Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Kwanza naomba nikushukuru sana kuruhusu hoja hii ijadiliwe na Bunge, lakini naipongeza Serikali kwa hatua ambayo kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu kufanya kuijadili kuangalia namna ya kupunguza shida ya mafuta Tanzania.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu wakati nimesimama hapa naomba mwongozo wako wakati ule ilikuwa ni hoja hii. Kwa hiyo, kwa kunipa nafasi ya kuchangia maana yake sintarudia tena kusimama itakuwa imekufa.
Mheshimiwa Spika, mambo yafuatayo moja ni kwamba bei imepanda ya mafuta na bei hizi kuna mjadala mkubwa sana kwenye mitandao ya kijamii inaendelea, wananchi wamepata mkanganyiko. Kama sisi kwa mfano, nchi kama Zambia ukiangalia bei ambao wanauza kule Zambia diesel kule shilingi 2,470 lakini tunajua wengi mizigo yao wanapitishia kwetu hapa, lakini sisi hapa Tanzania diesel imetangazwa bei ya EWURA ni zaidi ya shilingi 3,000.
Mheshimiwa Spika, watu wameenda mbali zaidi kuangalia mpaka Msumbiji kule Maputo bei ikoje, wamezungumza bei ya mafuta kule Zanzibar na wanajaribu pia kutugawa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni jambo ambalo Serikali lazima ichukue hatua za dharura. Kwa sababu, kwa mfano mimi natoka Tarime Vijijini kuna hoja imezungumzwa kwamba Rais wa Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta ameweka ruzuku ya Shilingi Bilioni 850 au Zaidi, lakini Wakenya wakati wa shida ya mafuta kule Kenya walipiga foleni kule Tarime mpaka hapa Kirumi kuja Musoma kuchukua mafuta. Baada ya Mheshimiwa Rais wa Kenya kuweka ruzuku kwenye mafuta yao zile foleni pale Tarime hazipo sasa, maana yake imekuwa na impact, mafuta kule Kenya yameshuka wanapata huduma ndani ya nchi yao.
Mheshimiwa Spika, kwa wale ambao wanabeza kwamba ruzuku haitasaidia kwamba siyo kweli, itasaidia sana kuondoa kero kwa wananchi, itasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliana kwamba sasa hivi kwa mfano, nadhani wiki iliyopita walitangaza kupandisha bei ya nauli kwa mabasi, sasa bei imepanda jana tutarajie kwamba kesho keshokutwa wenye mabasi watapandisha bei kwa sababu mafuta yamepanda na wanayo hoja ya kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hili kwa kweli ni jambo muhimu kweli Serikali kuchukua hatua. Hatua ya kwanza ni kwamba Serikali iangalie namna ya kuongeza ruzuku ili kupunguza bei. Pili ni kupunguza zile tozo ambazo bei zinapanda duniani kote, lakini bei zipo kwenye individual countries kwa sababu ya kodi ambazo wameziweka. Kwa hiyo, sisi kama Serikali, kama nchi tukae chini tuangalie ni kitu gani kifanyike kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wetu na wananchi hawana namna yoyote ile wanaangalia Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi, yenye huruma, sikivu iwaondolee uchungu wa maisha ya ukali ule ili waendelee kuishi kwa raha katika Serikali yao ambayo wanaipenda sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja tunatarajia kwa hatua ambayo Serikali imechukua jana kukaa pamoja, wasikae vikao virefu, watu wanaendelea kuumia, maneno mengi mtaani, waje na suluhu ya dharura ya kusaidia Watanzania ili maisha yaendelee.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Kigua. (Makofi)