Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kusimama tena katika Bunge hili Tukufu. Napongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya ndani ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Viwanda pamoja na Kilimo inasisitiza katika suala zima la agro-processing kwa maana ya kuchakata mazao ili kuyaongezea thamani sambamba na kuongeza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye tumbaku tumefanya vizuri tuna TCC, vile vile kwenye chai tuna viwanda mbalimbali vya kuchakata chai. Tukienda kwenye pamba, tuna asilimia 70 tunasafirisha pamba nje, hatujafanya vizuri. Nilikuwa naomba kilichotokea kwenye pamba tujitayarishe kisije kutokea kwenye zao la parachichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Njombe ni wazalishaji wazuri sana wa zao la parachichi pamoja na baadhi ya mikoa mingine ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, tuna uhakikia kabisa wa malighafi nyingi ya zao la parachichi. Ushauri wangu kwa Serikali ni kuona namna ya kuhamasisha na kuwashawishi wawekezaji wafungue viwanda vingi sana ndani ya Tanzania ili malighafi hii ya parachichi itumike hapa kwetu, ichakatwe katika viwanda vyetu ili kuwaongezea thamani wakulima na kilimo chao kiwe na tija, sambamba na kuongeza ajira ambayo ni changamoto kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuiomba Wizara iangalie namna ya kuongeza viwanda vya chuma vya msingi, kwa sababu Tanzania tuna viwanda vya msingi vya chuma viwili tu; tuna KMTC ambacho kipo Moshi na Mang’ula kile ambacho kipo Morogoro. Viwanda hivi vipo chini ya NDC, ni vya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia tuna viwanda vya nondo 15 ndani ya nchi yetu ya Tanzania. Viwanda hivi vyote vina-suffer raw material ya chuma, na matokeo yake vinatumia vyuma chakavu katika uzalishaji. Vile vile tumeona tumekuwa na changamoto nyingi sana ya uharibifu wa miundombinu, watu kutafuta hivyo vyuma chakavu ili viweze kwenda ku-supply kwenye viwanda vile vya nondo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais aliwahi kuzungumza kule Arusha na kutoa maelekezo kwamba Serikali ifanye mchakato haraka wa kumaliza mazungumzo na yule mwekezaji wa Liganga na Mchuchuma.

Naiomba Serikali tuendeleze hili zoezi la kuzungumza na huyu mwekezaji; huu mradi wa Liganga na Mchuchuma uweze kufanya kazi ili tuweze kupata viwanda vingi vya msingi vya chuma, tuweze kuzalisha vyuma vingi na tuweze kupata raw material nyingi ya chuma ambayo itatumika kwenye viwanda mbalimbali kama hivyo vya nondo.

Pia vitaanzishwa viwanda vingine vya kutengeneza mabati na misumari ili tusiwe na adha ya malighafi hii kwa sababu tunayo, tuitumie ili wananchi wa Mkoa wa Njombe, kule Ludewa na Tanzania kwa ujumla ili tuweze kunufaika nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Liganga na Mchuchuma tumeanza kuuzungumza tangu mwaka 2015. Hivi sasa ni takribani miaka saba. Kwa kweli naomba kama Mheshimiwa Rais alivyoelekeza, Serikali tufanye haya mazungumzo haraka ili tuweze…

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Neema Mgaya.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Neema Mgaya kwamba mradi huu siyo tu kwamba tumeanza kuuzungumza toka mwaka 2015 bali pia ulikuwa ni sehemu ya miradi ya kimkakati katika Taifa letu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema unapokea hiyo taarifa?

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naipokea taarifa kwa mikono miwili kwa sababu alichokisema ni uhalisia kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi wa Liganga na Mchuchuma ukifanya kazi, nimeshazungumza mara nyingi sana ndani ya Bunge hili, tangu mwaka 2010, takribani miaka 12 nazungumza suala la Lianga na Mchuchuma. Kila Bajeti ina maana nimezungumza zaidi ya mara 20 ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna reli ya kisasa ambayo tunatengeneza. Kama mradi huu ungekuwa tayari umeshaanza kazi, ina maana tungetumia chuma kwa bei nafuu kuliko vyuma ambavyo vinaagizwa kutoka nje. Lakini nipende tu kukwambia na niiambie Serikali kwamba, wanasayansi ulimwenguni wako busy kuumiza kichwa kuangalia namna gani watapata nishati mbadala ya makaa ya mawe. Kumbumbuka kwenye Liganga na Mchuchuma kuna makaa ya mawe. Na kama wako busy kutafuta nishati mbadala ya makaa ya mawe kwa sababu tu ya kulinda mazingira ili kumaliza mambo ya air pollution; na inasadikika kwamba baara ya miaka 10 haya makaa ya mawe nchi nyingi hayatokwenda kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hofu yangu ni kwamba, yasije kutokea kama yale yaliyotokea kwenye mkonge.

Wakati tuko tayari kuzalisha hayo makaa ya mawe ndipo hapo nchi sasa hazihitaji tena. Soko tena halipo na yale makaa sasa yanakuwa hayana maana tena. Kwa hiyo, bado naendelea kuisisitiza, Serikali mmalize hayo mazungumzo ili tuwe ndani ya muda. Serikali itambue kwamba dunia haitusubiri, dunia haitusubiri, dunia inakwenda kasi hivyo lazima na sisi twende kasi ili tuweze kwenda sambamba na dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, lakini vilevile kumpongeza. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni msikivu, lakini vilevile ni mlezi. Tulizungumza sana hapa masuala ya destination inspection na pre-arrival inspection; na juzi kwenye moja ya mikutano yake ametoa maelekezo kwa Serikali, kwamba waangalie system ya high breed atakayejisikia kufanya ukaguzi nje ya nchi sawa, atakayejisikia kufanya ukaguzi wa gari lake ndani ya nchi sawa. Hii inadhihirisha jinsi gani Mama alivyo mlezi na jinsi gani Mama anavyotaka kila mtu afanye mambo kutokana na vile anavyojisikia bila kuvunja sheria za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais na ninaomba hayo maelekezo Mheshimiwa Rais aliyoyatoa Wizara hii ifanyie kazi haraka na wale watakaojisikia kufanya destination inspection wataendelea na wale ambao wanataka pre-arrival inspection wataendelea ili mradi tu kila mtu aweze kufanya mambo yake kwa uhuru na kuweza kuona namna gani inaleta tija kwa huduma atakayoipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.