Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kushukuru sana kwa kupata fursa ya kuweza kuchangia na kutoa mchango wangu wa mawazo kwenye Wizara hii ya Madini. Nitajielekeza kwenye maeneo matatu; moja, kwenye dhana ya kuhamisha madini ya tanzanite kwenda Mererani; pili, changamoto zake halafu; na tatu, kwenye mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhana nzima ya kuondoa madini ya tanzanite na kutaka yauzwe Mererani peke yake inahusisha maeneo mawili. Eneo la kwanza, utoroshaji na kwenye utoroshaji wa madini sina mashaka kabisa kwa sababu kwenye eneo la Mererani ambako Serikali imejenga ukuta ndio eneo ambalo kuna ulinzi wa uhakika, kuna vyombo vyote vya ulinzi na usalama, kuna Jeshi la Wananchi, kuna Usalama wa Taifa, kuna TAKUKURU, kuna Polisi na kuna Wizara yenyewe ya Madini. Kwa hiyo, dhana ya utoroshaji na changamoto hiyo kwa muktadha wa Mererani haipo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasi hatutaki madini haya yauzwe Arusha peke yake, tunataka yauzwe Mererani, Arusha, Mwanza, Zanzibar na kwenye masoko yote ambayo yapo kwa mujibu wa sheria ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa changamoto; tuna changamoto ambazo tumezipata kutokana na maamuzi hayo ya Serikali. Changamoto ya kwanza, mapato ya Serikali yameshuka. Kabla ya maamuzi haya, kipindi kama hiki tulikuwa tunapata kiasi cha Shilingi bilioni 1.3 kwenye Soko la Madini la Arusha. Hiyo ni kwa madini yote, lakini kwa Tanzanite peke yake ilikuwa ni shilingi milioni 800. Leo tumepeleka Mererani kipindi kama hicho tunapata shilingi milioni 339. Kwa hiyo, changamoto ya kwanza Serikali imepata hasara, tumepoteza mapato.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya pili, katika Soko la Madini la Arusha, tuna maeneo kama NSSF, PSSF na AICC ambayo ni majengo ya Serikali. Serikali ilikuwa inapata kodi kupitia wafanyabiashara ya madini, ambapo kwa mwezi tulikuwa tunapata shilingi milioni 128. Hadi kipindi cha sasa tumepotezza kiasi cha shilingi bilioni 1.152 ya pango kwenye taasisi hizi za Serikali. Kwa hiyo, unaona maamuzi haya tuliyoyafanya yametuletea changamoto kubwa ya kukosa mapato kwa pande zote.

Mheshimiwa Spika, pia tuna changamoto kwenye upande wa ajira. Tumekosa ajira 403 kwa wale ambao wote ambao walikuwa wanafanya biashara hizo kwenye masoko yetu ambayo yapo hapa. Tumepata changamoto kwa ma- broker wetu; ma-broker 2,500 mpaka 300 wamepata changamoto kubwa sana kwa sababu asilimia karibu 80 ya madini yanayouzwa kwenye masoko ya Arusha yanatokana na Tanzanite.

Mheshimiwa Spika, pia tulikuwa na mashine 427 kwenye Soko la Madini la Arusha, sasa hivi Mererani zimekwenda mashine 48 tu ambayo ni sawa sawa na asilimia kama 11.24. Kwa hiyo, unaona mashine ambazo zimebaki hazitumiki watu wamekosa ajira kwenye maeneo hayo, lakini pia na changamoto nyingine nyingi kwa mapana yake.

Mheshimiwa Spika, kutaka tu madini ya Tanzanite yauzwe Mererani peke yake, una-monopolize soko lenyewe, inasababisha kushuka kwa thamani, kwa sababu kunakuwa hakuna ushindani. Leo ukiuza madini Mererani, ukiuza Arusha, ukiuza Mwanza, ukiuza Zanzibar na maeneo mengine ya Tanzania, itasaidia sana kwa wafanyabiashara hao kushindana kutafuta wanunuzi nje ya nchi na mwisho wa siku faida itakuwa ni kubwa zaidi na mapato pia yataweza kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, pia kitendo cha kuruhusu wageni kutoka nje ya nchi kwenda moja kwa moja Mererani kununua madini, kwanza ni hatari kwa usalama wa nchi yetu, lakini pia inaondoa fursa kwa watu mbalimbali walio katika nchi ya Tanzania kuweza kunufaika na madini hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, nilikuwa na mapendekezo yafuatayo kwa Wizara yetu ya Madini na Serikali kwa ujumla. La kwanza, sisi hatuna tatizo kabisa, tunataka Serikali ikusanye kodi na tunataka kodi zote zilipwe pale Mererani; walipe kama ni mrabaha, inspection fee, baada ya kulipa kama ambavyo wanaruhusiwa leo, wakishalipa wapeleke madini yao India, Marekani na maeneo mengine, waruhusiwe pia kupeleka na Tanzania kwa sababu ni sehemu ya dunia ambayo inachanganya Arusha, Mwanza, Zanzibar, na Mererani kwenyewe.

Mheshimiwa Spika, tunao mfano, tuna madini kama haya yanaitwa pink ruby ambayo yanapatikana kule Thailand peke yake. Madini haya yanayopatikana kule pamoja…

(Hapa kengele ililila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, naamini hiyo ni kengele ya kwanza.

SPIKA: Kengele ni moja tu. Malizia sentensi yako.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, tunaamini kwamba madini haya yakiruhusiwa kuuzwa kwenye masoko mbalimbali itatusaidia sana.

Kwanza yatatoka kwa mchimbaji, yatakwenda kwa broker, baadaye yatakwenda kwa dealer na baada ya hapo yataongeza mzunguko ndani ya nchi yetu na pia yatafika huko duniani.

Mheshimiwa Spika, pia tunaomba…

SPIKA: Ahsante sana. Muda wako umeisha.

MHE. MRISHO M. GAMBO: …tuweze pia kuanzisha maonesho ya madini, ili madini yetu haya ya Tanzanite na madini mengine tuwe na maonesho yake pale Arusha, dunia nzima iweze kuyaona, na mwisho wa siku iweze kutusaidia kuitangaza Tanzania, na kuleta watalii ndani ya nchi yetu. (Makofi)