Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na EFD machine; EFD machine ni chombo ambacho kinasaidia Serikali kukusanya mapato. Pamoja na umuhimu wa chombo hiki bado utaratibu wake unavyotolewa mfanyabiashara mwenye mtaji wa shilingi 600,000 akanunue mashine yenye thamani ya shilingi 800,000; mfanyabiashara mwenye mtaji wa shilingi 800,000 na kuendelea mpaka shilingi milioni 10, shilingi milioni 20 mpaka shilingi milioni 200 ukiangalia utaratibu wa hii bei ya mashine haumsaidii mfanyabiashara mdogo. Kama mashine hii inasaidia Serikali kukusanya mapato, ni kwa nini Serikali, isitoe mashine hizi bure kwa wafanyabiashara ili zisaidie kukusanya mapato kwenye Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa hii mashine unaonekana tu pale ambapo mfanyabiashara mkubwa ana uhakika wa kufanya biashara zake. Huyu mfanyabiashara mdogo leo hata anayetamani kuisaidia nchi hii kulipa kodi anaangalia mtaji wake wa ahilingi 600,000 halafu mashine ya ahilingi 800,000 nani anaweza kufanya hivyo biashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, badala ya kuisaidia Taifa tunapoteza mapato kwa jambo ambalo linawezekana tu kukaa mezani, kuwe na utaratibu mzuri wa utolewaji wa hizi mashine na kulingana na umuhimu wake wa kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza kwenye hali ya mitaji ya wafanyabiashara wetu. Hali ya wafanyabiashara mitaji yao imezidi kushuka siku hadi siku, nini kinapelekea mitaji yao inashuka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuna utitiri wa tozo za ajabu na hali hii ikiendelea ina maana maduka yatakwenda kufungwa. Maduka yakifungwa Serikali inakosa mapato, lakini pia tunapoteza ajira za vijana wetu ambao kwa sasa ni changamoto kwenye Taifa letu. Ni wakati wa Serikali kuchukua hatua kabla biashara hizi hazijafungwa, tusirudi huko tulikotoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza hapa badala ya sisi kuuza zaidi nje ya nchi, tunauza kwa asilimia 14 lakini tunaagiza kwa asilimia 87. Lazima tujue tunahitaji nini, sisi hitaji letu kama Taifa tunahitaji kuuza zaidi kuliko kununua kuleta kwenye Taifa letu. Kuna haja sasa aidha, kubadilisha mitizamo ya wataalam wetu kwenye Wizara hii, ianze kufikiri kwamba Wizara hii ni kiini cha kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waache kufikiri haya ambayo tunafikiri leo kwenye hii asilimia nane inayochangia kwenye Pato la Taifa. Tuanze kufikiri asilimia 26 ili tufike kwenye asilimia 26 ni lazima kubadilisha mtizamo waanze kufikiri nje ya box namna ya kulikomboa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati hapa tunazungumza mfumuko wa bei, mfumuko wa bei hauwezi kudhibitiwa kwa mtutu wala polisi, unahitaji fikra makini na uzalendo wa nchi hii. Tunahitaji leo tunapozungumza hapa bidhaa zikipatikana kwa wingi huwezi kutumia nguvu kudhibiti mfumuko wa bei. Bidhaa zikipatikana kwa bei ambayo ni rafiki kwa wananchi huwezi kutumia nguvu, huwezi kutumia mtutu, kila kitu kinakuja automatically. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunazungumza mfumuko wa bei ukiangalia bei tu ya mafuta ya kula kwa nini Serikali isitumie taasisi zake. Leo tunapozungumza hapa Magereza wana maeneo makubwa kuliko yale ambayo wanayatumia. Kwa nini Serikali isiwekeze huko kwenye taasisi zake ikiwemo Magereza na JKT, ikapeleka mbegu nzuri, wakawapa vifaa vya kisasa, ni mwaka mmoja tutakuwa tunazungumza ni namna gani tunaweza kuuza nje ya nchi badala ya kufikiri leo kutoa nje kuleta ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo tu Gereza la Kitete, Wilaya ya Nkasi wale watu wanaweza kuzalisha alizeti, alizeti hiyo ukitoka hapo utakwenda kwenye Gereza lingine lipo Mpanda peke yao tu kwa maeneo ambayo yako nje hawazalishi na maeneo yapo na zile ni taasisi zenu tunahitaji Malaika Gabriel kwenye jambo hilo? (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji uthubutu tu wa viongozi mliopewa dhamana leo na mimi niwaambie hakuna majibu mepesi kwenye mambo magumu. Tunajua kuna vita inaendelea imetuathiri, lakini unapopewa mamlaka hawamaanishi kwamba utapita kwenye kipindi kizuri tu na huu ndio muda wa kupimana uwezo wetu wa kuongoza Taifa kwenye mambo magumu kama haya. Hatutakuja tunasema unajua vita, ndio vita ipo, lakini onesha uwezo wako uliyepewa dhamana. Haya mafuta leo tutakwenda kwa wafanyabiashara kuwadhibiti, tukiwadhibiti wafanyabiashara, msifikiri ile athari ni ya wafanyabiashara inakwenda kuathiri wananchi moja kwa moja mpaka wa kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali pamoja na hatua zenu ambazo mnazichukua, tunahitaji kuonesha uwezo wa kutosha wa kuwakomboa Watanzania wanaoathirika leo. Kama ardhi tunazo mikopo tumeweza kufanya vizuri na mimi ninampongeza Mheshimiwa Rais kwenye jambo hili na ninyi ambao mmepewa dhamana mshaurini vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tumechukua mikopo kwa ajili ya Covid tukajenga madarasa, nini kinapelekea leo tushindwe kudhibiti mfumuko wa bei huu ambao unaendelea pamoja na changamoto nyingine zinazoendelea?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa mimi niwaombe Mawaziri ambao mmepewa dhamana ya kumshauri vizuri Mheshimiwa Rais, mumshauri vyema kwa kuangalia uhalisia namna ambavyo Watanzania wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hili jambo naomba Wizara ya Kilimo na Wizara hii ninyi ni Wizara pacha, kwa hali ya kawaida kuna mambo ambayo yanawezekana kabisa, mkitanguliza uzalendo sio uzalendo wa kuvaa tai yenye nembo ya Serikali, tunataka uzalendo wa vitendo wa kusaidia Taifa hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo yanaumiza sana, kwa hali ya kawaida mimi ninaamini mfumuko wa bei ambao leo unawaathiri Watanzania mtu yeyote aliyepo humu ndani na anayejua amechaguliwa na Watanzania, kuna haja sasa ya kuangalia ni namna gani pamoja na kwamba tutakuwa na udhibiti wa muda mfupi, lakini lazima tuwe na utaratibu mzuri kama Taifa. (Makofi)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba tayari Serikali kupitia Waziri Mkuu wameshatoa maelekezo, kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nchini kote kwenda kudhibiti na kuangalia mfumuko wa bei katika maeneo yetu huko. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aida taarifa hiyo umeipokea?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa zake hizo ambazo amezitoa mimi sizipokei.

NAIBU SPIKA: Endelea na mchango wako.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa sababu tunazungumza mambo ambayo ni serious, ni vizuri tukajua haya mambo kwamba yanawaathiri wananchi waliotuleta hapa ndani ya Bunge hili. Hatuhitaji maagizo wala maelekezo, tunahitaji kudhibiti kwa mfumuko wa bei, kama maagizo yanakwenda kuondoa mfumuko wa bei sisi hatuna shida na maagizo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotaka ni mazingira yaliyopo sasa hivi, na mimi nawapongeza Watanzania kwa kuwa wavumilivu kwa mapito ambayo wanapitia. Ni kweli ni tatizo la sisi sote, lakini narudia tena ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani kuhakikisha jambo hili linadhibitiwa, halihitaji nguvu linahitaji uwezo mkubwa wa kufikiri kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninarudia tena hawa mnaowaona sijui panya road, sijui watu gani, ni mazingira haya ambayo yanatokana na hii hali iliyopo sasa hivi. Lazima tushirikiane kwa pamoja na tuieleze Serikali kwa ukweli. Lazima tuje na majibu ambayo tunategemea yataenda kuleta suluhisho kuondoa hali ambayo ipo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo unapozungumza suala la mafuta ya kula, halijatokea leo tu kwa sababu ya vita inayoendelea huko, tumeanza kuzungumza Bunge la mwaka jana hapa, lakini unakuwa unajiuliza shida ni nini? Ni kwa sababu hatuna vipaumbele? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na Mheshimiwa Waziri, slogan ya Awamu ya Tano ilikuwa ni Serikali ya Viwanda. Serikali ni ileile ameondoka…

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)