Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya mambo ya Ndani iliyoko mbele yetu. Kabla ya kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii na mimi nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya, hasa jinsi alivyochukua hatua za haraka na za makusudi akishirikiana na IGP Sirro kwenye kutatua tatizo la kiusalama lililopo kwenye baadhi ya maeneo ya katika Jiji la Dar-es-Salaam. Wanastahili pongezi kwa jinsi wanavyochukua hatua za kutatua changamoto hizo za kiusalama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi katika mchango wangu nataka nijikite kwenye mambo mawili makuu au matatu. Kwa uchache wa muda nataka niende harakahara.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni kuhusu uhaba wa vituo vya polisi kwenye maeneo yetu. Kwa mfano mimi kwenye Jimbo langu la Chakechake, Wilaya nzima ya Chakechake ambacho ndicho kitovu na centre ya uchumi katika Kisiwa cha Pemba tuna Kituo cha Polisi kimoja tu. Watu wanafuata Kituo cha Polisi wakitoka masafa ya mbali kwelikweli.

Mheshimiwa Spika, polisi wanapofanya shughuli zao wanatoa huduma kwa kuwa shughuli za kipolisi ni huduma kama vile wananchi wanavyohitaji maji, elimu pamoja na umeme. Kwa hivyo wanavyohitaji ulinzi wa mali zao na wao raia kulindwa ndivyo wanavyohitaji huduma kama huduma nyingine. Kwa hivyo mtu kutoka eneo moja kutembea zaidi ya kilometa 15 ama 20 kufuata Kituo cha Polisi hili ni jambo ambalo sasa linatakiwa lifike mwisho. Watu wanatoka Pojini kufuata Kituo cha Polisi Madungu. Watu wanatoka Ole kufuata Kituo cha Polisi Madungu. Kituo hicho chenyewe ni kidogo, hakitoshi, kuna mlundikano wa mahabusu ambao wanakuwepo kwenye Kituo cha Polisi kabla hawajapelekwa Mahakamani. Kichumba hicho cha mahabusu cha ndani ya polisi ni kidogo, baadhi ya nyakati kinakusanya mpaka watu 40 ama 50 at a time, ni jambo ambalo sio zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi hapa alikuwa anajibu swali Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Sagini, alisema lilishatengwa eneo katika Wilaya ya Chakechake kwa ajili ya kujengwa kituo kingine ili kuondoa huo usumbufu, lakini tuliposoma eneo lote la bajeti hatukuona kwamba kuna jitihada za makusudi za kujengwa kituo kingine cha polisi. Kwa hiyo natoa wito, hali yetu ni mbaya, wananchi wanatembea masafa marefu kufuata huduma za kipolisi. Sasa tuko miaka 58 sasa ya tangu muungano wetu na tangu tulivyounganisha Jeshi letu la Polisi, lakini bado tuna kituo kimoja wilaya nzima. Hii haikubaliki, tunahitaji, na ushauri wetu ni kwamba, polisi waongeze huduma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi walioko kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili utajikita kwenye kubadilika kwa ufanyaji wa makosa. Sasa hivi ufanyaji wa makosa unafanywa sana online, unafanywa kwenye mitandao, lakini uwezo wa Jeshi letu la Polisi kwenye kukabiliana na kufanya upelelezi kwenye mitandao uko nyuma kulingana na ufanyaji wa uhalifu walioko mbele. Teknolojia imewafanya wahalifu wawe mbele zaidi kuliko uwezo wa Jeshi letu la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetunga Cyber Crime Act ili kukabiliana na makosa yanayofanyika kwenye mitandao. Tunayo Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Electronic and Postal Communication Act, lakini kufanyika kwa investigations za kipolisi kumekuwa na changamoto kubwa kwelikweli. Kituo cha Cyber cha Kipolisi kipo kimoja tu, Dar-es-Salaam. Sasa hivi ukitaka kufanya investigation za ki-digital kwa mfano kosa limeanzia kwenye simu, inabidi uchukue hiyo simu uliyoikamata kama kielelezo, uisafirishe, ipelekwe cyber center ikafanyiwe upelelezi. Hata ikirejeshwa ukitaka huyo shahidi atoke Dar-es- Salaam mpaka afike Pemba hilo kosa limeshachukua miaka miwili halijasikilizwa Ushahidi wake; kwa hiyo tuna changamoto kubwa kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa wito kwamba, umefika wakati sasa tupanue vituo vya cyber centers kwa ajili ya investigations za kipolisi kwenye maeneo ya kikanda, hasa Zanzibar. Muda umefika tuwe na kituo cha cyber cha Zanzibar kwenye kufanya investigations za kipolisi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)