Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma ambaye ametusaidia mpaka hivi sasa tumekuwa tukitimiza majukumu yetu. Lakini pia niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi kama nilivyowahi kufanya siku zote kwa kuweza kunisaidia kuniombea dua hivyo kuhakikisha kwamba matarajio yao tunayatimiza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba Wizara hii ni Wizara muhimu sana katika nchi hii, lakini hata nchi yoyote ile duniani, kama haujajipanga vizuri kwenye Wizara hii ya muundo huu yenye viwanda basi wewe upange kwamba unakaribia kufeli. Nashukuru kwamba kwa namna moja ama nyingine kumekuwa na uthubutu mkubwa sana kutaka Wizara hii ifanye kazi kwa kadri tunavyotarajia, lakini bahati mbaya tumekuwa na mtazamo ambao sio sahihi katika kuhakikisha kwamba Wizara hii inapewa uhalisia au inapewa hadhi inayostahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu gani, ukiangalia bajeti ya Wizara hii ni bajeti finyu sana, lakini ukiangalia umuhimu wake utakuta kwamba hii Wizara ina umuhimu mkubwa kwa sababu biashara ipo kwenye Wizara hii, sekta ya uzalishaji mali nyingine kwa maana ya viwanda ipo katika Wizara hiyo, lakini sekta ya ujasiriamali pia inashughulikiwa kikamilifu katika Wizara hiyo na sekta ya uwekezaji pia. Sasa ukiangalia sekta ya biashara, uwekezaji, ujasiriamali, na viwanda ni kama vile ni Wizara nne tofauti ambazo zimewekwa katika Wizara moja kwa maana hii unaweza ukaona kwa jinsi gani Wizara hii ni muhimu sana katika mhimili wa uchumi lakini uzalishaji na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyotangulia ukiangalia majukumu ambayo Wizara hii imepewa yameji- limit kwenye uratibu tu yaani Wizara hii haijajielekeza katika utekelezaji, kuna mambo mengi sana ambayo ni ya msingi sana katika kuhakikisha nchi inakwenda ambapo kama Wizara hii ingepewa jukumu hilo hayajapewa na hasa hasa tukiangalia kwa mtazamo huo inakuwa ni vigumu sana kwa Wizara hii kujiendesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachoomba kwa ujumla tunatakiwa wote sisi kwa maana ya Wabunge tukae pamoja na hii Wizara tuisaidie, itazame katika mtazamo sahihi, iwe ni Wizara sahihi ya uzalishaji lakini ni Wizara ya kibiashara lakini ni Wizara ya kiuwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali iliyopo sasa hivi imekuwa kama na Wizara inayojishughulisha na masuala ya uchuuzi tu, jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Rais kwa namna moja ama nyingine zinaonekana, lakini ninahofia kwamba hivi jitihada zinaweza zisifike popote kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya Wizara hii, lakini ufinyu wa utendaji kazi kwenye hii Wizara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninawaomba sana ndugu zangu watu wa Wizara, lakini wadau wengine naomba tuishughulikie hii Wizara iwe na muonekano sahihi wa Wizara ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumzia hapa linahusiana na vikwazo vya Wizara hii kuna nyenzo muhimu sana ambayo Wizara hii kama kweli tunataka ifanye kazi nayo ni blueprint. Blueprint ni assurance kwa wafanyabiashara au wawekezaji kuja kuwekeza, hatuwezi kuwaambia tu kwa maneno kwamba mje muwekeze wakati hakuna sheria zinazo wa-assure kwamba wakija hapa mali zao zitakuwa guided, lakini pia uwekezaji wao utakuwa ni wenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna changamoto nyingi sana kwenye blueprint ukiangalia kwa mfano masuala ya kodi, kodi kwa mfano ya VAT ukiangalia unaona kwa jinsi gani inavyoathiri na kuwafanya wawekezaji washindwe kuweka fedha zao, tulipotembea kwenye shughuli za kikamati kwa mfano Dar es Salaam kwenye Kampuni ya ALAF na ile kampuni nyingine sikumbuki vizuri ambayo wanajishughulisha sana masuala ya uzalishaji wa mabati na aluminum kwa ujumla wanalalamika kwamba wanaidai Serikali VAT kwa takribani shilingi bilioni 20 ambazo zilitakiwa zirudishwe…
(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: ...kwa makampuni hayo mawili tu. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mchungahela, ahsante sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahante naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante. (Makofi)