Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi na mimi pia ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara. Nina masuala kadhaa ya kuzungumza, lakini kubwa zaidi ni suala la ugonjwa wa malaria hapa Tanzania. Ni jambo la Wizara ya Afya, lakini suluhisho la malaria lipo katika Wizara hii ya Viwanda kwa maana tuna kiwanda cha kuzalisha viuwadudu kipo Kibaha (Tanzania Biotech Limited) ambacho kinapaswa kuzalisha dawa zinazoweza kuuwa viuwadudu na kumaliza malaria hapa Tanzania. Hii ni ajenda ya Serikali tangu Serikali ya Awamu ya Nne, Serikali ya Awamu ya Tano na sasa Serikali ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mshabiki au nina interest kubwa kuona kwamba malaria inakuwa zero Tanzania. Tunajadili sana kwenye Kamati masuala haya, lakini ninachokiona kinachotakiwa ni nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha malaria inakuwa sifuri, lakini kwa sasa bado sijaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri nafahamu kwamba Waziri ameingia mpya Mheshimiwa Dkt. Kijaji, yeye ni mgeni. Nina imaninaye kubwa ninaamini anaweza kufanya kitu, lakini pia Wizara ya Afya ina Waziri Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa yuko pale Mheshimiwa Bashungwa, ninaimani nao kubwa sana wao pamoja na wasaidizi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi kiwanda kilijengwa na kimeanza uzalishaji mwaka 2016 kwa ajili ya kuzalisha hiyo dawa iweze kumaliza malaria. Kiwanda uwezo wake wa kuzalisha ni lita milioni sita kwa mwaka, lakini uhitaji wetu ili kumaliza malaria tunahitaji lita milioni tano na laki saba kwa mwaka. Mpango ulikuwa ndani ya miaka mitano Tanzania iwe na malaria free. Kwa hiyo, ukiangalia hapa uzalishaji na uhitaji wa lita milioni tano na laki saba kwa mwaka, maana yake ndani ya miaka mitano tunahitaji lita milioni kama 28 na gharama yake ya jumla ni kama bilioni 330. Kwa hiyo, kimsingi Tanzania haihitaji story nyingi, inahitaji bilioni 330 kufanya malaria sifuri, lakini jitihada ambayo sidhani kama imefanywa kwa ukubwa ambao unastahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hii kwa maana ya hiki kiwanda ambacho tunacho kilikuwa na mikataba miwili, kwa maana ya na taasisi mbili; ya kwanza na Kampuni ya Labio Farm ambao ndio wenye teknolojia ya uzalishaji wa hii dawa ya kule nchini Cuba. Tulikuwa na mikataba nao kama mitatu, wa kwanza watusaidie kujenga kiwanda, tuliweka fedha karibu shilingi bilioni 46 kiwanda kijengwe na kilijengwa pale Kibaha, lakini mkataba wa pili tulikubaliana nao watusaidie ku-transfer technology kwa maana ya kufanya management ya muda mfupi wa kile kiwanda kuwa-train Watanzania waweze kuzalisha dawa na baadaye tuwe free tuendelee kujitegemea. Mkataba wa tatu ulikuwa wa kutumia jina la brand yao, ile dawa ambayo inazalishwa kampuni yetu tutumie brand yao, tumesaini nao mkataba tumekubaliana nao ili tuweze kutumia zile dawa kwa maana kuweza kutumia lile jina kuweza kuuza nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa changamoto zipo kadhaa; kwenye mkataba wa kwanza kwa maana ya ujenzi ulishakamilika, lakini kwenye management, mkataba wa pili ulikuwa kidogo una shida kwa maana wale mabwana wakawa wanafanya management yote ya kwao, wanazalisha dawa kwa ukubwa na udogo ambao walifanya, lakini uuzaji wa dawa kwa asilimia nyingi ile kampuni kwa maana ya Labio Farm walikuwa wanauza wao. Wanauza dawa nje ya nchi na fedha nyingine mpaka leo Serikali tunawadai, kwa maana ya Tanzania inawadai hela wale mabwana wa Cuba, hizo fedha hawajatulipa mpaka leo ambazo wameuza dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia suala lingine ni suala la mkataba wa kutumia jina lao kwa zile dawa. Sioni kama hili jambo lina mantiki kwa sababu lengo letu la kwanza kufanya malaria iwe sifuri Tanzania. Tunashindwa kufanya hili jambo kuna sababu zilikuwa zikisemwa hapa kuna suala la ithibati, Umoja wa Mataifa kwa maana ya WHO hawajatoa ithibati kwa dawa ambazo tunazalisha pale Kibaha na hili jambo mchakato wake umechukua muda mrefu kidogo. Sasa nikawa nawaza unahitaji ithibati ya Umoja wa Mataifa kuuwa viuwadudu kule Nachingwea? Unahitaji WHO ije itupe ithibati ili Malinyi kule malaria iishe? Katika hali ya kawaida haiingii akilini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, mimi jambo hili tumekuwa tumekuwa tukibishana nao muda mrefu na mpaka sasa suing mkono suala la mikataba hiyo ambayo ilikuwa imetokea. (Makofi)

Kwa hiyo, ninachoishauri Serikali management ya sasa ya Watanzania ina uwezo mkubwa, wameshajifunza kutoka Labio Farm wanaweza kuzalisha dawa vijana wetu, wanaweza kufanya hivyo, hilo jambo lifanyike mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kabla ya kuzalisha dawa kwa maana ya kabla ya operation pale kuanza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa maana ya NDC ilisaini mkataba na Wizara ya Afya, ilisaini mkataba na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tarehe 11 Machi, 2015 ili waweze kununua dawa yote ambayo itazalishwa pale. Kwa hiyo, maana yake kiwanda kile hakina haja ya kuhangaika kutafuta wateja, lakini kilisimama muda mrefu kwa kukosa wateja wa kuuza ile dawa ya kumaliza malaria. Wizara ya Afya ndio jukumu lake walisaini kukubaliana na NDC, lakini hawakununua dawa hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unajaribu kuwaza, sitaki kutumia lile neno gumu ambalo huwa anatumia Mheshimiwa Halima, lakini nichukue tu la Mheshimiwa Kirumbe Ng’enda, kweli hii ni busara? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha Serikali, fedha zilizojenga za Serikali, mteja anatakiwa awe Serikali Wizara ya Afya na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, halafu bado hainunui dawa zake yenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kawaida inafikirisha na muda mwingine inatia hasira, lakini sijaona seriousness ya Serikali kwenye kumaliza malaria Tanzania. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)