Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa kibali kusimama hapa leo.
Mheshimiwa Spika, kwa haraka haraka naomba nianze kwanza kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ujumla na Jeshi la Polisi na hasa IGP Sirro. Juzi tumemwona Mheshimiwa Waziri na Afande IGP wakitoa tamko na tamko lao limeanza kufanyiwa kazi na kazi tumeiona. Angalau kwenye Sikukuu hii kumekuwa na utulivu kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Jeshi la Polisi kupitia usalama barabarani kumekuwa na madereva ambao ni watukutu na hasa madereva ambao wanaendesha mabasi yaendayo Mikoani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukifika saa 12 pale katika Kituo cha Magufuli, Dar es Salaam, jinsi magari yanavyoongozana, yanakimbia utafikiri Nyumbu wanatoka Serengeti kwenda Masai Mara; ni mbio bila huruma. Hawajali abiria wala magari. Vile vile kuna madereva wa magari ya Serikali, wanaendesha magari kwa kasi sana. Wamehatarisha maisha ya viongozi, na maisha ya wataalam wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, roho za watu haziuzwi dukani. Tunaomba kila mtu afuate taratibu. Kwa sababu dereva wa Serikali anaweza kusababisha kukatisha maisha hata ya masikini ambaye anategemewa na watu huko nyumbani. Tunaomba Jeshi la Polisi lifanye kazi yake, litoe semina kwa hawa madereva ambao hawajafuata taratibu za usalama barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongee kidogo kuhusu hili suala la panya road, wamekuwepo siku nyingi na viongozi wameshatoa matamko mengi. Hata hivyo, kumbukumbu yangu inanieleza kwamba wamekuwepo kipindi kirefu huko nyuma, wanakuja wanaondoka, wanakuja wanaondoka.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali tuweke mifumo ambayo itasaidia malezi kwa vijana wetu. Wanapomaliza darasa la saba wanakosa kazi, wanaenda kukaa kwenye magenge yale wanaita vijiwe. Kwenye vijiwe kule wanavuta bangi. Ukivuta bangi unaondoa uoga, unakuwa mkatili, wanakwenda kuwararua wazazi wao ambao hawana hatia.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali itenge makambi ya kilimo kwa ajili ya vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam, hawa nguvu zao wakazitumie kwenye kilimo. Serikali iandae masoko, iweze kuwasimamia hawa vijana waweze kupata fedha, tusiwaache bure. Ukiwaacha bure, watakuwa wanapata walimu wa kuwafundisha maovu. Naomba sana Serikali itusikilize katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongee kuhusu Jeshi la Zimamoto. Jeshi hili limekuwa halina wataalam wazamiaji. Mfano mmoja, juzi kulitokea maafa kule Bagamoyo, kuna kijana alizama kwenye dimbwi la maji pale Msata, wakaitwa Jeshi la Zimamoto, walikosa watu wa kwenda kuwaokoa. Wakaita watu wa private, wakawalipa shilingi milioni moja wakaenda kuokoa, wakakuta yule mtu ameshafariki. Naiomba Serikali itoe mafunzo kwa Askari wetu wa Zimamoto, itenge fedha za kutosha katika Jeshi hili ndani na nje, lakini pia iwape motisha ili wawe na mvuto katika kufanya kazi katika Jeshi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba vitendea kazi. Hawana magari ya kutosha, vifaa hakuna vya kutosha, lakini maendeleo yanakuja kwa kasi, majengo makubwa yanakuja, kuna viwanda, kuna reli, kote kule kuna tahadhari zinatakiwa kwa ajili ya hili Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili wapate vifaa waweze kusaidia hapo itakapotokea hayo majanga.
Mhshimiwa Spika, nije kwenye Jeshi la Magereza. Nalipongeza Jeshi la Magereza kwa sababu kwa sasa limejitegemea kwa asilimia 80 kwa chakula, kutoka zero mpaka asilimia 80 kwa chakula, nalipongeza sana. Naomba Serikali iwaongeze ili waweze kujitegemea kwa asilimia 100 ili kuipunguzia Serikali katika kupanga bajeti za kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee NIDA.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Spika, naomba niongelee NIDA, dakika moja tu. (Makofi)
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)