Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana; na mimi nichangie hoja ya Mheshimiwa Kigua ambayo naiunga mkono asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Watanzania wapo katika hali ngumu sana sasa hivi kutokana na kupanda kwa bei za mafuta ambako kunapandisha sasa bei karibu zote. Na ni jambo la kuipongeza Serikali kwa kikao cha jana, wamekaa kikao cha jana, tumepata taarifa. Lakini yale yaliyojadiliwa jana yanalenga kupunguza kuanzia mwezi wa sita mwishoni, wa saba, wa nane huko. Maana yake ni kwamba hapa katikati hapa maumivu kwa Watanzania yatakuwa makubwa.

Mheshimiwa Spika, mimi nina ushauri. Ushauri wa kwanza nilikuwa kwenye nchi ya Kenya wiki tatu zilizopita na bahati nzuri nikakutana na Waziri wa Fedha Kenya, Mheshimiwa Ukur Yattani, nikamuuliza mmepata wapi fedha ninyi kwenye bajeti yenu za kutoa ruzuku takriban shilingi za Kenya bilioni 34.4 ambazo kwa Tanzania hapa ni karibu shilingi bilioni 900, mmepata wapi kwenye bajeti? Akaniambia bwana hatujapata kwingine isipokuwa hizi fedha tumezikopa IMF.

Sasa kama wenzetu Kenya wanaweza wakakopa hizo fedha wakawapunguzia wananchi wao maumivu ya mafuta na Kenya maumivu ya mafuta ni makubwa kuliko ya Tanzania, foleni zilizokuwepo Kenya wakati ule na mpaka sasa bado zinaendelea na wana ration ya mafuta, sisi hapa hatujapata hali kama hiyo. Sasa kama wenzetu Kenya wana maumivu makubwa na Serikali yao imechukua hatua hiyo ya dharura, kwa nini sisi Serikali yetu isikope kwa ajili ya kupunguza maumivu kama walivyofanya wenzetu?

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni kweli nchi yetu ni kubwa kuliko nchi nyingine. Katika nchi zinazotuzunguka hapa sisi Tanzania ni kubwa kuliko nchi nyingine isipokuwa Kongo, kwa hiyo, hatuwezi kulingania intervention zinazochukuliwa na Tanzania tukalinganisha na Burundi, tukalinganisha na Rwanda ni vinchi vidogo vidogo sana vikieneo, ukalinganisha na Malawi sijui Zambia, hapana. Nchi yetu ni kubwa…

SPIKA: Mheshimiwa Kakunda subiri kidogo, ni nchi ndogo kwa maeneo ya kijiografia siyo vinchi. Rekebisha kauli yako.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nchi ndogo kijiografia yaani kieneo, yaani sisi ni nchi kubwa kieneo, kilometa za mraba kwa mfano. Sizungumzii nchi ndogo kwa namna kudharau, hapana, hizi nchi zinazotuzunguka ni ndogo kijiografia.

Kwa hiyo kusafirisha kwa mfano mafuta kutoka Dar es Salaam mpaka Kagera ni mwendo mrefu zaidi kuliko kusafirisha mafuta kutoka kwenye ncha moja ya nchi ya Rwanda kupeleka ncha ya mwisho. Kwa hiyo, ni gharama kubwa zaidi kusafirisha mafuta kwa nchi yetu. Kwa hiyo ushauri wangu kwa Serikali yangu hata usafirishaji wa mafuta inabidi muubadilishe, kwamba katika maeneo mengi tutumie reli badala ya kutumia malori ya matenki ya mafuta itashusha gharama za mafuta.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa mwisho, ningependa kuishauri Serikali yangu na hili ni jambo la muhimu sana. Wananchi wanahitaji kupata matokeo ya haraka, kama kuna mbinu mbadala za kuagiza mafuta ambazo zitashusha bei ya mafuta kwa haraka basi zitumike hizo badala ya mbinu ambayo sasa hivi imesababisha ongezeko la mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)