Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na nikuombe radhi sauti yangu sio nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili tukufu na kunipa nafasi kuchangia kwenye Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana nikupongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Ashatu, Naibu Waziri na wasaidizi wako wote kwa kazi nzuri ambayo mmeendelea kuuifanya ambayo imeonekana kwenye hotuba uliyowasilisha katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na mjadala mkubwa hata kabla ya uwasilishaji wa bajeti ya Wizara hii hususani katika eneo zima la kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali na mimi naomba nichangie kwa bidhaa mbili ambazo zinawagusa wanawake wa Tanzania na hususani wanawake ambao ninawawakilisha wa Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mjadala huu lakini lazima tukubaliane sababu zinazotolewa za kupanda kwa bei ya bidhaa ikiwemo ugonjwa wa Covid, ikiwemo vita ya Ukraine na Urusi ni sababu za msingi, hata ukisoma mitandao mbalimbali duniani sababu hizo zinatajwa. Kwa hiyo kwa sasa hatuwezi kubishania sababu, lakini sababu zipo na athari zake ndio hizi kupanda kwa bei za bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nikubaliane na niipongeze Serikali kwamba imeonesha uongozi kwa namna mbalimbali, kwa mfano kwa bei ya mafuta kwa hatua ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo kuwa champion katika mazao yanayohusiana na bidhaa ya mafuta mfano, mawese, ufuta, karanga, soya na alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ametoka kusema hapa namna ambavyo amegawa mbegu ya alizeti katika mikoa mbalimbali na mimi niseme kwa Mkoa wa Pwani tumefikiwa na mbegu za mawese na imewezesha kikundi kimojawapo cha Kata ya Ruwaruke, Kibiti kimepata biashara kubwa ya mafuta ya mawese kwa sababu Wilaya ya Kibiti mawese yanastawi. Lakini katika hili nishauri, niiombe Serikali kampeni hii iwe kaya kwa kaya kama ambavyo imetokea nyakati mbalimbali za wakati wa njaa kwa mfano Mkoa wa Mtwara kulikuwa na kampeni ya ondoa njaa Masasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika wakati huu wa kupambana kushusha bei ya mafuta niiombe Wizara ya Kilimo kwa kusaidiana na Wizara hii igawe mbegu kwa kaya zote katika maeneo yanayostawi alizeti, lakini Wizara ya Viwanda mtusaidie kupitia SIDO kuzalisha vifaa vidogo vidogo vya kuchakata haya mafuta yafike ngazi ya kaya ili kupunguza bei hiyo ya mafuta kwamba tutakuwa tunazalisha kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la mbolea pamoja na jitihada zinazoendelea uwepo wa kiwanda cha kuzalisha mbolea hapa Dodoma niiombe Serikali iifufue mazungumzo ya viwanda vya kuzalisha mbolea vya Kilwa na Mtwara ambako makampuni yalijitokeza na kilichobishaniwa pale ni bei ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kwakuwa hata Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais alilishughulikia hili mkamilishe na natambua uwezo huo upo kwa kuwa mmefanya kazi kubwa katika mradi wa kuchakata gesi asilia Lindi. Nina imani kwa bei ya gesi ili viwanda vile viwe vikianzisha vitapunguza bei ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye suala zima la ngano niiombe Serikali pia pamoja na kwamba tunaagiza kiwango cha ngano cha kutosha nje ya nchi ifufue mashamba ya ngano na kuwekeza zaidi ili tuweze kuzalisha kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima hili la bei najiuliza ni kweli bei zinapanda, lakini kama tungekuwa Serikali haitafakari kuongeza ajira, haitafuti wawekezaji nje ya nchi ili kuja kuanzisha viwanda hapa na katika hili nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na kuonesha uongozi, pamoja na changamoto inayoendelea lakini kwa hatua zake za kusafiri pamoja na sekta binafsi kufanya vikao, kuvutia uwekezaji, tutaendelea na kupanda kwa bei, lakini tuna uhakika sasa kwa mfano makubaliana ya Marekani ya zaidi ya trilioni 11 kupitia Expo Dubai trilioni 18; lakini wamesema hapa Jumuiya ya Ulaya wamekubaliana trilioni 11 tuna uhakika wa uwekezaji huo na hapa nishukuru Mkoa wetu wa Pwani wa kupata kongano eneo la Kwala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunaokaa Mkoa wa Pwani tunaona namna ya safari za Mheshimiwa Rais na jitihada zake zinavyoleta matumaini, tunapokuwa na mfumuko wa bei unakuwa na vijana wengi wasiokuwa na ajira unakuwa na Watanzania wengi wasiokuwa na ajira, bei zimepanda hana kitu cha kununua bidhaa hizo haiwezekani, lakini unapokuwa na mfumuko wa bei unakuwa na nchi ambayo haizalishi kuna bidhaa hatuzalishi, lakini kupitia hatua hizi za kuvutia wawekezaji naamini tutavuka ingawa inaweza ikachukua muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niiombe Serikali, nikuombe Mheshimiwa Waziri Dkt. Ashatu, sekta binafsi ni kama jimbo lako la pili ilee hii sekta binafsiā€¦

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)