Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia Wizara hii muhimu kwa mambo makuu saba.

Mheshimiwa Spika, kulingana na sheria za kimataifa ambazo nasi tumeingia mkataba zinataka wafungwa na mahabusu waweze kupewa haki na heshima kama binadamu wengine. Pia Sheria ya Magereza ya mwaka 2002 kifungu cha 58 kinaelekeza magereza kuwa na miundombinu wezeshi na toshelezi kuweza kutoa huduma bora ya afya, usalama maeneo ya gereza, usafiri imara, maji safi na salama, mfumo wa maji taka, majengo imara na salama, umeme na kadhalika, hayo yote yamekuwa ni kitendawili kwenye huduma za magereza.

Mheshimiwa Spika, ripoti ya ukaguzi ya ufanisi iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iligundua kutokuwepo na sera na mipango ya kitaifa ya huduma za magereza, licha ya kuwa kwenye Mpango Mkakati wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 kuonesha umuhimu wa kuwa na sera ya kitaifa ili kuwezesha utolewaji wa huduma za magereza nchini.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mrundikano mkubwa wa mahabusu na wafungwa kwenye magereza nchini ambapo hupelekea mlipuko wa magonjwa kama vile homa ya matumbo, UTI, amoeiba, kuhara na kadhalika. Haya yote yanasababishwa na kuchakaa kwa miundombinu ikiwemo mifumo chakavu ya maji safi na salama, maji taka, makazi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, huu mrundikano unatokana na uhalisia kwamba magereza mengi yamejengwa tangu enzi za mkoloni, mfano Gereza la Tarime limejengwa tangu mwaka 1942 ambapo uwezo wa gereza ilikuwa ni watu 209 lakini leo hii linabeba kati ya watu 460 hadi 600 zaidi ya mara tatu. Vilevile ripoti ya ukaguzi imeonesha mrundikano mkubwa kwenye Gereza la Keko ambalo lilikuwa na idadi ya mahabusu na wafungwa 999 badala ya uwezo wake wa 340.

Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto hii ni lazima Serikali ifanye ukarabati wa majengo na upanuzi ili uendane na hali halisi ya ongezeko la watu, ujenzi wa magereza walau kila Wilaya kwa kuzingatia uhalisia wa mahitaji kutokana na idadi ya uhalifu.

Mheshimiwa Spika, mpango mkakati wa Jeshi la Magereza ilikuwa kujenga magereza kumi ndani ya miaka mitano, ila ripoti ya ukaguzi imegundua kuwa ni magereza mawili tu yalijengwa Chato mwaka 2018 na Ruangwa mwaka 2019 bila kufanya uhakiki wa mahitaji (needs assessments), ambapo walijenga magereza bila kuwa na mpango wa mwaka wala bajeti na hivyo kutojulikana hata chanzo cha fedha kwa ujenzi wa magereza hayo kwenye eneo ambalo halina idadi kubwa ya wahalifu.

Mheshimiwa Spika, magereza nyingi zimechakaa sana na hazifai kwa binadamu kuishi, mfano Gereza la Tarime limechakaa sana, linavuja, miundombinu ya majitaka na maji safi na salama. Magereza nyingi hazina miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji, miundombinu ya maji taka imechakaa na kuvuja, magodoro, miundombinu ya vyoo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilisitisha kupeleka fedha kwenye Jeshi la Magereza tangu mwaka 2016/2017 na hivyo kupelekea ugumu katika kutekeleza na kuhudumia Jeshi la Magereza. Ni rai yangu sasa Serikali iwe inapeleka fedha kwani mapato ya ndani kwa magereza ni fedha ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile kumekuwa na uhaba wa nyumba za wafanyakazi kwenye Jeshi la Magereza. Ripoti ya ukaguzi iligundua upungufu wa nyumba za askari magereza ambapo uhitaji wa nyumba ni 14,747 na zilizokuwepo ni nyumba 4,221 sawa na 29%. Licha ya mpango mkakati wa Jeshi la Magereza kuonesha kujengwa kwa nyumba 14,000 na kukarabati 2,000, cha ajabu hakukuwahi kuwepo na mpango wa mwaka wala bajeti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizi. Nyumba nyingi ni zile zilizojengwa tangu enzi za mkoloni mwaka 1942 mfano Gereza la Tarime nyumba za wafanyakazi zimechoka na kuchakaa zilijengwa enzi ya mkoloni na ni full suit ya bati, zinavuja na hazina faragha ya kifamilia, walau Tarime kuna nyumba tatu ambazo zilijengwa kwa juhudi za aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Ndugu Luoga kwa kushirikiana wadau mbalimbali mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, ripoti ya ukaguzi iligungua uchakavu wa nyumba za askari magereza kulikopelekea miundombinu mbalimbali kuchakaa kama vile ya maji safi na maji taka. Ukosefu huu wa nyumba unapelekea askari magereza kukaa nje ya eneo la magereza kinyume na Prison Standing Order ya 2003. Wafanyakazi wengi wanakaa nje ya gereza mfano Gereza la Wazo Hill askari zaidi ya 72% na Gereza la Segerea zaidi ya 65% wanakaa nje ya gereza.

Mheshimiwa Spika, naomba pia kuzungumzia uhaba wa usafiri kwa mahabusu, wafungwa na askari magereza. Ni muhimu sana magari yakawepo walau moja kwenye kila gereza ili kurahisha upelekwaji wa mahabusu mahakamani na hivyo kuharakisha usikilizwaji wa kesi na kupunguza msongamano.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza halijawahi kununuliwa magari nje ya yale nane yaliyotewa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Pwani kwa msaada wa Legal Sector Reform Programs ambapo magari nane yalikabidhwa mwaka 2008 ili kupeleka mahabusu mahakama.

Mheshimiwa Spika, hii ni fedheha na kutokuweka vipaumbele kwenye maslahi ya Watanzania. Hivi kweli tunakosa fedha za kununua magari haya muhimu na ya bei nafuu ila tunapata fedha za kununulia magari ya washawasha ambayo yanatumika mara moja kila baada ya miaka mitano kwenye nyakati za uchaguzi tu, tena gari moja la washwasha ni zaidi ya gari nane za kutoa huduma ya kupeleka mahabusu mahakamani. Mfano ripoti ya ukaguzi imeonesha upungufu mkubwa wa magari mfano Gereza la Butimba wanaupungufu wa magari sita, Keko magari manne, Segerea magari manne, huku Gereza la Pangami likiwa halina gari kabisa.

Mheshimiwa Spika, Tarime napo hamna gari, wanatumia la Jeshi la Polisi lakini gereza lile linachukua watu toka nje ya Tarime kama vile Wilaya ya Rorya walau kwa sasa kesi zinapelekwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Tarime. Sasa kuna ujenzi wa mahakama unaanza Wilaya ya Rorya na kule hamna gereza je, hawa mahabusu na wafungwa wenye rufaa watafikaje mahakamani Rorya toka Gereza la Tarime bila gari? Vinginevyo Serikali ifunge mifumo ya kisasa kama ile ya mahakamani ili kuweza kurahisisha usikilizwaji wa kesi bila mahabusu kwenda mahakamani, ili kupunguza mrundikano wa mahabusu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia Serikali iweze kutoa fedha kwa ajili kutengeneza magari machache yaliyopo kwenye baadhi ya magereza. Kuweza kununua magari ya ambulance kwa ajili ya huduma kwenye magereza zote nchini.

Mheshimiwa Spika, magereza zinatumika kuhifadhi binadamu wanaostahili heshima kama binadamu wengine, lakini kumekuwepo na upungufu wa miundombinu na mifumo ya kiusalama kama vile scanner, metal detector, search light na CCTV camera kwenye magereza nyingi nchini. Mfano ripoti ya ukaguzi inaonesha kati ya magereza 15 zilizofanyiwa ukaguzi ni Gereza la Keko na Segerea tu ndio walikuwa wamefungwa CCTV camera tu. Hii sio sawa ikizingatiwa aina ya upekuzi inayofanyika katika magereza yetu yanatweza utu wa binadamu na tumekuwa tukisisitiza kubadilishwa kwa aina ya ukaguzi ili kuendana na dunia ya sasa.

Mheshimiwa Spika, ni muda muafaka sasa Serikali kuhakikisha inatenga fedha ili kufunga scanner machine walau kwenye magereza ya Mikoa na Wilaya.

Mheshimiwa Spika, mwisho kumekuwepo na muendelezo wa matabaka kwenye maslahi ya askari wa Jeshi la Magereza ikilinganishwa na askari wa Jeshi la Polisi wakati wapo kwenye Wizara moja. Mfano askari polisi mwenye degree analipwa shilingi 860,000 wakati askari magereza analipwa shilingi 770,000. Lakini pia mwanajeshi mwenye nyota moja na degree analipwa shilingi 1,200,000 na stahiki zingine lukuki kama vile posho ya pango, umeme, maji. Nashauri yafanyike marejeo ya mishahara na stahiki zingine ili kuondoa haya matabaka na kuongeza morali ya kazi.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna askari magereza walipandishwa vyeo tangu mwezi Julai, 2021 lakini hawajaanza kulipwa mshahara mpya, je, tatizo ni nini?

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazingira magumu, baadhi ya mambo ambayo yanahitaji jitihada za haraka ni maofisa na wakaguzi kuhamishwa bila kulipwa fedha za uhamisho, mfano kuna askari ambao wanahamishwa hadi mara tatu ila hawalipwi stahiki zao za uhamisho mpaka wanastaafu hadi wengine wanafariki dunia.

Pili, vitendea kazi vimekuwa ni shida kwenye kutekeleza majukumu yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao, hakuna magari mapya ambayo yamenunuliwa tangu mwaka 2015. Magari yaliyopo ni mabovu na fedha za kuyatengeneza hazitolewi, jeshi linageuka kuwa ombaomba kwa matajiri hata fedha za mafuta ya magari za operations za kila siku. Maana wakijaziwa basi nilita 10 au 20 tu ambazo si chochote.

Mheshimiwa Spika, samani za ofisi za Jeshi la Polisi zimekuwa chakavu na za kuokoteza, yaani ofisini ni mabenchi yaliyochoka, viti vya plastic tofauti tofauti. Yaani zikishachokwa huko kwenye ofisi zingine ndio wanapewa hawa askari wa chini. Ukiingia kwenye ukumbi au bwalo la polisi utadhani store ya viti chakavu.

Mheshimiwa Spika, stahiki za upelelezi, ujuzi na pango la nyumba, kuna askari polisi wanazungushwa stahiki zao hizi hadi wanastaafu. Pia outpost nyingi zimechakaa na mapaa yanavuja, wakati hizo outpost ndio zinasaidia sana.

Mheshimiwa Spika, kumeanzishwa polisi kata wenye nyota moja lakini hawana hata usafiri wa pikipiki. Hii sio sawa maana hawa wanawajibika kwa usalama wa raia na mali zao kwa kata nzima. Inasikitisha jinsi Jeshi la Polisi halipewi kipaumbele mfano Mtendaji Kata ana pikipiki na hata Afisa Ustawi wa Jamii ila Afisa Polisi wa Kata hana kitu.