kwamba shughuli hizi zinaendelea na kwa shukrani niwashukuru sana Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utakumbuka nilitoa dakika 15 za mwanzo kabla ya Bunge kuanza na dakika 15 baada ya Bunge kuahirishwa, kuingia Bungeni kusikiliza Wabunge walio na kero zao ambao huenda wanahitaji kuongea na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mwakilishi wa Ofisi kuu ya Utumishi wa Umma upande wa Sheria. Niwashukuru wengi wamekuwa wakiniona na nimeendelea kutimiza wajibu wangu kwa kufanya nao kazi kwa karibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hoja na michango iliyowasilishwa katika Bunge hili na Wabunge wachangiaji ambao wote tunawashukuru sana, labda kiasi nichangie hili, kuna hoja imetolewa na Mheshimiwa Luhaga Mpina kuhusiana na usiri wa mikataba.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mpina ameeleza kwamba ana maelezo mengi zaidi ya yale ambayo ameyasema hapa na nashawishika na kumwomba hata Waziri wangu wa Katiba na Sheria, yawezekana tunahitaji kukaa naye na kujifunza mambo mengi sana ambayo huenda hayapati fursa ya kushughulikiwa kwenye michakato ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapoongelea masuala ya mikataba, mikataba yote inayofuata sheria inaongozwa na sheria na kwa ushiriki wa Bunge hili Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, wote mnajua kabisa kwamba Bunge hili kwa Mujibu wa Ibara 63(2) na (3) ninao wajibu mahsusi kwa mambo yanayohusu mikataba. Wajibu wa kwanza ni ule wa mikataba ambayo inatakiwa kuridhiwa na Bunge hili ambayo ni kwa mujibu wa Ibara 63(3)(e). Sijaona kama kuna lalamiko kwamba kuna mikataba ya kuletwa hapa haijaletwa. Kwa hiyo mchango wangu ni kwamba Ofisi yangu itaendelea kuhakikisha kwa wajibu wake kwamba Mikataba ya kuletwa kuwasilishwa Bungeni hapa kuridhiwa na Bunge hili itaridhiwa na Bunge kwa kufuata matakwa ya Katiba na Sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa wajibu wa Bunge kusimamia Serikali niamini kwamba Kamati za Bunge hili Tukufu ambazo zipo zinasimamia Wizara na kila Sekta ya Serikali na zinao wajibu kutembelea maeneo miradi iliko ambapo naamini kazi zinazoendelea kule ni pamoja na kufuata matakwa ya mikataba iliko. Kwa hiyo niamini kwamba Bunge hili na Kamati zake vile vile itaendelea kuhakikisha kwamba zile Kamati zinapewa fursa ya kuwianisha miradi iliyopo na mikataba inayohusika na naelewa katika mwaka wa kazi kuna kikao mahsusi ambacho kama sikosei ni kikao cha mwezi wa Tisa ambapo Serikali huwa inakuja na shughuli za Serikali Bungeni, lakini kikao kinachofuata ambacho ni cha mwezi wa Kumi na Moja ni Kamati za Bunge kuja kufanya mawasilisho ya shughuli ambazo zimeangalia utendaji wa kazi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hilo naamini kwamba kama zile Kamati za Bunge zinazosimamia maeneo ya utendaji wa Serikali kuliko na mikataba hiyo zimenyimwa fursa ya kujua mikataba hiyo ina nini, ukiachilia ile ya kuleta hapa Bungeni, basi tupo tayari kama Serikali kupokea hoja kama kuna ukiukwaji huo kuushughulikia, lakini kwa mapendekezo ya Mikataba, ni wajibu wetu kuendelea kujenga uwezo kama Serikali kuhakikisha kwamba tunao uwezo wa kufanya majadiliano na kama mnavyofahamu ile Kamati ya Serikali inayoshughulika na mradi wa LNG jana ilikuwa kwenye ziara mojawapo. Serikali haipo tupu sana kwa maana ya wataalam, lakini wajibu wetu ni kuendelea kuhakikisha kwamba Serikali yetu inao uwezo wa kutosha kuhakikisha kwamba kadri kunapokuwa na uwekezaji mkubwa basi wataalam wetu wote kutoka sekta mbalimbali wanahusishwa pamoja na kushughulika kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, lakini faraja yangu mara nyingi wanapenda kudadisi, Bungeni humu kuna Wanasheria zaidi ya 30 na hawa wote nimeshawakaribisha kuwa sehemu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mambo yote ambayo wataona wanahitaji maboresho, wote tunaijua tasnia ya sheria sio maneno matupu. Tasnia ya sheria inaongozwa na uhalisia na baadaye uhalisia kutokana na mambo yanayoibuka, basi wote tunakuwa na ile collective responsibility na hata kuona maeneo yapi ambayo yanahitaji kuboresha sheria zetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa muda ulionipatia na naunga mkono hoja ya Waziri wa Katiba na Sheria. (Makofi)