Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza kabisa niende moja kwa moja kutokana na muda na nikuombe ikikupendeza basi unaweza kuniongeza dakika tatu ili niweze kuwasilisha hoja mahsusi.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya, pia nimpongeze Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakiri kwamba Mheshimiwa Waziri huyu anafanya kazi kubwa sana akisaidiwa na Naibu Waziri wake, na viongozi wote wa Tume pamoja na Wizara wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nijikite kwenye ukurasa wa 32 ambapo Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amezungumzia juu ya suala zima la CSR. Nitajikita kwenye suala zima la CSR lakini nitajikita kwenye suala zima la local content na nitajikita kwenye suala zima la fidia ambazo zinaendele kwenye maeneo ambayo tunatoka kwenye migodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgodi wa Bulyanhulu ni mgodi unaopatikana katika Halmashauri ya Msalala, mgodi huu au maeneo haya ni maeneo ambayo yanachangia kiasi kikubwa kwenye Pato la Taifa hapa Tanzania. Mheshimiwa Waziri ametuambia hapa ni takribani zaidi ya Shilingi Bilioni 16 ambazo zimetolewa kama fedha ya CSR katika maeneo yetu na Msalala ikiwemo.

Mheshimiwa Spika, niseme tuna mgodi pale unaitwa Bulyankhulu, mgodi huu upo katika Jimbo langu la Msalala pia mgodi huu upo katika Jimbo la Mheshimiwa Waitara. ninakiri kwamba mgodi huu umeendelea kutumia fedha vibaya za CSR ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Geita wanapokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kama fedha ya CSR lakini Bulyankhulu na North Mara, Bulyankhulu tunapokea Bilioni 2.5 tu fedha ya CSR. Leo Mheshimiwa Waziri amezungumzia hapa kwamba fedha hizi zimeenda kujenga barabara, zimeenda kusambaza maji, zimeenda kujenga miundombinu ya elimu. Nikuhakikishie katika Jimbo langu la Msalala ambapo makinikia mengi yanachimbwa barabara hakuna.

Mheshimiwa Spika, utaona malori na Malori ya makinikia yakisafirishwa, vumbi kali wananchi wanapata taabu lakini hakuna tunachonufaika juu ya uwepo wa barabara. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, kama ni taarifa nilinde utaniongezea dakika.

SPIKA: Muda hauongezeki nadhani tulishaambiana humu ndani, muda wa taarifa ni wewe unaongezewa kwenye mchango wako Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba nataka kumwambia mchangiaji kwamba katika hiyo CSR ya mgodi huo wa Barrick walitakiwa watengeneze barabara ya lami inaanzia hapo Kakola inakuja mpaka Busisi hawajatekeleza hilo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2000 na 2003 mgodi ya Bulyankhulu uli-declare kwamba ulitumia kaisi cha Shilingi Bilioni 50 kwenye miradi ya maendeleo kwenye maeneo yale, walitumia fedha zilezile za CSR kujenga nyumba za watumishi Bugarama na Ilogi.

Mheshimiwa Spika, TRA waliwasamehe kodiā€¦

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge muda wenyewe wa kuchangia ni mfupi sana kwa Mbunge sasa taarifa zikiwa nyingi yeye mwenyewe atakuwa hamalizi, Mheshimiwa Waitara.

T A A R I F A

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kule Nyam ongo waliahidi kujenga Chuo cha VETA chenye hadhi ya Wilaya tangu mwaka 1995, hawajajenga mpaka leo. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo nikuombe uniongezee dakika tano. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, walitumia fedha za CSR kujenga nyumba za wafanyakazi na waka-declare fedha zile kwamba wametumia kwenye kujenga miradi ya maendeleo, lakini cha kushangaza nyumba zile walianza kuuziwa tena watumishi na zile fedha hatujui mpaka leo zimeenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgodi huo wa Bulyankhulu umekuwa ukilalamikiwa kila kona na tukisema hapa tunaambiwa jambo moja tu, kwamba mkisema mwekezaji huyu mkubwa tutakuwa blacklisted. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunasema wananchi wa Jimbo la Msalala hasa Bulyankhulu, hatuko tayari kupata manyanyaso haya yanayoendelea kwa hofu ya kwamba tutafungiwa. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge lakini nafikiri hoja yako imeeleweka na Mheshimiwa Waziri ni muhimu, nafahamu sheria inaweka mwongozo lakini ni muhimu ninyi kama Wizara kufuatilia hizi fedha zinazotolewa zinafanya kazi gani, kwa sababu bila kuwa mnafahamu zinafanya kazi gani ndiyo hivyo mtu anaamua kupeleka kule anakotaka yeye na siko kule wananchi wanakotaka fedha zipelekwe. (Makofi)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.