Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru na mimi kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nifanye rejea kwamba duniani kote na tukiangalia tangu kuanza kwa shughuli ya viwanda duniani katika historia imekuwa inahusishwa na sera ya mambo ya nje, wakati Japan kupitia Waziri wake wa Viwanda na Biashara, na wakati ule kipindi kile cha Marekani zaidi walikuwa wanaangalia Rais anayekuja ana mtizamo gani na katika siasa ya sasa ya mambo ya nje wanaangalia Rais anayekuja ana mtizamo gani na hiyo ina reflect biashara ya nchi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu katika vipindi mbalimbali tumekuwa na marais wetu katika Awamu ya Kwanza mpaka sasa Awamu ya Sita, sote tunajua sera ya Mwalimu Nyerere kuhusu foreign policy na suala la viwanda, tukija hivi karibuni katika Awamu ya Mheshimiwa Kikwete, Rais Kikwete katika historia ya nchi yetu ndiye Rais aliyeenda zaidi katika kujiunganisha na mataifa ya nje katika suala zima la biashara na wazungu wanasema kama alienda ku-strike deal, ali-strike deal nyingi lakini bahati mbaya utekelezaji wake haukuweza kwenda sawasawa na matamanio ya Rais Kikwete mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumempata Rais Magufuli yeye sera yake zaidi ilikuwa ni ya protectionism, si zaidi ya nje, lakini alitaka kukuza base ndani ya nchi. Tumempata Mheshimiwa Samia katika Awamu ya Sita yeye zaidi anaangalia foreign policy na anaangalia zaidi katika kutafuta mitaji ya nje katika kukuza biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kifupi tumeona Mheshimiwa Samia ameenda katika nchi za Ulaya, ameenda Amerika, ameenda na Uarabuni. Safari ya Ulaya peke yake ina mikataba kiasi cha trilioni 11.7; lakini ile ni mikataba na katika mikataba kuna makubaliano, kinachosumbua katika nchi yetu ni namna gani sasa kufuatilia mikataba ile na kwa dhati mimi nataka nimpongeze sana Rais wa Awamu ya Sita anapokuwa nje mazungumzo yake mengi ni biashara na siyo misaada. Ukimnukuu na ukimfuatilia Rais wetu hayuko katika syndrome ya misaada anaangalia zaidi biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wasiwasi wangu ambao naupata kwamba tutapata mikataba mingi, lakini umadhubuti wa kutekeleza mikataba ndiyo changamoto tuliyonayo katika nchi yetu. Mikataba itakuja mingi na Rais atasafiri, lakini nani anafuatilia kutekeleza mikataba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo na Mheshimiwa Rais amekuwa anarudia kwamba kuna tatizo la coordination ndani ya Serikali na hili ni kweli ukiangalia katika Wizara hizi za biashara kwa maana ya Madini, Kilimo, Utalii na Uwekezaji, Viwanda na Biashara lakini nani anawaunganisha, hakuna chombo kinachowaunganisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Presidential Delivery Unit, wenzetu wa Malaysia wanaendelea nayo na ile ndiyo unaweza ku-coordinate, watu wa Wizara wakishatoka nje na ziara na Mheshimiwa Rais wakifika documents zinawekwa inakuja ziara nyingine documents zinawekwa lakini ni nani anasema sasa mkataba ule wa Belgium mkataba ule wa Ufaransa ni nani anafanya sasa jambo lifanyike. (Makofi)

Kwa hiyo, tutaenda sana nje, Rais wetu atafanya sana mahusiano ya mikataba, lakini utekelezaji ni changamoto. Kipindi cha Rais Kikwete tuliwahi kufanya makubaliano ya kwamba wale IBM ile the brain behind ya computer waje hapa Tanzania, lakini mikataba ile ilipotea, hatukuweza kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende haraka haraka tunaishauri Serikali kwanza iweke kitengo cha uwekezaji kwa mitaji ya nje na mitaji ya ndani, tunavutia wawekezaji waje ndani, lakini tuna Watanzania ambao wana uwezo mkubwa hatujaweza kuwaendeleza. Naishauri Serikali tuna makampuni makubwa wakina Azam, benki zetu kubwa kama CRDB sasa wako Burundi, je, tuna mpango gani wa kupanua zaidi kwamba na sisi watu wetu tuweze kuwatafutia maeneo na mitaji zaidi na masoko kwa ajili ya kwenda kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaweza tukataka kwamba tulete mitaji ndani, lakini mitaji tuliyonayo hatujaiendeleza, tunao Watanzania wenye mitaji kuanzia shilingi bilioni 10 kwa nini Mheshimiwa Rais asikutane nao na tuweze kupanga namna gani tunaweza kuwasaidia ili waweze kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Dangote tunayemuona leo ametengenezwa na Serikali ya Rais Obasanjo, Dangote alikuwa mchuuzi wa kawaida lakini akatengenezwa na Rais Obasanjo, sasa na sisi ni lazima tufanye hivyo tuwatengeneze matajiri wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa lipo suala la kupanda bei vitu, nataka niseme kwenye eneo moja tu na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda anielewe. Nchi yetu kila inavyofika Disemba cement inapanda katika kipindi cha miaka mitatu minne iliyopita na tatizo lililopo ni kwamba muwekezaji mkubwa wa cement anazima kiwanda kila mwezi wa 11 afanye matengenezo. Cement ilikuwa shilingi 16,000 mwezi Novemba alipozima ikapanda ikaenda hadi shilingi 20,000 na inaendelea hivyo hivyo. Sasa na ninaamini na mwezi wa 11 mwaka huu tena atazima kiwanda na cement itapanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini mchezo huu tuendelee kuwa nao ambao tunawaambia Fair Competition waangalie wadhibiti lakini hawawezi kufanya hivyo, ni kwamba kinachotokea ni kwamba ni mtu mmoja anazima kiwanda kwa ajili ya matengenezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)