Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi hii kuhitimisha hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini Mwaka wa Fedha 2022/2023. Wizara imepokea michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameitoa kwa kusema, pia tumepata ushauri na maoni ya mapendekezo kutoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati ya Madini ambayo kwa kweli ni muhimu sana kwetu.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla ushauri na maoni yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni ya msingi sana. Huo ni ushahidi mwingine kuwa Bunge lako ni Bunge ambalo kwa kweli linasimamia maslahi mapana ya wananchi wetu wa Tanzania. Ukiwasikiliza kwa kiwango kikubwa yale wanayoyazungumza ni yale ambayo ama yanaathiri uchimbaji ama biashara yenyewe ya madini na hivyo kufanya sekta hii isikue. Kwa hiyo, tumeyachukua kwa uzito mkubwa na sisi kama Wizara tutaenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, naomba tu nifafanue kwa kifupi hoja mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezielezea. Nieleze kwamba Wizara ya Madini kwa vyovyote vile ili uweze kufanya maendeleo kwenye sekta na kuifanya sekta ikue haiwezi kuwa na monopoly ya mawazo au ya fikra, ni lazima ichukue mawazo ya Waheshimiwa Wabunge, mawazo ya wadau wengine waliomo kwenye sekta na kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mmeona hapa hoja zinazozungumzwa kwa kweli ni zile ambazo zinatufundisha au zinatuelekeza kwenye kuboresha zaidi, zinaweza kuzungumzwa kwa tone tofautitofauti lakini bottom line ya kila hoja iliyosemwa ni kuhakikisha kwamba manufaa ya madini haya yanakuwa kwa Watanzania na kwa nchi yetu na kwakweli ndiyo kiu yetu sisi Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, sasa limezungumzwa eneo la wachimbaji wadogo, nataka nilielezee hilo kwa kifupi tu. Ni kweli kwamba yapo maeneo watu wamepewa leseni na toka wamepewa leseni inawezekana hawafanyi chochote kwa namna ya kuonekana kwa macho, lakini uchimbaji wa madini wenyewe ulivyo si kila atakayepewa leseni leo leo ataanza kuchimba, mwingine ataanza kufanya utafiti, mwingine ataanza kutafuta hizo data na baadaye aanze kuchimba.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie kwamba Wizara ya Madini toka tumeanza kuwapa nguvu wachimbaji wadogo hizo ndizo hatua tunazochukua. Tunapata lawama hapa na pale kwamba tunafuta leseni, ni kwa sababu tunatekeleza maelekezo ya Bunge, lakini tunatekeleza maelekezo ya viongozi wetu kwamba ni lazima wachimbaji wadogo wapewe kipaumbele. Hivi nilivyosimama hapa tumeshafuta zaidi ya leseni mia mbili ambazo ni dormant na zipo nyingine nyingi zaidi ya 400 ambazo zina-default notice, process ya kufuta inaendelea.
Mheshimiwa Spika, process ya kufuta leseni ina lawama nyingi, sisi Wizara ya Madini tumekubali kubeba lawama hiyo kwa niaba ya wachimbaji wadogo, kwa sababu wapo watu wengine ambao ni kweli watashika yale maeneo kufanya udalali, nitakaa na leseni kutegeshea kuona ni nani anakuja. Wengine wanasubiri wachimbaji wadogo waende kwenye hile leseni wachimbe, halafu aseme hapa ni kwangu awaondoe wale wachimbaji wadogo. Nataka niwahakikishie wale wenye leseni kwamba wale ambao wanatekeleza matakwa ya sheria, Wizara tutawalinda lakini wale ambao hawatekelezi matakwa ya kisheria, maeneo hayo tutayachukua tuwapatie wale ambao wanahitaji kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, jambo ambalo limeelezwa hapa kwa uchungu mkubwa ni jambo la CSR. Inawezekana kuna migodi mingine haifanyi vizuri. Nieleze kwa ujumla kwamba migodi mikubwa hii inatekeleza kwa kiwango kikubwa matakwa ya sheria ya kutenga fedha kwa ajili ya CSR. Sasa tunachogombea hapa siyo uwepo wa fedha, tunagombea matumizi ya fedha na nadhani hili ni jambo zuri. Tulikotoka tulikuwa tunagombea uwepo wa fedha zenyewe, sasa hivi hiyo siyo story tena, story ni namna gani hizo fedha zinavyotumika.
Mheshimiwa Spika, Sheria yetu ya Madini, section ya 105 imetoa utaratibu mzuri sana kama ambavyo Mheshimiwa Makamba ameeleza kwamba ni lazima mipango ile ya CSR ipelekwe kwenye Halmashauri. Kazi ya Halmashauri kubwa ya kwanza ni kuthibitisha au ku-approve hiyo mipango. Una- approve kwa kuangalia value for money. Kuna wakati fulani miradi mingine ilikuwa inatekelezwa; mfuko mmoja wa cement unatekelezwa kwa CSR lakini mfuko wa cement unauzwa shilingi 80,000/=. Sasa kama hali ndiyo hiyo, kazi ya Halmashauri ni kuhakikisha kwamba mfuko wa bei ya soko ni huu au bidhaa inayotakiwa kununuliwa kwa ajili ya kutekeleza bei ni hii.
Mheshimiwa Spika, mgodi tuliokuwanao kwenye framework, mgodi ambao CSR yake unaweza kuiona kuanzia day one, ni migodi inayosimamiwa na Twiga, ukiwemo Mgodi wa Bulyanhulu pamoja na Mgodi wa North Mara. Hii CSR yake iko packed kwenye uzalishaji wa dhahabu. Kila wakia moja ya dhahabu unachukua dola sita unaziweka pembeni kwa ajili ya CSR.
Mheshimiwa Spika, hata North Mara, tunavyozumza, fedha zipo Shilingi bilioni 5,600 hazijafanyiwa kazi. Kuna Shilingi bilioni moja nyingine ya mwaka 2021 ipo haijafanyiwa kazi. Kinachotokea ni kwamba kuna matatizo ya usimamizi wa fedha za CSR. Kwa hiyo, kuna wakati mwingine tunafanya auditing, tunachukua muda mrefu na auditing hizo wanaoumia siyo sisi, ni wananchi, lakini kuja kumlaumu mgodi kama mtu ambaye hajatoa hizo fedha, na penyewe kwa kweli tuwatendee haki kidogo. fedha hizi wao wamezitoa na tayari ziko kwenye utaratibu wa kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, hata kule Bulyanhulu, tunazungumza kujenga barabara; ni kweli, mgodi umeshatenga Dola za Kimarekani milioni 40; na barabara ambayo tunabishana, tujenge kutokea Mwanza kuja Kakola au kutokea Kakola kwenda Kahama, hilo ndiyo bado tunabishana. Ila kazi ya mgodi, tayari hela zake ameshatenga, anasubiri uamuzi wetu wenyewe.
Nawaomba wale wote tuliopewa wajibu wa kusimamia mambo haya, tufanye haya mambo kwa haraka ili huduma zipatikane kwa wananchi ili imani ya wananchi kwamba sekta hii inawasaidia kwenye maisha yao iweze kupatikana.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, nami nisingependa kuchukua muda mrefu, ni jambo lililozungumzwa kuhusiana na Merelani. Nimesikia concern ya Waheshimiwa Wabunge, lakini lazima tukubali, maeneo mengi yanayochimbwa madini, watu wamebadilisha maisha yao. Ukienda Mahenge, kabla hatujapasimamia vizuri na leo hali yake ni tofauti; ukienda Geita hali ni tofauti, ukienda Kahama hali ni tofauti, lakini bila kuficha Mererani hali yake ni tofauti sana.
Mheshimiwa Spika, hali ya Mererani ni mahali pa ukiwa. Watu wana hali ngumu, lakini watu wanapishana na magari, wanakuja Mererani, wanaondoka. Ndiyo Serikali ikaja na utaratibu kwamba tuongeze manufaa kwa kujenga soko Mererani. Nafurahi kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya kujenga lile soko ni Shilingi bilioni tano na bilioni moja imeshatolewa kwa ajili ya kujenga lile soko.
Mheshimiwa Spika, yako matatizo tutakutana nayo kwenye kutekeleza, ni kwamba ni kweli pengine biashara itashuka, kutakuwa na turbulence ya hapa na pale, isituvunje moyo. Kazi yetu kama Serikali, yale yote aliyosema hata Mheshimiwa Gambo na Wabunge wengine wa Manyara, tutayaangalia yote kwa ujumla wake, tuje na utaratibu mzuri zaidi ambao utafanya sekta hii iweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie la mwisho kabisa kwamba, katika uchimbaji madini wanawake wamechangamkia fursa sana. Naomba nichukue nafasi hii niwapongeze sana wanawake wa Tanzania na ndiyo wamekuwa walipa kodi wakubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Wizara tumeona hiyo ni fursa ya kuwatumia wanawake kwenye sekta ya madini. Tunataka tuwahamishe wanawake kwenye utoaji wa huduma kwenye midogo waende kwenye utendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi hii hatuwezi kuifanya wenyewe, tunahitaji Waheshimiwa Wabunge na wenyewe watusaidie. Kwa msingi huo, Wizara tumekaa, na tumeona kwamba tunahitaji tupate ma-champion Wabunge wanawake watakaotusaidia kuhamasisha wanawake wengine kushiriki kwenye uchumi wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo tunaomba Waheshimiwa Wabunge wafuatao watukubalie, watusaidie kwenye jambo hili; Mheshimiwa Munde Tambwe, Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Janejelly Ntate James na Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga. Hawa wawe mabalozi wa wachimbaji madini wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. Naomba Bunge likubali kutupitishia makadirio ya fedha tulizoomba ili tukafanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naafiki.